Netanyahu apongezwa na viongozi mbalimbali | Matukio ya Kisiasa | DW | 10.04.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Netanyahu apongezwa na viongozi mbalimbali

Viongozi mbalimbali duniani wamempongeza Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu baada ya kuchaguliwa tena katika uchaguzi wa bunge kwa muhula mwingine.

Viongozi mbalimbali duniani wamempongeza Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu baada ya kuchaguliwa tena katika uchaguzi wa bunge kwa muhula mwingine.

Kansela wa Austria Sebastian Kurz na Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi walikuwa miongoni mwa viongozi wa kwanza kutuma salamu za pongezi. Kurz amesema kuwa yuko tayari kushirikiana na Netanyahu katika siku zijazo kwa maslahi ya watu wa Israel na Austria. Aidha, katika ukurasa wake wa Twitter, Waziri Mkuu Modi amesema Netanyahu ni rafiki mkubwa wa India na ataendelea kushirikiana naye kwa lengo la kuufikisha mbali uhusiano wao.

Kwa upande wake Rais wa Marekani, Donald Trump amesema kuchaguliwa tena kwa Netanyahu ni ishara nzuri ya amani. Trump amezitoa pongezi hizo mjini Washington wakati akizungumza na waandishi habari.

Ujerumani: Tuna uhusiano mzuri na Israel

Ujerumani nayo imesema iko tayari kufanya kazi kwa karibu na serikali mpya ya Israel na imesisitiza kuhusu uhusiano mzuri kati ya nchi hizo mbili, licha ya kuwepo tofauti hivi karibuni kuhusu sera ya Israel ya makaazi. Msemaji wa serikali ya Ujerumani, Steffan Seibert amesema nchi hiyo inasubiri matokeo rasmi ya uchaguzi huo uliofanyika jana Jumanne.

Huku asilimia 97.4 ya kura zikiwa zimeshahesabiwa, matokeo yanaonesha kuwa chama cha Likud cha Netanyahu na washirika wake wa kisiasa kimepata ushindi wa viti 65 katika bunge la Israel lenye viti 120 na matokeo rasmi yanatarajiwa kutolewa kesho mchana.

ISRAEL-DENMARK-DIPLOMACY-diplomacy-Denmark-Israel (Getty Images/AFP/G. Tibbon)

Rais wa Israel, Rueven Rivlin

Hata hivyo, kiongozi wa ngazi ya juu wa kundi la Hamas, Khalil al-Hayya ameyapuuza matokeo ya uchaguzi wa Israel akisema kuwa hayana maana.

''Hakuna tofauti kati ya vyama vya Israel, vyote ni sawa, vina msimamo wa kukalia kwa mabavu. Msimamo wetu uko wazi, tutakabiliana na matokeo yote haya na tutaongeza nguvu kuhakikisha tunamaliza ukaliaji wa kimabavu na kufikia malengo yetu ya kitaifa na kanuni za watu wa Palestina,'' alisema Al-Hayya.

Aidha, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu ameitaka Israel kuachana na msimamo wake mkali wa kizalendo kwani uchaguzi umeshakamilika. Naye msaidizi wa Rais wa Palestina, Mahmoud Abbas amesema matokeo ya uchaguzi wa Israel yanaongeza wasiwasi kwa Wapalestina kuhusu Israel kuyanyakua maeneo ya Ukingo wa Magharibi.

Hayo yanajiri wakati ambapo Rais wa Israel, Rueven Rivlin amesema mazungumzo yake na vyama vya kisiasa vilivyochaguliwa kuhusu mchakato wa kuunda serikali mpya, yataanza wiki ijayo. Taarifa iliyosomwa leo na msemaji wa Rais Rivlin imeeleza kuwa mkutano huo utaonyeshwa moja kwa moja kwenye televisheni na majukwaa yote ili kuleta uwazi.

Baada ya kusikia mapendekezo ya vyama kwa waziri mkuu ajaye, rais atatangaza mbunge ambaye ataaminiwa katika kuunda serikali. Mtu huyo atakuwa na siku 28 za kufanya hivyo na anaweza akaongezewa siku nyingine 14. Bunge jipya litaapishwa Aprili 23 na serikali mpya inatarajiwa kuapishwa ifikapo mwanzoni mwa mwezi Juni.

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com