Rais wa Iran ziarani Iraq. | Matukio ya Kisiasa | DW | 03.03.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Rais wa Iran ziarani Iraq.

Rais wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad leo ameingia katika siku ya pili ya ziara yake nchini Iraq, ambapo lengo la ziara hiyo ni kuimarisha ushirikiano wa nchi hizo mbili hasa kiuchumi.

Rais Mahmoud Ahmadnejad wa Iran na mwenzeye wa Iraq Jalal Talaban, mjini Baghdad.

Rais Mahmoud Ahmadnejad wa Iran na mwenzeye wa Iraq Jalal Talaban, mjini Baghdad.

Akiwa nchini humo, Rais Mahmoud Ahmadinejad alitembelea eneo linalotukuzwa na madhehebu ya shia la Imam Musa Kadhim mjini Baghdad na kuswali .

Hata hivyo kiongozi huyo wa Iraq, huko hakuongozana kiongozi yoyote mwandamizi wa Iraq na kwamba alipokelewa na kiongozi wa utawala wa eneo hilo.

Rais wa Iran aliwasili jana nchini Iraq katika ziara ya kwanza na ya kihistoria kwa kiongozi wa Iran.

Leo Rais huyo wa Iran atasimamia kutiwa saini kwa makubaliano ya kuimarisha mshikamano wa kiuchumi kati ya nchi hizo.

Maafisa wa Iraq wanasema takriban mapatano 10 yatasainiwa katika ziara hiyo ya kwanza kwa kiongozi wa Iran tangu aliyekuwa Rais wa Iraq, Saddam Hussein kuanzisha vita vilivyodumu kwa miaka minane katika miaka ya 80, ambavyo vilisababisha watu milioni kuuawa.

Mikataba itakayosainiwa ni pamoja na inayohusu ushirikiano katika masuala ya usafiri ikiwemo reli, usafiri wa majini na uchukuzi wa mizigo.

Katika siku yake ya kwanza ya ziara nchini humo Rais wa Iran alisema, ziara hiyo ni ya kwanza kwa kiongozi wa kwanza katika eneo hilo la mashariki ya kati, tangu Marekani ilipoongoza uvamizi nchini humo mwaka 2003, na kufungua ukurasa mpya wa mahusiano kati ya Iran na Iraq.

Mwaka huu unafikisha maadhimisho ya miaka 20 tangu kuzuka kwa vita vya Iran na Iraq.

Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa ziara ya Rais Ahmadnejad inaonesha kukuwa kwa ushawishi wa Iran katika eneo hilo na kwamba uwepo wake Baghdad kama mgeni wa serikali ya Iraq, kuna shusha madai ya Marekani kwamba nchi hiyo imekuwa ikichochea ghasia nchini Iraq kwa kuunga mkono wanamgambo wa kishia.

Rais AhmadNejad jana aliitolea maneno makali Marekani, nchi ambayo ina zaidi ya wanajeshi laki moja na elfu 50 nchini Iraq, kwa kuisema kuwa inawajibika kwa kukuza ugaidi katika eneo hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukutana na kiongozi wa siasa wa Kishia Abdul Aziz al Hakim, Rais wa Iran alisema miaka sita iliyopita katikia eneo hilo hakukukuwa na masuala ya ugaidi.

Aidha jana Rais wa Iran, alikana shutuma zilizotolewa dhidi ya nchi yake na Rais George w Bush wa Marekani, kwamba Iran inaunga mkono na kufadhili wapiganaji wa kishia, walioko Iraq ambao wanaua wanajeshi wa Marekani.

Alisema kitendo cha Rais Bush kutoa lawama, bila ushahidi wowote kinaongeza matatizo katika eneo hilo na kwamba hakitatatua matatizo hayo.

Aliwataka Wamarekani kuelewa ukweli katika eneo hilo, kwamba watu wa Iraq hawaipendi Marekani.

Ahmadnejad anayejulikana kwa uzungumzaji wake, ameonekana ni mtu wa kujizuia kufanya hivyo wakati wa ziara yake hiyo nchini Iraq, licha ya kuikosoa kwa utaratibu Marekani, hali ambayo inaonekana kutotaka kumuudhi mwenyeji wake Iraq.

Hata hivyo ziara hiyo Rais wa Iran nchini humo imepokelewa kwa hisia tofauti na Wairaq wenyewe, hasa wa madhehebu ya Shia, ambao ndio waliokuwa watawala wakati wa uongozi wa Saddam Hussein.

Nchi zote mbili Iraq na Iraq zimekuwa na jamii ya washia, lakini Iraq ni warabu na Iran ni waajemi.

Ziara hiyo ya Rais wa Iran mbali ya kupingwa na Wasuni, lakini pia ilipokelewa vizuri katika mji mtakatifu wa Najaf.

Wakati huohuo Watu 15 wameuawa na wengine 45 wamejeruhiwa baada ya bomu la kutegwa barabarani kulipuka karibu na jengo la wiraza ya kazi mjini Baghdad.

Maafisa wa usalam nchini humo wamearifu kuwa waliojeruhiwa ni pamoja na wafanyakazi wa wizara hiyo na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Baghdad kilicho jirani na shambulio lilipotokea.

 • Tarehe 03.03.2008
 • Mwandishi Nyanza, Halima
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DGzD
 • Tarehe 03.03.2008
 • Mwandishi Nyanza, Halima
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DGzD
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com