Rais wa Sudan Omar Hassan al-Bashir azuru Darfur | Matukio ya Kisiasa | DW | 23.07.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Rais wa Sudan Omar Hassan al-Bashir azuru Darfur

Rais wa Sudan Omar Hassan al-Bashir anafanya ziara katika jimbo lenye machafuko la Darfur, magharibi mwa Sudan. Ziara hiyo imefanyika huku tuhuma za ukiukwaji wa haki za binaadamu zinazomkabili zikizidi kutatanisha.

Rais wa Sudan Omar Hassan al-Bashir

Rais wa Sudan Omar Hassan al-Bashir

Rais Omar Hassan al-Bashir atakuwa na ziara ya siku mbili katika jimbo hilo lenye machafuko la Darfur, magharibi mwa Sudan. Ataitembelea miji mikuu ya maeneo matatu yanayounda jimbo hilo la Darfur ikiwa ni pamoja na El-Fasher upande wa kaskazini, Nyala kusini na El Geneina upande wa magharibi mwa jimbo hilo. Mabolizi na wawakilishi wa mashirika ya kigeni wamealikwa kushiriki katika ziara hiyo. Balozi wa Uingereza nchini Sudan Rosalind Marsden yeye amekubali mualiko huo akisema kwamba hawajui atakachokizungumzia rais al-Bashir, na bora wakuwepo bila hata hivyo kubadili msimamo wa nchi yake kwamba rais al-Bashir afikishwe mbele ya mahakama.

Hatua hiyo ya kumshtaki rais al-Bashir kwa mauaji ya kuangamiza jamii, uhalibifu wa kivita na makosa dhidi ya binaadamu ambayo ilitolewa na mwendeshamshtaka mkuu wa mahakama ya kimataifa ya jinai ya mjini The Hague Uholanzi Luis Moreno Ocampo, imezidi kutatanisha na kuleta migawanyiko.

Kwanza kabisa Umoja wa Afrika ungependa hatua hiyo isimamishwe kuuokoa mpango wa amani nchini Sudan. Mkuu wa mawasiliano kwenye Baraza la amani na usalama la Umoja wa Afrika Hassan Ba, amekubusha hivyo katika mkutano na waandishi wa habari mjini Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia na makao makuu ya Umoja wa Afrika:´´Umoja wa Afrika umechukuwa msimamo wake kwamba kama mwanachama wetu tumeshikamana na Sudan na tunaomba Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa atumie kipengele cha 16 kuahirisha hatua yile kwa mwaka moja. Umoja wa Afrika kwa upande wake ufanye juhudi kuhakikisha kwamba mpango wa kusaka amani unasonga mbele na wanaokiuka haki za binaadamu wamefikishwa mbele ya sheria. Kwa hiyo nia yetu hapa ni kutovuruga mpango wa amani nchini Sudan´´.

Hayo ndio maoni yake pia makamu wa rais wa Sudan kutoka kundi la waasi wa zamani wa kusini la SPLA Salva Kiir ambae jana akiwa ziarani nchini Uganda alisema ´´vizuri wasiharakishe kumkamata rais al-Bashir, pawe kwanza mashauriano ya kutosha´´.

Msimamo huo wa Umoja wa Afrika na viongozi wa kiafrika kwa jumla, ni tofauti na ule wa nchi za magharibi kama Marekani na nchi za Umoja wa Ulaya ambazo zinaunga mkono hatua ya mwendeshamashtaka mkuu wa mahakama ya kimataifa ya jinai ya mjini The hague Uholanzi, Luis Moreno Ocampo. Kwenye Baraza la usalama la Umoja wa amataifa, nchi mbili miongoni mwa zile nchi tano wanachama wa kudumu Rashia na China zinapinga.

Katibu mkuu wa Umoja wa nchi za kiarabu Arab Ligue Amr Mussa kwa upande wake, amesema serikali ya Sudan imekubali pendekezo la Umoja wa nchi za kiarabu la kuunda mahakama maalum za kuchunguza na kushughulikia visa vya ukiukwaji wa haki za binaadamu katika jimbo la Darfur kwa ushirikiano na Umoja wa mataifa, Umoja wa Afrika na Umoja wa nchi za kiarabu.


 • Tarehe 23.07.2008
 • Mwandishi Nijimbere, Gregoire
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EiYk
 • Tarehe 23.07.2008
 • Mwandishi Nijimbere, Gregoire
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EiYk
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com