Putin na mkakati wa kubakia na nguvu za madaraka hata baada ya kuacha Urais. | Matukio ya Kisiasa | DW | 03.10.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Putin na mkakati wa kubakia na nguvu za madaraka hata baada ya kuacha Urais.

Rais wa Urusi Vladimr Putin, ametoa ishara ilio wazi kwamba atabakia kuwa na nguvu za kisiasa baada ya kipindi chake cha urais kumalizika mwaka ujao, lakini kufanya hivyo atahitaji kubadili taratibu za muda mrefu kuhusu namna madaraka yanavyodhibitiwa nchini humo.

Rais Vladimr Putin

Rais Vladimr Putin

Mapema juma hili Rais huyo wa Urusi alizusha mshangao mwengine akikubali ombi la chama kikubwa kabisa cha kisiasa nchini humo” Urusi ilioungana” kumtaka aongoze kundi la wagombea wake katika uchaguzi ujao wa bunge mwezi Desemba na kuashiria kwamba huenda akawa Waziri mkuu siku za usoni.

Katika taifa ambako kunafutiliwa kwa undani tetesi juu ya hali ya baadae ya Putin baada ya muda wake wa urais kumalizika mwishoni mwa 2008, matamshi ya rais huyo yametafsiriwa kuwa ni kielelezo cha jinsi atakavyobakia kuwa na usemi hata akiwa hayuko madarakani. Katiba Urusi haimruhusu kugombea urais kwa kipindi cha tatu.

Uhariri wa gazeti moja VEDOMOSTI ulikua na maneno ,”Kwa mara nyengine Putin ameonyesha uwezo wake wa kubadili mfumo wa kisiasa wa nchi bila ya kuirekebisha katiba.”Wawekezaji wameipongeza ishara ya kwamba Putin ataendelea kuwa na madaraka kuwa , kama ni dalili ya kwamba sera zilizosababisha mafanikio yasiotarajiwa ya kiuchumi kwa miaka minane iliopita yataendelea. Hisa zilipanda.

Pamoja na kuwepo kwa tatizo la rushwa na kuzidi uhuru wa vyombo vya habari na siasa za upinzani kuekewa mipaka ,wawekezaji kutoka nje wamepaata tija kutokana na kukua haraka kwa uchumi wa Urusi, jambo ambalo limeifanya nchi hiyo kuwa moja wapo ya masoko ya kuvutia duniani. Lakini wengine wameonya kwamba mkakati wa Putin pia una hatari zake kwa nchi ambayo imekua na mtindo wa madaraka kudhibitiwa na mtu mmoja.

Wakosoaji wa jinsi mkondo wa demokrasia unavyokwenda nchini humo, wataiona hali hii kuwa ni mfano wa kurudi katika ule mfumo wa iliokua urusi ya zamani-Soviet Union. Wakati ule mkuu wa taifa yaani rais alikua ni sawa na mkuu wa heshima tu, lakini madaraka yote yalikua mikononi mwa kiongozi wa chama cha Kikoministi.

Leo waziri mkuu ana madaraka ya kiwango fulani tu na hana usemi katika sera ya nje, wala idara ya usalama na upelelezi na anaweza kufukuzwa kazi na Rais wakati wowote. Huenda Putin ana azma ya kuufanya wadhifa wa waziri mkuu kuwa wenye madaraka zaidi.

Wadadisi wanaashiria kwamba huenda akajaribu kuyahamisha madaraka ya idara muhimu zenye nguvu kama idara ya upelelezi FSB katika ofisi ya waziri mkuu badala ya Ikulu. Kufanya mageuzi hayo Putin atahitaji theluthi mbili ya wabunge kuyaunga mkono na kuirekebisha katiba.

Ikitarajiwa kwamba Putin hatotafuta mbinu ya kubadili katiba ili agombee tena mhula wa tatu, atahitaji mtu mwenye uwezo na atakayeleta mabadiliko kuwa rais kabla ya yeye kuwa Waziri mkuu. Wakosoaji wake wanasema kwamba kwa vyovyote itakavyokua hivi sasa ni dhahiri kwamba

Putin pamoja na kuacha urais hatoachia madaraka. Alexei Venedictov , mhariri mku wa stesheni ya redio Ekho Moskvy alisema Ni wazi Putin hatoondoka na si muhimu ni wadhifa gani atakayoshika baadae, kwa namna yoyote ile ataondoka na madaraka yake ya kisiasa kushika wadhifa mpya.”

 • Tarehe 03.10.2007
 • Mwandishi Mohammed Abdul-Rahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CH7E
 • Tarehe 03.10.2007
 • Mwandishi Mohammed Abdul-Rahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CH7E

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com