Poroshenko ataka vikwazo zaidi kwa Urusi | Matukio ya Kisiasa | DW | 24.11.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Poroshenko ataka vikwazo zaidi kwa Urusi

Poroshenko na maafisa wakuu wa EU wakutana Brussels. Miongoni mwa ajenda ni vikwazo kwa Urusi, kuondolewa kwa lazima ya visa kwa raia wa Ukraine, demokrasia ya Ukraine pamoja na kukithiri kwa ufisadi nchini Ukraine

Rais wa Ukraine Petro Poroshenko anawashinikiza wakuu wa Umoja wa Ulaya kutilia mkazo vikwazo dhidi ya Urusi, wakati ambapo Umoja wa Ulaya ukitaka uhakikisho kutoka kwa Ukraine kuwa unafanya linalohitajika kupiga vita ufisadi.

Poroshenko na viongozi wa taasisi za Umoja wa Ulaya wameanza mkutano wa kilele leo mjini Brussels, wenye lengo la kutathmini uthabiti wa uhusiano kati ya Ukraine na Umoja wa Ulaya, kando na kujadili masuala ya sekta za demokrasia, nishati, biashara na usalama.

Kando na kutaka vikwazo dhidi ya Urusi kupewa kipaumbele hasa ikizingatiwa vikwazo dhidi yake kiuchumi vinakamilika mwisho wa Januari mwakani, ajenda nyinginezo kwenye mkutano ni kuondoa kipengee kinachohitaji raia wa Ukraine wawe na visa kuzuru nchi wanachama sawa na watu wanaozuru Ukraine.

Wiki jana, nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zilisema zitaidhinisha mpango huo ikiwa sheria madhubuti itapitishwa kuuruhusu Umoja wa Ulaya kuondoa kipengee hicho kikihitajika.

Maafisa wa EU Gipfel, Junker na Schulz

Maafisa wa EU Gipfel, Junker na Schulz

Akizungumzia suala la visa la Ukraine kabla ya mkutano huo, spika wa bunge la Umoja wa Ulaya Martin Schulz amesema: "Tuko tayari, tumeandaa kila kitu tulichotarajia hata kura katika kamati husika, kuhusu kuwa na visa huria na kwa upande mwingine kuondoa kipengee cha visa. Kila kitu kinachosalia kipo hapa kwenye baraza si katika bunge la Ulaya na ninatumai nchi wanachama zitapata suluhisho".

Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, Umoja wa Ulaya umeipa Ukraine takriban euro bilioni 3.5. pia ulizindua mchakato uliolenga kukuza demokrasia katika taifa hilo ambalo awali lilikuwa chini ya Jamhuri ya Muungano wa Soviet.

Lakini ufisadi uliokithiri umelemaza ukuaji wa nchi hiyo. Wanasiasa wawili wakuu wenye mawazo ya mageuzi walijiuzulu mapema mwezi huu wakidai kuhangaishwa.

Kando na hayo, uhusiano kati ya Ukraine na Urusi umeendelea kuwa tete, kufuatia hatua ya Urusi kuimega sehemu ya Crimea na kuunga mkono wapiganaji waliopo mashariki mwa Ukraine huku wakiiunga mkono Urusi.

Mapema leo, maafisa wa Urusi wamemzuilia nahodha wa zamani wa baharini kwa madai kuwa anafanyia Ukraine ujasusi nchini humo.

Rais Poroshenko na maafisa wa EU Johannes Johannes Hann na Cecilia Malmstrom

Rais Poroshenko na maafisa wa EU Johannes Johannes Hann na Cecilia Malmstrom

Leonid Parkhomenko anayezuiliwa katika jiji la Sevastopol anakabiliwa na mashtaka ya uhaini kwa kukusanya kisiri habari kuhusu kikosi cha kivita cha Urusi cha Black Sea Fleet na kuwasilishia idara ya ujasusi ya jeshi la Ukraine. Hayo yamesemwa na shirika la ujasusi la Urusi FSB.

Mapema wiki hii, Ukraine iliwakamata wanajeshi wawili wa Urusi walioingia katika eneo la mpaka wa Crimea linalodhibitiwa na Ukraine.

Urusi iliimega sehemu ya Crimea kutoka kwa Ukraine na kuifanya ngome ya kikosi chake cha baharini Black Sea miaka miwili iliyopita, baada ya Ukraine kumpindua mamlakani rais aliyeipendelea Urusi kufuatia maandamano ya kushinikiza kujengwa kwa uhusiano wa karibu na mataifa ya magharibi.

Moscow iliyoyashutumu mapinduzi hayo na kuyataja kuwa njama ya magharibi, iliamua kuunga mkono waasi wa Ukraine waliopo maeneo mawili makuu ya mashariki mwa nchi hiyo.

Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu 9000 wamefariki kutokana na mvutano kati ya nchi hizo mbili.

Mwandishi: John Juma/DPE/APE/RTRE

Mhariri: Josephat Charo

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com