1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa kiuchumi wajadiliwa katika ofisi ya kansela

Oumilkher Hamidou15 Desemba 2008
https://p.dw.com/p/GGMB
Mkutano wa viongozi kwa lengo la kuufufua uchumiPicha: AP


Njama ya kutaka kumuuwa mkuu wa kituo cha polisi cha Passau,idara ya upelelezi ya Ujerumani na suala la vita vya Irak na mkutano wa kilele kuhusu mzozo wa kiuchumi ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.


Tuanze lakini na mzozo wa kiuchumi na jukumu la kansela Angela Merkel katika mkutano wa kilele ulioitishwa jana katika ofisi ya kansela mjini Berlin.Gazeti la LÜBECKER NACHRICHTEN  linaandika:



Sura inayotokana na siasa ya Ujerumani kwa jumla hivi sasa,si ya kuvutia hivyo kuweza kuhamasisha imani ya watu..Badala yake sura hiyo inachangia kumkanganya mtu.Si msimamo wa kujihami wa kansela katika kukabiliana na mzozo uliosababisha hali hiyo,msimamo ambao unaeleweka,bali zaidi ni ile hali ya udhaifu inayojitokeza katika uongozi wake, inayowafanya watu wapotelewe na imani mbele ya kansela,baraza lake la mawaziri na hata vyama vinavyounda serikali kuu ya muungano."


 Gazeti la BERLINER MORGENPOST linamulika hatua ziada ili kuufufua uchumi.Gazeti linaendelea kuandika:



"Kwakua Merkel bado amefungika kutokana na serikali ya muungano wa vyama vikuu,kuna kitisho hata mpango mpya wa kufufua uchumi usilete tija inayotarajiwa.La maana ingekua kuweka vitega uchumi katika soko la ajira,ambapo tija yake haitakawia kuonekana.Wanauchumi wanazungumzia kila kwa mara kuhusu miradi ya kuinua miundo mbinu.Lakini bora zaidi ni kuhakikisha fedha zinawekezwa katika kutengeneza njia na shule.Bila ya shaka vitega uchumi vitakavyoleta tija zaidi ni vile  vitakavyowekezwa katika shule za chekechea na sio katika barabara za konkriti."



Mada ya pili magazatini inahusu shambulio la wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia dhidi ya mkuu wa polisi huko Passau.Gazeti la Ostesee-Zeitung la mjini Rostock linaandika:



Mkuu wa polisi Alois Mannichl amepata bahati kweli kweli-amenusurika na shambulio lililolengwa kumuangamizia maisha yake.Mara baada ya habari kujulikana,sauti zikaanza kusikika;kila la kufanya litafanywa kuwakamata wahusika na hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.Kamisheni maalum ikaundwa kuishughulikia kadhia hiyo-Yote hayo ni sawa.Lakini haitoshi.Kuna umuhimu pia wa kuchunguzwa na kupambana na sababu zinazopelekea kuzidi matumizi ya nguvu.


 Gazeti la OLDENBURGISCHE VOLKSZEITUNG linaandika:


Mkuu wa polisi ya Passau Alois Mannichl anasifiwa sana na kutajwa kua mfano wa kuigizwa katika fani yake.Mkakamavu na hafanyi mzaha linapohusika suala la kupambana na vichwa upara wanaofuata siasa kali za mrengo wa kulia.Watu kama Mannichl ni miongoni mwa nguzo za demokrasia nchini Ujerumani.Hata hivyo bado si hakika kama shambulio la kutaka kumuuwa limefanywa na wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia.Lakini kila kitu kinaonyesha wako nyuma ya shambulio hilo lililokua nusra limuangamizie maisha.