Rais wa Yemen aahidi kujibu mashambulizi
4 Juni 2011Rais Saleh ambaye kwa miezi kadhaa amekuwa anakabiliwa na upinzani dhidi ya utawala wake, alijeruhiwa kidogo kisogoni. Serikali ya Rais Saleh inalishutumu kundi hilo la kikabila linaloongozwa na Sheikh Sadiq al-Ahmar kuhusika na shambulio hilo.
Katika taarifa iliyotolewa jana jioni, Rais Saleh ambaye anatibiwa katika hospitali ya wizara ya ulinzi mjini Sanaa, amesema anaendelea vizuri na kuongeza kusema kuwa mashambulio hayo yamewaua watu saba.
Wakati huo huo, Ujerumani leo imeamuru kufungwa kwa ubalozi wake nchini Yemen na kurudishwa haraka kwa wafanyakazi wake kutokana na machafuko yanayoendelea nchini humo.
Taarifa ya wizara ya mambo ya nchi za nje imesema japokuwa mapigano kwenye mji mkuu wa Sanaa hayawalengi raia wa kigeni, hatari iliyopo ndiyo imeisababisha wizara hiyo kuchukua uamuzi huo.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFP)
Mhariri: Mohamed Dahman