Rais aliyepinduliwa wa Honduras arejea kwa siri nyumbani | Matukio ya Kisiasa | DW | 22.09.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Rais aliyepinduliwa wa Honduras arejea kwa siri nyumbani

Walimwengu watoa mwito mzozo wa Honduras ufumbuliwe kwa amani

default

Rais aliyepinduliwa wa Honduras Manuel Zelaya

Rais aliyetimuliwa madarakani nchini Honduras,Manuel Zelaya amerejea kwa siri nyumbani mjini TEGUCIGALPA na kuwataka wanajeshi washamiri silaha zao dhidi ya "maadui wa umma",huku akielezea utayarifu wake wa kuzungumza na serikali.

Manuel Zelaya amepokelewa kwa shangwe aliporejea nyumbani, na wapinzani wake sio tuu hawakuweza kumzuwia,hata kujua kama karejea hawakujua.Hivi sasa Manuel Zelaya amekimbilia katika ubalozi wa Brazil akiwaacha wafuasi wake nje wakimshangiria.

"Vikosi vya jeshi vinastahiki kushamiri silaha zao dhidi ya maadui wa umma na sio dhidi ya umma" amesema rais huyo aliyepinduliwa na kuongeza:

"Nnawataka viongozi walioko madarakani wasitumie nguvu.Tunabidi tusake njia ya kumaliza mzozo."

Manuel -Mel-Zelaya amerejea nyumbani katika wakati ambapo viongozi wa ulimwengu mzima wanatazamiwa kuhudhuria mkutano wa hadhara kuu ya Umoja wa mataifa mjini New-York.

Wakiduwaa kwa kurejea nyumbani rais huyo aliyepinduliwa,viongozi walioingia madarakani nchini Honduras wamepitisha hatua za aina peke.Rais wa mpito Roberto Micheletti ametangaza amri ya kutotoka ovyo-viwanja vya ndege vinne vya kimataifa vimefungwa na kuitaka Brazil imtoe Manuel Zelaya apate kuhukumiwa.

Hapo awali,Manuel Mel Zelaya,akijitokeza na kofia yake ya Texas,aliwatolea mwito wananchi wa Honduras wateremke kwa wingi mjini TEGUCIGALPA ili kuishinikiza serikali ya mpito iheshimu katiba.

Mamia ya wafuasi wake walioitika mwito huo na kumiminika mbele ya ubalozi wa Brazil, walijikuta wakitimuliwa na polisi.Ripota wa shirika la habari la Reuters aliyekua karibu na ubalozi wa Brazil mjini Tegucigalpa amesema polisi wamefyetua gesi za kutoa machozi dhidi ya waandamanaji na kwamba mabomu yasiyopungua mawili ya kutoa machozi yameangukia katika ubalizi wa Brazil.

Akihojiwa na kituo cha televisheni cha Venezuela Zelaya amesema Ubalozi wa Brazil umezungukwa na polisi na wanajeshi na anahofia visa vibaya zaidi vya matumizi ya nguvu akisisitiza tunanukuu"wanajeshi wanaweza kuuvamia ubalozi wa Brazil."Mwisho wa kumnukuu.

Manuel Zelaya aliyepinduliwa na wanajeshji June 28 mwaka huu na kukimbilia uhamishoni nchini Nicaragua amekiambia kituo cha televisheni cha Canal 11,amewasiliana na viongozi wa serikali ya mpito .

Konfrontation in Tegucigalpa

Jeshi lafyetua gesi za kutoa machozi

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani,Hillary Clinton anasema kurejea nyumbani Zelaya ni fursa ya kuupatia ufumbuzi mzozo wa Honduras.Bibi Hillary Clinton ameendelea kusema:

"Cha muhimu zaidi kwa sasa ni kuhakikisha kwamba uamuzi wa kurejea nyumbani rais Zelaya haupelekei kuzidi makali ugonvi au matumizi ya nguvu,badala yake unasaidia kupatikana njia ya kuufumbua mzozo uliopo kwa njia ya amani."

Umoja wa Ulaya pia umezitolea mwito pande zote zinazohusika zisake ufumbuzi kwa njia ya mazungumzo.

Mwandishi Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters

Mhariri:M-Abdul-Rahman

 • Tarehe 22.09.2009
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Jmaf
 • Tarehe 22.09.2009
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Jmaf

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com