Rais wa Pakistan atia saini kuridhia sheria kali za kiislam | Matukio ya Kisiasa | DW | 14.04.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Rais wa Pakistan atia saini kuridhia sheria kali za kiislam

Rais Asif Ali Zardari wa Pakistan ametia saini makubaliano ya kutumika kwa sheria kali za kiislam yyani sharia eneo la bonde la Swat linalodhibitiwa na wanamgambo wanaoungwa mkono na Taliban.

Rais Asif Ali Zardari

Rais Asif Ali Zardari

Hatua hiyo ya Rais Zardari ni katika juhudi za kumaliza mashambulizi ya wanamgambo wa Kitaliban, ingawaje kwa upande wa pili inazua shakashaka kuwa huenda ikachochea kuongezeka kwa imani za siasa kali.


Hatua hiyo ya Rais Zardari ni kukamilisha makubaliano yenye utata kati ya serikali yake na kundi la kikabila linaloungwa mkono na wataliban ambalo linaongoza maelfu ya wanamgambo katika vita dhidi ya majeshi ya Marekani nchini Afghanistan.


Karte Taliban

Eneo la Bonde la Swat

Sheria hiyo inaihusu wilaya ya Malakanda ambako kuna kiasi cha watu millioni tatu, wilaya ambayo iko katika jimbo linalojumuisha pia bonde la Swat.


Serikali kuu ya Pakistan ilipoteza udhibiti wa bonde hilo la Swat, baada ya kiongozi wa kikabila Maulana Fazlullah kuanzisha harakati za kutaka kuwekwa kwa sheria zinazofuatwa na wataliban, yaani sheria kali za kiislam.


Katika harakati hizo wanamgambo wake waliwachinja watu waliyokuwa wakipinga, kulipua mashule na kusababisha maelfu ya watu kuyakimbia makazi yao.

Bonde la Swat hapo kabla lilikuwa ni kituo maarufu cha utalii kwa michezo ya kuteleza katika barafu pamoja na vito vya thamani nchini Pakistan.


Waziri wa Mambo ya Ndani wa Pakistan Rehman Malik akizungumzia hatua hiyo ya kutiwa saini sheria hiyo, alisema kuwa kwa uwezo wa mwenyezimungu ana matumaini italeta matunda mazuri katika eneo hilo la Swat.


Amesema kuwa anategemea wale wote waliyokuwa wakitaka kuwepo kwa sheria hiyo, watasalimisha silaha zao na kufanya hali iwe ya amani.


Hata hivyo wakosoaji wanasema kuwa mpango huo unafungua mlango kwa itikadi za kitaliban kusambaa nchini Pakistan, huku shutuma zikiendelea kutolewa baada ya kuonyeshwa kwa mkanda wa video unaomuonesha mwanamke mmoja akichapwa viboko hadharani.


Msemaji wa kundi la wazee wakikabila wanauliunga mkono kundi la Taliban, ambaye alitia saini makubaliano hayo, Soofi Mohammad amesema kuwa hatua ya Rais Zardari kutia saini, itachangia hali kuwa ya amani katika bonde hilo la Swat, ambalo liko kiasi cha kilomita 160 kutoka mji mkuu wa Pakistan Islamabad.


Amesema kuwa watafanya kila lililo ndani ya uwezo wao kuhakikisha amani inarejea katika eneo hilo.


Kwa upande mwengine msemaji wa Taliban katika bonde la Swat Muslim Amir amesema kuwa kwa hatua hiyo hakuna haja tena ya kuendelea na mashambulizi.


Chini ya sheria hizo, wanawake hawataruhusiwa kwenda kazini au sokoni kwani hawaruhusiwi kuonekana hadharani, na kuongeza kuwa wataanza kuweka ratiba ya mafunzo ya kiislam katika shule.


Mahakama za kiislam zimekuwa zikifanyakazi katika eneo hilo la bonde la Swat toka mwezi uliyopita, lakini matumuzi haswa ya sheria za kiislam yalikuwa katika mjadala.


Obama in Baden-Baden

Rais Barack Obama

Pakistan ambayo Rais Barack Obama wa Marekani ameipa umuhimu katika vita dhidi ya al Qaida inakabiliwa na mbinyo mkubwa unaoitaka kupambana na watu wenye imani kali za kidini, lakini serikali ya nchi hiyo imesema kuwa majadiliano ndiyo njia nzuri ya kufikiwa kwa amani.


Jeshi lake linakabiliwa na uhaba wa vifaa kuweza kukabiliana na wanamgambo wa ndani, na pia unasaba wake na Marekani umeendelea kuifanya kupoteza umaarufu miongoni mwa wananchi wake.


Maeneo ya kaskazini magharibi ndiyo yamekuwa yakikabiliwa na ghasia na mashambulizi mengi.Maeneo hayo ndiko walikokimbilia wapiganaji wa Al Qaida na Taliban baada ya kurushwa kutoka Afghanistan mwaka 2001 kufuatia uvamizi wa majeshi ya Marekani.


Zaidi ya watu 1,700 wameuawa toka mwezi July 2007 ambapo zaidi ya wanajeshi 1,500 wa serikali wameuawa toka mwaka 2002 kutokana na mashambulizi ya wanamgambo.

Mwandishi:Aboubakary Liongo

Mhariri.Saumu Mwasimba


 • Tarehe 14.04.2009
 • Mwandishi Aboubakary Jumaa Liongo/AFP
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/HWbg
 • Tarehe 14.04.2009
 • Mwandishi Aboubakary Jumaa Liongo/AFP
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/HWbg
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com