Mpango wa amani kati ya Israel na Palestina umo mashakani? | Matukio ya Kisiasa | DW | 09.05.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mpango wa amani kati ya Israel na Palestina umo mashakani?

Waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert analazimishwa kujiuzulu kutokana na kashfa mpya ya ufisadi inayomkabili

default

Waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert

Mpango wa amani kati ya Israel na Palestina huenda ukasimamishwa kwa mwaka mmoja iwapo waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert atalazimika kuondoka mamlakani kutokana na kashfa za ufisadi.


Wapinzani wa Olmert wanamtaka ajiuzulu wakizua madai mapya kwamba alipokea mlungula kutoka kwa raia mmoja wa Marekani kimyume na sheria.


Olmert anadaiwa kupokea mlungula wa maelfu ya dola kutoka kwa mfadhili huyo lakini anapinga madai hayo.


Hata hivyo anasema atajiuzulu iwapo atashtakiwa katika kesi inayotishia siasa za mashariki ya kati kwa wakati huu ambapo eneo hilo linatafuta amani kwa udi na uvumba.


Kura ya maoni nchini Israel inaonyesha chama cha Likud chenye siasa kali kitapata ushindi mkubwa iwapo uchaguzi utafanyika.


Olmert mwenye miaka 62 aliingia mashakani baada ya jaribio la kuizima kesi hiyo kutupiliwa mbali na mahakama hapo jana.


Sakata ya ufisadi inayomkabili imekuja wakati Israel inasherehekea miaka 60 na pia Rais wa Marekani George Bush anatarajiwa kuwasili nchini humo wiki ijayo.


Gideon Star anaeongoza kundi la wabunge wa chama cha kihafidhina cha Likud anasema kashfa inayomzunguka Olmert haiwezi kumpatia nafasi nzuri ya kufanya kazi yake.


Waziri huyo mkuu amekuwa akiandamwa na kashfa mbali mbali tangu alipochukua atamu mwaka wa 2006; jambo linalozua shauku miongoni mwa wanachama wenzake.


Katika hali ya kujitenga na Olmert katibu mkuu wa chama cha Labour Eytan Cabel amesema ukitazama chunguzi zote za awali utajua kwamba mrija tu ndio uliovunja mgongo wa ngamia.


Kwa upande mwengine maafisa wa Palestina wanahofia kwamba sakata hiyo huenda ikaathiri mpango wa amani hususan iwapo uchaguzi wa mapema utaitishwa.


Mjumbe mkuu wa Palestina katika mazungumzo ya amani Ahmed Qurie amesisitiza kwamba Palestina inachukulia sakata ya Olmert kama siasa za ndani ya Israel na anatumai hazitaathiri mpango wa amani hata waziri huyo akilazimika kujiuzulu.


Mjumbe mwengine wa Palestina Saeb Erekat anasema serikali yao inafuatilia kwa makini sakata hiyo.


Kwengineko msemaji wa serikali ya Marekani Gordon Johndroe amesema ziara ya Rais wa nchi hiyo George W Bush nchini Israel itaendelea kama ilivyopangwa na atakutana na Olmert katika ziara hiyo.


Rais huyo anafanya bidii ili mpango wa amani ulioanzishwa na Marekani nevember mwaka uliopita ufaulu kabla hajaondoka mamlakani januari mwaka ujao.


Waziri wa haki amesema Olmert anachunguzwa kufuatia madai kwamba alipokea mlungula kutoka kwa mfanyibiashara wa kimataifa alipokuwa meya wa mji wa Jerusalem na waziri wa viwanda.


Akiongea na vyombo vya habari Olmert amesema iwapo mkuu wa sheria ataamua kumfungulia mashtaka basi atajiuzulu. Anasema atachukua hatua hiyo licha ya sheria kumkataza.


Anakubali kupokea kile anachokiita misaada ya kifedha kutoka kwa mfayibiashara myahudi anaeishi Marekani Morris Talanski mwenye miaka 75. Anasema hayo hayakuwa kinyume na sheria.


Wachunguzi wa kashfa za ufisadi wamekutana na Olmert kwa saa moja leo na pia wamekutana na mkurugenzi wake wa zamani Shula Zaken mara nne.


Olmert aliingia mamlakani baada ya aliyekuwa waziri mkuu Ariel Sharon kuugua na kulazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi mwaka wa 2006. Mnamo Machi mwaka huo alikiongoza chama chake cha Kadima katika ushindi na akaingia mamlakani kama waziri mkuu.


Amekabiliwa na kashfa kadhaa za ufisadi, na umaarufu wake umepungua; vile vile analaumiwa kwa kushindwa katika vita vya mwaka wa 2006 dhidi ya Hezbollah na pia anakabiliwa na tisho la kuugua saratani.


Waziri mkuu anapojiuzulu, Rais wa Israel ambaye sasa ni Shimon Peres atamchagua kiongozi mwengine atakaechukua mamlaka hayo na kuunda serikali mpya. Iwapo hayo hayatajiri basi uchaguzi wa mapema lazima utafanyika.


Kwa sasa waziri wa mambo ya nje Tzipi Livni ndio anaetarajiwa kuchukua mahala pa Olmert iwapo atajiuzulu.


Mawaziri wakuu wa zamani Ariel Sharon, Ehud Barak na Benjamin

Netanyahu pia walikabiliwa na kashfa za ufisadi lakini hakuna kesi hata moja dhidi yao iliyofaulu.

 • Tarehe 09.05.2008
 • Mwandishi Mwakideu, Alex
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DxRw
 • Tarehe 09.05.2008
 • Mwandishi Mwakideu, Alex
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DxRw
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com