Obama afanya mkutano wa kwanza na waandishi wa habari | Matukio ya Kisiasa | DW | 10.02.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Obama afanya mkutano wa kwanza na waandishi wa habari

Rais Barack Obama wa Marekani ametaka kupitishwa haraka kwa mpango wa kuupiga jeki uchumi wa nchi hiyo

default

Rais Barack Obama

Rais Barack Obama amesema hayo katika mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari toka aingie madarakani siku 20 zilizopita


Akizungumza mnamo wakati ambapo mpango wake huo wa kuupiga jeki uchumi wa Marekani wenye thamani ya dola billioni 850 ukisubiriwa kupigiwa kura na seneti hii leo Rais Obama ameonya kuwa kucheleweshwa kwa mpango huo kunaweza kusababisha hali kuwa mbaya zaidi.


Amesema kuwa kutokana na hali iliyovyofikia hivi sasa ambapo sekta binafsi iko hoi, ni serikali pekee ndiyo itakayoweza kuunusuru uchumi kutoka katika hali ngumu iliyonayo.


´´Katika kipindi hiki ambapo sekta binafsi imedhoofishwa na mgogoro huu wa uchumi, serikali ndiyo chombo pekee kilichobakia na uwezo wa kuurejesha katika uhai uchumi wetu.Ni serikali tu itakayoweza kubadilisha hali ya watu kupoteza ajira zao na hicho ndicho ambacho mpango unaopitishwa na Congress umepanga kukifanya´´


Saa chache kabla ya mkutano huo wa Rais Obama na waandishi wa habari, baraza la seneti lilipiga kura kumaliza mjadala juu ya kuupitisha mpango wa kuupiga jeki uchumi na sasa kinachosubiriwa ni kura ya kuupitisha.


Wiki iliyopita Baraza la Wawakilishi liliupitisha mpango wa kuupiga jeki uchumi wenye thamani ya dola billioni 819.


Rais Obama ambaye aliingia madarakani kwa ahadi ya kuleta mabadiliko baada ya miaka minane ya utawala wa George Bush, katika mkutano wake huo wa kwanza na waandishi wa habari aliashiria dhamira yake ya kuendelea kuondoa mfumo na sera za utawala uliyopita ikiwemo hekima ya kuwa na mazungumzo na maadui wa Marekani.


Akijibu swali juu ya mtizamo wake kuhusiana na uhusiano kati ya Marekani na Iran, Rais Obama amesema kuwa anategemea kutumia kila aina ya uwezo ambao Marekani inao ikiwemo diplomasia kujadiliana na Iran na akaonesha azma ya kuwepo kwa mazungumzo ya ana kwa ana na Tehran.


´´Ni lazima tuchukue mwelekeo wa kukabiliana na Iran utakaohusisha njia zote na hii inajumuisha diplomasia,na mategemeo yangu ni kwamba katika miezi ijayo tutakuwa katika nafasi ya kuweza kuanza kukaa ana kwa ana katika meza ya mazungumzo ya awali ya kidiplomasia ambayo yataturuhusu kutekeleza sera zetu katika mwelekeo mpya´´


Kauli hiyo ya Rais Obama imekuja mnamo wakati ambapo kiongozi wa Bunge la Iran Ali Larjani ameitaka Marekani kuwasilisha mapendekezo yaliyowazi kwa nchi yake na kuongeza kuwa Iran haitaingia katika majadiliano kwa msingi wa majadiliano tu bali kwa msingi wa kufikia suluhisho thabiti.


Larjani alisema hayo baada ya kukutana na Waziri Mkuu wa Uhispania Jose Luis Rodriguez Zapatero mjini Madrid.


Ikumbukwe ya kwamba sera za mtangulizi wa Rais Obama, George Bush zilikuwa ni kutaka kutengwa kwa Iran, mzozo ukiwa ni mpango wake wa nuklia.Rais Obama pia katika mkutano huo alisema kuwa hakuna shaka ya kwamba magaidi wa al Qaida na Taliban wanalitumia eneo la mpaka wa Afghanistan na Pakistan kama maficho yao salama na kwamba hatoruhusu hali hiyo kuendelea.


´´Tutahitaji ushirikiano zaidi katika juhudi za kijeshi, kidiplomasia, kimaendeleo na kieneo, ili kufanikisha malengo.Hili ni eneo ambalo lilitumika kama ngome ya kuanzishia mashambulizi ya septemba 11 yaliyowaua wamarekani elfu tatu.Hatuwezi kuruhusu al-Qaida waendelee na ugaidi wao, siwezi kuruhusu al-Qaida au Bin Laden kutumia eneo hilo kupanga mashambulizi dhidi ya Marekani´´


Aidha kuhusiana na uhusiano wa Marekani na Urusi, Rais Obama alisema nchi hizo mbili ni lazima zioneshe njia ya kuelekea katika uzuiaji wa kusambaa kwa silaha za nuklia, kwa kurejea tena katika mazungumzo baina yao ya kupunguza silaha za atomik


 • Tarehe 10.02.2009
 • Mwandishi Aboubakary Jumaa Liongo/AFP/CNN
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GqfB
 • Tarehe 10.02.2009
 • Mwandishi Aboubakary Jumaa Liongo/AFP/CNN
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GqfB
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com