Rais Abdullahi Yusuf wa Somalia kujiuzulu | Matukio ya Kisiasa | DW | 24.12.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Rais Abdullahi Yusuf wa Somalia kujiuzulu

Rais Abdullahi Yusuf wa Somalia ameamuwa kujiuzulu na anatarajiwa kutangaza ku'gatuka kwake hauko hapo Jumamosi.

Rais wa serikali ya mpito ya Somalia Abdullahi Yusuf.

Rais wa serikali ya mpito ya Somalia Abdullahi Yusuf.

Tangazo hilo linakuja muda mfupi baada ya kujiuzulu kwa mwanasiasa aliemtuwa kuwa waziri mkuu wiki iliopita kusema kwamba alikuwa hataki kuwa kikwazo cha amani katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Hatua ya rais Yusuf inakuja wakati kukiwa na onyo la kusambaratika kwa serikali ya mpito ya Somalia.

Hussein Mohamed Mahmud msemaji wa rais ameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters leo hii kwamba rais tayari ameandika baruwa yake hio ya kujiuzulu na anatazamiwa kuitangaza Jumamosi inayokuja.

Ameongeza kusema kwamba haitokuwa vyema kwake yeye kutabiri au kuelezea sababu zake za kujiuzulu na kwamba Rais Yusuf ataelezea kila kitu wakati anapojiuzulu.

Yusuf alimteuwa Mohamed Mohamud Guled kushika wadhifa wa waziri mkuu baada ya kumtimuwa Waziri Mkuu Nur Hassan Hussein mapema mwezi huu lakini bunge na jumuiya ya kimataifa vilimuunga mkono Hussein na hiyo moja kwa moja kuifanya serikali hiyo ambayo tayari ni dhaifu kuwa na mawaziri wakuu wawili.

Tokea wakati huo rais amekuwa chini ya shinikizo zito la serikali ya Marekani kuzuwiya serikali ya mpito ya Somalia isisisambaratike na serikali za eneo hilo zilimmwekea Yusuf vikwazo wiki hii kwa kukwamisha mchakato wa amani unaosimamiwa na Umoja wa Mataifa.

Mfarakano kati ya Yusuf na Hussein umekuwa ukilaumiwa kwa kukwamisha mazungumzo ya amani na kutishia kuisambaratisha serikali hiyo inayoungwa mkono na mataifa ya magharibi wakati waasi wa itikadi kali za Kiislam wakiwa wamepiga kambi kwenye viunga vya mji mkuu wa Mogadishu.

Wachambuzi wa mambo wanaamini kwamba kambi za kisiasa zinazopingana zinaweza kufufuwa harakati za wanamgambo na kupelekea mapigano ya mitaani ambapo waasi wanapambana na vikosi vya Ethiopia na wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika.

Hussein yuko tayari kuwajumuisha Waislamu wa itikadi kali katika mchakato wa amani na kuwa na mazungumzo nchini Djibouti mwishoni mwa juma lililopita na kiongozi wa upinzani wa Waislamu wa msimamo wa wastani Sheikh Sharif Ahmed.

Mataifa ya magharibi na yale ya jirani na Somalia yameweka mtaji mkubwa sana wa kisiasa kwa serikali ya mpito ya Somalia na yamekatishwa tamaa kwamba serikali hiyo hadi sasa imethibitisha kwamba imeshindwa kufanya kazi.

Wanajeshi kutoka nchi jirani ya Ethiopia wamekuwa wakiipa nguvu serikali hiyo kwa miaka miwili iliopita lakini ina wanajeshi 3,000 waliobakia nchini humo na serikali ya Ethiopia imesema wataondoka nchini humo ifikapo mwezi wa Januari.

Katika repoti mpya iliochapishwa na Kundi la Kimataifa linalojishughulisha na migogoro duniani lenye makao yake makuu mjini Brussels Ubelgiji imeonya kwamba serikali hiyo ya mpito iko kwenye ukingo wa kusambaratika na imetowa wito wa kujumuishwa kwa Waislamu vichwa ngumu wa itikadi kali katika mchakato wa amani.

Waasi wa itikadi kali za Kiislam wanadhibiti takriban eneo zima la kusini mwa Somalia nje ya mji mkuu wa Mogadishu na Baidoa makao makuu ya serikali na wachambuzi wa mambo wanatabiri kwamba wataichukuwa Somalia nzima wakati vikosi vya Ethiopia vikiwa vimeondoka venginevyo wanajeshi zaidi wa kulinda amani wanapelekwa nchini humo.

 • Tarehe 24.12.2008
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GMYu
 • Tarehe 24.12.2008
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GMYu
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com