Rais Obama atetea mpango wake wa kunyanyua uchumi wa Marekani | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 25.03.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Rais Obama atetea mpango wake wa kunyanyua uchumi wa Marekani

Serikali ya Marekani imesisitiza kuwa inafanya juhudi zote kupambana na athari za msukosuko wa kiuchumi katika nyanja zote.

default

Rais Barack Obama akifanya mkutano wake wa pili na waandishi wa habari

Katika hotuba yake ya pili tangu kuingia madarakani Rais Obama alitetea mkakati mpya wa serikali yake ulio na azma ya kuukwamua uchumi wa Marekani. Ifahamike kuwa mkutano wa kilele wa kiuchumi G20 umepangwa kufanyika tarehe mbili mwezi ujao. Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Rais Obama kukutana na viongozi wa mataifa makubwa kiuchumi.


Katika hotuba yake ya pili na waandishi wa habari tangu kuingia madarakani Rais Obama alisisitiza kuwa uamuzi wa serikali yake tayari umeanza kuwa na mafanikio na ndio msingi wa ufanisi wa kiuchumi


''Tuna uwezo wa kushughulikia matatizo ya bajeti ambayo kwa sasa hayajapata suluhu kamilifu katika mpango uliopo ila hatua zimepigwa. Katika mfumo mzima wa mabenki tutalazimika kufanya mabadiliko zaidi ila tunafuata mkondo wa sawasawa ''


Bajeti hiyo inapingwa vikali na wafuasi wa chama cha Republican wanaodai kuwa itasababisha nakisi kubwa.

Itakumbukwa kuwa mwanzoni mwa wiki hii serikali ya Marekani ilipitisha uamuzi wa kutumia dola bilioni 180 kuiokoa kampuni ya kimataifa ya bima ya AIG. Punde baada ya hatua hiyo kampuni hiyo iliwatunuku maafisa wake wa ngazi za juu kiasi cha dola milioni 165 jambo lililozua mitazamo tofauti.


Waziri wa Fedha wa Marekani Timothy Geithner aliyetangaza mwanzoni mwa wiki hii mpango mpya wa kuyanusuru mabenki ameeleza kuwa mtikisiko huo wa kiuchumi umedhihirisha kuwa sheria za biashara nchini humo zina mapungufu.


''Msukosuko huu wa kiuchumi umeweka bayana kuwa kuna mapungufu katika sheria za kusawazisha biashara kwenye masoko ya fedha. Ukosefu wa mamlaka maalum ya kushughulikia suala hilo katika taasisi za fedha zisizotoa huduma za benki umechangia katika matatizo haya na hilo litaendelea kuathiri uwezo wetu wa kutafuta suluhu.''Kwa upande mwengine China nayo pia imeongezea uzito kauli za Rais Obama na washauri wake wa benki kuu wanaripotiwa kusema kuwa uchumi wa nchi hiyo ulio wa tatu kwa ukubwa kote ulimwenguni huenda umepata ahueni tangu mwishoni mwa mwaka uliopita.

Hata hivyo kulingana na viashiria vyote uchumi wa Marekani na ulimwengu kwa jumla utaendelea kudorora kwa muda mrefu nayo mataifa yanayotegemea kuuza bidhaa nje hayatapata ahueni katika kipindi kifupi kijacho.

Kutokana na hilo biashara katika bara la Ulaya nayo huenda ikastawi kwa kasi ndogo sana wakati ambapo tathmini ya hali ya biashara ya hapa Ujerumani IFO ikisubiriwa mwezi huu. Kwa mujibu wa wataalam biashara inatabiriwa kuwa itapungua.

Rais Obama kadhalika hakuzipa uzito mkubwa hisia zinazoashiria mgawanyiko katika suala zima la kuunyanyua uchumi wa ulimwengu. Viongozi wa bara la Ulaya wamepinga mapendekezo yaliyotolewa na Marekani ya kutumia fedha zaidi kuokoa uchumi. Badala yake viongozi hao wamesisitiza umuhimu wa kuweka sheria madhubuti za usimamizi wa fedha.Waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown anasisitiza kuwa ''katika juhudi za kulinda fedha zilizochangishwa na wateja sharti tuhakikishe kuwa sheria madhubuti zinadumishwa barani Ulaya sio tu katika nchi moja bali pia katika mabara mengine kote ulimwenguni''.


Shirika la Fedha Ulimwenguni IMF liliamua kubadili mfumo wake wa mikopo kwa mataifa yaliyo na uchumi uliostawi kwani ndiyo yaliyoathirika zaidi na mtikisiko wa kiuchumi.

Mwandishi:Thelma Mwadzaya

Mhariri:Josephat Charo

AFPE/RTRE

DW inapendekeza

 • Tarehe 25.03.2009
 • Mwandishi Thelma Mwadzaya
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/HJCn
 • Tarehe 25.03.2009
 • Mwandishi Thelma Mwadzaya
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/HJCn
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com