1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama aongoza New Hampshire kwa uchunguzi wa maoni

7 Januari 2008

Kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni Barak Obama anaongoza kwa asilimia 10 dhidi ya Hilary Clinton katika kuwania uteuzi wa ugombea wa urais kwa tiketi ya chama cha Demokrat katika jimbo la uchaguzi la New Hampshire.

https://p.dw.com/p/Clab
Obama yuko mbele dhidi ya Clinton kwa asilimia 10 katika jimbo la New HampshirePicha: AP

Pia kwa mara ya kwanza kabisa wapiga kura zaidi wa New Hampshire wanamuona Obama kuwa mgombea wa chama cha Demokrat mwenye uwezo mkubwa wa kumshinda mgombea hasimu wa chama cha Republican ambapo uchunguzi wa maoni wa CNN na WMUR umempa Obama asilimia 42 dhidi ya asilimia 31 za Clinton kwa uwezekano wa kuteuliwa kuwa mgombea wa urais wa chama cha Demokrat katika jimbo la New Hampshire.

Katika mikutano ya hadhara ya kampeni kwenye jimbo hilo lote la kaskazini mashariki mwa Marekani Obama ameweza kufikisha ujumbe wake wa matumaini na mabadiliko ambapo amesema imani yake iko kwa vijana wa Marekani hata kama kila mtu anasema hawatoshiriki katika upigaji kura.

Katika kampeni hizo Obama pia amekuwa akimshutumu Mama Clinton mwenye umri wa miaka 60 kwa kutumia mbinu chafu. Obama mwenye umri wa miaka 46 ambaye anataraji kuwa Rais wa kwanza mweusi wa Marekani amesema kwamba kile wanachokishuhudia hivi sasa ni kwa serikali ya Marekani ikiwa katika tapa tapa zake za mwisho za kuzuwiya mabadiliko,kuvuruga ukweli na rekodi za watu pamoja na kubadili maneno.

Hilary Clinton mke wa aliyekuwa rais wa Marekani Bill Clinton ambaye wakati fulani alikuwa akiongoza kwa umashuhuri wa kukubalika kwenye jimbo hilo la kaskazini mashariki mwa Marekani inaonekana nyota yake kufifia wakati wapiga kura wakimkimbilia Seneta Obama kutoka jimbo la Illinois ambaye anaendeleza wimbi la ushindi kufuatia ule wa jimbo la uchaguzi la Iowa.

Clinton ambaye amekuwa akiiungwa mkono zaidi na wapiga kura watu wazima amekiri kwamba anawajibika na kutopata uungaji mkono mkubwa wa vijana na invyoelekea ameanza kuwavutia vijana katika kampeni zake kwa kusema kwamba anagombea urais ili kuurudisha tena mustakbali kwa ajili yao wote kwa watu wa umri wote lakini hususan kwa vijana wa Marekani,

Clinton amekuwa akiendesha kampeni kali za kumzuwiya Obama asinyakuwe jimbo la New Hampshire baada ya kumbwaga kwenye jimbo la Iowa wiki iliopita.

Clinton ambaye atafanya historia iwapo atachagulikuwa kuwa rais wa kwanza mwanamke Marekani amewataka wanachama wa Demokrat wamchaguwe mtendaji na sio msemaji ambapo amesema kuna tafauti kubwa kati ya kuzungumza na kutenda na kati ya kuahidi na kutekeleza.

Wakati huo huo wagombea wa chama cha Republican wamekuwa kwenye malumbano mengine ya kuwania kuteuliwa kwenye jimbo hilo la New Hampshire kwa tiketi ya chama chao ambapo mgombea Mitt Romney akimshambulia Seneta John McCain amesema hakuna njia ambayo kwayo Seneta McCain anaweza kwenda Hempshire na kusema kwamba yeye ni mgombea mwenye kuwakilisha mageuzi kijembe ambacho McCain alikijibu kwa kusema kwamba havutiwi pale mtu anapobadilsiha misimamo yake moja kwa moja kwa kila suala kuu.

Uchunguzi mpya wa maoni unaonyesha McCain anaongoza dhidi ya Romney kwa asilimia 34 dhidi ya 30.