Mzuka wa WikiLeaks waidamana Marekani kila iendapo | Matukio ya Kisiasa | DW | 01.12.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mzuka wa WikiLeaks waidamana Marekani kila iendapo

Huku jumuiya ya OSCE ikitoa wito wa kujiimarisha, inaonekana mzuka wa nyaraka za siri kutoka vyanzo vya kidiplomasia zilizochapishwa na mtandao wa WikiLeaks umeendelea kuiandama Marekani popote pale iendapo

Taarifa za WikiLeaks kwenye magazeti

Taarifa za WikiLeaks kwenye magazeti

Kwa mara nyengine tena, Hillary Clinton amejikuta akitanguliza kujilinda kabla hajashambuliwa. Akijua kwamba, mzuka wa nyaraka za siri zilizovujishwa na mtandao wa WikiLeaks, hauwezi kumuacha popote aendapo, leo (1 Disemba 2010) aliwatoa wasiwasi washirika wa Marekani kwenye mkutano huo wa OSCE kwamba kamwe jambo hili halitaizuia nchi yake kufanya kazi nao.

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya mkutano huo, Bi Clinton amesema na hapa namnukuu: "Mimi mwenyewe ndiye niliyeliibua suala hili kwa wenzetu, ili kuwahakikishia kuwa nyaraka za WikiLeaks hazitaweza kwa namna yoyote ile kuingilia diplomasia yetu wala ahadi yetu ya kuendeleza kazi muhimu ambayo inaendelea."

Bi Clinton amesema kwamba alitangulia kutoa tamko hilo, licha ya kuwa hajapokea taarifa yoyote ikiwa kuna nchi inayotaka kujitoa kwenye majadiliano na Marekani kwa sababu ya kuchapishwa kwa nyaraka hizi.

Hillary Rodham Clinton

Hillary Rodham Clinton

Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi mwenyeji wa mkutano huo, Kanat Saudabayev,ameelezea kuyafahamu mashaka hayo ya Marekani na akathibitisha kwamba nyaraka za WikiLeaks hazitakuwa na athari kwa mkakati wa nchi hizo mbili. Alisema na hapa namnukuu: "Naamini kwamba kilichotokezea ni jambo la kawaida ambalo hutokezea mara kwa mara katika kazi zetu."

Ili kutolipa nafasi jambo hili, haraka wajumbe wa mkutano huu wakarukia katika ajenda zilizowaleta, ikiwemo ya usalama wa Ulaya, Marekani na dunia, ambapo Bi Clinton aliuambia mkutano huo kwamba migogoro inayojumuisha mataifa mbalimbali imekuwa ni kitisho kwa amani ya ulimwengu, huku akisisitizia suala la demokrasia na haki za binaadamu.

Masuala yote aliyoyataja Bi Clinton yanahusiana moja kwa moja na eneo la Asia ya Kati ambako mkutano huo unafanyika. Kuna migogoro kadhaa inayofukuta katika eneo hilo ambalo lina nchi nyingi zilizokuwa sehemu ya Shirikisho la Kisovieti, ukiwemo ule wa Nagorno-Karabakh kati ya Armenia na Azerbaijan, uasi wa eneo la Moldova katika Transdniestria na mikoa inayotaka kujitenga kutoka Georgia, ya Ossetia ya Kusini na Abkhazia. Migogoro yote hii imewekwa kwenye orodha ya juu katika ajenda za mkutano huo.

Nchi za Magharibi, ikiwemo Marekani, inazilaumu serikali za nchi kwenye eneo hili kwa kutokuzingatia demokrasia na haki za binaadamu, na kwa hakika huko mwanzoni walikuwa hawapendelei nchi ya Kazakhstan kupewa heshima ya kuandaa mkutano huu.

Kazakhstan, ambayo ni miongoni mwa nchi zenye uchumi mkubwa kwenye eneo hili la Asia ya Kati, inalaumiwa kwa uvunjaji mkubwa wa haki za binaadamu. Lakini kiongozi aliyeliongoza taifa hilo kwa mwaka wa 20 sasa, Rais Nursultan Nazarbayev, anajisifu kwamba angalau nchi yake imeweza kuleta aina ya demokrasia katika eneo ambalo haikuwahi kuwapo kabisa hapo kabla.

"Hapa Kazakhstan, utulivu kwanza unamaanisha ukuwaji wa uchumi. Kwanza tulikuza uchumi ili umasikini usiidhalilishe demokrasia yetu changa." Nazarbayev aliuambia mkutano huo.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFPE/DPA

Mhariri: Othman Miraj

DW inapendekeza

 • Tarehe 01.12.2010
 • Mwandishi Admin.WagnerD
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/QNB5
 • Tarehe 01.12.2010
 • Mwandishi Admin.WagnerD
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/QNB5

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com