1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu atoa utetezi wake juu ya uvamizi wa meli za misaada

9 Agosti 2010

Aishutumu Uturuki kuchangia kutokea kwa tukio hilo.

https://p.dw.com/p/OfO5
Waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu ashikilia msimamo wake kuwa wanajeshi wa Israel,walifuata utaratibu katika uvamizi wa meli za misaada ya kiutu,na kuieleza tume kuwa anaamini itabaini ukweli juu ya kauli yake.Picha: AP

Waziri mkuu wa Israel,Benjamin Netanyahu ametoa utetezi wake mbele ya kamati maalumu, inayochunguza tuhuma za uvamizi wa meli za misaada,na kusisitiza kuwa uamuzi wa jeshi la nchi hiyo dhidi ya wanaharakati hao,ulikuwa ni sahihi.

Katika utetezi wake mbele ya kamati hiyo iliyo chini ya Israel,Netanyahu pia ameilaumu Uturuki kwa kushindwa kuzizuwia meli za misaada ya kiutu kwa wakaazi wa Gaza,kwa kueleza kuwa ilichangia uamuzi wa Israel,kuzivamia meli hizo za misaada.

Tume inayosikiliza utetezi wa Waziri mkuu Benjamin Netanyahu,imeundwa na Bunge la nchi hiyo,ikiwa na wajumbe ambao wanaelezewa kuwa hawatoweza kuuliza maswali yatakayombana Waziri huyo,pia itamuhoji Waziri wa ulinzi Ehud Barack hapo kesho,ina wajumbe 5 na waangalizi 2 wa kimataifa.

Akionekana mwenye kujiamini, Netanyahu ameieleza tume hiyo kuwa ana imani kuwa mwisho wa uchunguzi wa tume hiyo,itabaini kuwa Serikali ya Israel jeshi lake,lilifuata utaratibu sahihi kabla ya kuamua kufanya uvamizi katika meli hizo za misaada,na kusababisha vifo vya wanaharakati 9,wa kituruki.

Netanyahu wakati akitoa utetezi wake,ameielezea serikali ya Uturuki kutochukuwa hatua yeyote katika kuhakikisha wanazizuwia meli 6 za misaada kuvuka kizuizi kilichowekwa na Israel huko Gaza,licha ya onyo lililotolewa hapo kabla na Israel,kuwa waandaaji wa misaada hiyo,wana mafungamano na kundi la Hamas.

Waziri Netanyahu amezidi kueleza kuwa hata hivyo alitoa maelekezo kwa jeshi la nchi hiyo,kutumia busara zaidi bila kusababisha umwagikaji damu wakati wa uvamizi huo,huku akikanusha kuwa hakukuwa na mahitaji ya dharura kwa wakaazi wa Gaza kama ilivyoelezwa hapo awalai na waandaaji wa misaada hiyo,na kufahamisha kuwa lengo lilikuwa lilikuwa kuvuka vizuizi vilivyowekwa na Israel,na kuchochea mtafaruku.

Hata hivyo,wachambuzi wamekosoa uundwaji wa tume hiyo,kutokana na kile kinachoelezwa kuwa Netanyahu pamoja na viongozi wengine 3 watakaohojiwa kufuatia uvamizi huo,hawatakumbana na maswali magumu,kutokana na chombo hicho kuwa chini ya serikali ya Israel.

Israel imekuwa ikisisitiza hapo kabla kuwa inayo haki ya kuzuia chombo chochote kuvuka vizuizi ilivyoweka katika ukanda wa Gaza,kutokana na kile wanachoeleza kuwa ni kuzuia silaha zínazoweza kutumiwa na kundi la Hamas,ambalo limeapa kuliangamiza taifa la wayahudi.

Wiki iliyopita,Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa,Ban Ki Moon,naye alitangaza kamati maalumu ya kuchunguza juu ya uvamizi huo,ambayo inatarajiwa kuanza kazi hapo kesho,na kuwajumuisha wawakilishi kutoka Israel na Uturuki,ili kuutafutia suluhu mgogoro baina ya mataifa hayo mawili.

Wakati huo huo,meli iliyohusika katika uvamizi huo,iliyokuwa katika msafara wa meli za misaada ya kiutu kwa wakazi wa Gaza,imewasili Uturuki siku ya Jumamosi,ambapo serikali ya nchi hiyo imeweka ulinzi mkali na kuzuia waandishi habari kuingia ndani ya meli hiyo.

Uturuki imeeleza kuwa meli hiyo,itakaguliwa na maafisa wa nchi hiyo,pamoja na wale wa umoja wa mataifa,ambao wameamua kuanza uchunguzi juu ya tukio hilo,ambalo lilisababisha jumuiya ya kimataifa kulilaani,na kutaka kuitishwa uchunguzi huru.

Mwandishi; Ramadhan Tuwa/AFPE

Mhariri;Miraji,Othman.