1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kutambuliwa Palestina kama dola huru kwasifiwa na kupingwa

22 Mei 2024

Baada ya Norway, Ireland na Uhispania kutangaza mipango ya kuitambua rasmi Palestina kuwa ni dola huru, nchi mbalimbali zimesifu hatua hiyo huku Israel ikisema hatua hiyo sio sahihi hata kidogo

https://p.dw.com/p/4g9kE
Machi 28 2022, Ramallah, Ukingo wa Magharibi, Mamlaka ya Palestina: Kiongozi wa Palestina Mahmoud Abbas akutana na Mfalme wa Jordan Abdullah ll
Kulia: Kiongozi wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas alipokutana na Mfalme wa Abdullah ll wa Jordan mnamo Machi 28.2022 katika mji wa Ramallah kwenye Ukingo wa MagharibiPicha: IMAGO/ZUMA Wire

Saudi Arabia imeupongeza uamuzi wa Ireland, Norway na Uhispania wa kulitambua taifa huru la Palestina na imezitaka nchi nyingine kufanya hivyo.

Katibu mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Palestina (PLO), Hussein Al-Sheikh, amesema hatua hii ni ya kihistoria na amezishukuru nchi ambazo zimetambua na zinazofanya jitihada za kulitambua Taifa huru la Palestina. Amethibitisha kuwa hii ni njia ya utulivu, itakayoleta usalama na amani katika kanda ya Mashariki ya Kati.

Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman bin Abdulaziz Al Saud
Mwanamflame wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman bin Abdulaziz Al SaudPicha: Sergei Savostyanov/Sputnik/REUTERS

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan Ayman Safadi, amesema kwenye mkutano na waandishi wa Habari akiwa pamoja na mwenzake wa Hungary huko mjini Amman kwamba wameyakaribisha maamuzi yaliyochukuliwa na nchi tatu rafiki wa bara la Ulaya ambazo zimetangaza kutambua mchakato wa Palestina kuwa taifa huru.

Soma Zaidi:Ireland, Uhispania, Norway zatangaza kuitambua Palestina kma taifa huru

Safadi amesema wanauthamini uamuzi huo na wanauchukulia kuwa ni hatua muhimu kuelekea kupatikana suluhisho la nchi mbili litakalojumuisha taifa huru la Palestina kwa kuzingagtia mipaka ya Juni, 1967.

Jordan ni mlinzi wa maeneo matakatifu ya Waislamu na Wakristo katika mji wa Jerusalem, na imekuwa na jukumu la upatanishi kati ya Israeli na Wapalestina hapo awali.

Mataifa ya Ghuba yaunga mkono

Nchi sita wanachama wa Baraza la Ushirikiano wa nchi za Ghuba pia zimeunga mkono hatua ya nchi za Ulaya ya kuitambua Palestina kama dola huru. Katibu mkuu wa baraza hilo Jasem Mohamed Albudaiwi, amesema hiyo ni hatua muhimu na ya kimkakati itakayowezesha kufikiwa suluhisho la kuundwa mataifa mawili na litakaloumaliza mzozo wa Israel na Palestina.

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC, yenye makao yake makuu katika mji mkuu wa Saudi Arabia, Jeddah, imesema hiyo ni hatua muhimu ya kihistoria.

Kiongozi wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas
Kiongozi wa mamlaka ya Palestina Mahmoud AbbasPicha: Saudi Press Agency/Newscom/picture alliance

Waziri wa usalama wa taifa wa Israel, Itamar Ben Gvir, anayeelemea siasa kali za mrengo wa kulia alitembelea eneo takatifu la msikiti wa Al- Aqsa katika mji wa Jerusalem Jumatano ambapo alilaumu vikali uamuzi wa Uhispania, Ireland na Norway wa kuitambua Palestina kama taifa huru. Amesema: 

"Nchi zilizoitambua Palestina kama taifa huru leo hii zimewapa nguvu wapiganaji wa Hamas, wauaji na wanyanyasaji. Na mimi nasema hivi: Hatukubaliani na kauli kuhusu kuwepo taifa huru la Palestina au hata kauli inayosema kuwepo nchi kama hiyo.”

Nchi zipatazo 140 wanachama wa Umoja wa Mataifa zinaitambua Palestina kama taifa. Idadi hiyo ni zaidi ya thuluthi mbili ya nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa. Lakini nchi zenye nguvu kama, Marekani, Ujerumani, Ufaransa na Uingereza bado hazijaitambua Palestina kama dola huru.

Soma Zaidi:Israel yakabiliwa na shinikizo la kuafiki uwepo wa taifa huru la Palestina

Ujerumani yasemaje

Ujerumani inaunga mkono suluhu ya serikali mbili inayotafutwa kwa muda mrefu kati ya Israel na Wapalestina imesema hatua ya kuanzishwa kwa nchi ya Palestina inaweza tu kufanikiwa kwa kufanyika mazungumzo ya moja kwa moja kati ya pande hizo mbili.

Israel Jerusalem | Waziri wa Usalama wa Taifa wa Israel Itamar Ben Gvir
Waziri wa Usalama wa Taifa wa Israel, Itamar Ben GvirPicha: Debbie Hill/UPI Photo/IMAGO

Vita vya Israel dhidi ya kundi la Hamas vilianza Oktoba 7, mwaka jana pale wanamgambo wa Hamas walipofanya mashambulizindani ya ardhi ya Israeli, ambapo watu 1,200 waliuawa na wengine 250 walichukuliwa mateka.

Wakosoaji na washirika wa Israeli wanazidi kuchanganyikiwa kutokana na vita vinavyoendelea ambavyo vimesababisha maalfu ya watu kupoteza maisha katika Ukanda wa Gaza na wakati huo huo kuwalazimisha maelfu ya watu kuyahama makazi yao na pia kutokana na kuongezeka hali mbaya ya kibinadamu katika eneo hilo.

Mamlaka ya afya katika Ukanda wa Gaza inayoendeshwa na Hamas imesema zaidi ya watu 35,500 wameuawa hadi kufikia sasa.

Vyanzo: AP/AFP/DPA