1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MOSCOW: Urusi yalitaka baraza la usalama liamue kuhusu hatima ya Kosovo

25 Julai 2007
https://p.dw.com/p/CBfU

Urusi imelitaka baraza la usalama la Umoja wa Mataifa liamue hatima ya jimbo la Kosovo nchini Serbia, licha ya uamuzi wa kuliwasilisha swala hilo kwa kundi la mataifa sita.

Marekani na washirika wake wa Ulaya Ijumaa iliyopita iliahirisha mpango wa Umoja wa Mataifa kuipa uhuru Kosovo huku Urusi ikitishia kuuzuia mpango huo kutumia kura yake ya turufu.

Mmoja wa wajumbe wa baraza la usalama, bwana Wolf, amesema lengo ni kutoa mwanya mazungumzo yaendelee kufanyika.

´Kucheleweshwa kwa mpango huo kunalenga kutoa nafasi majadiliano yaendelee kufanyika jambo ambalo baadhi ya wanachama wa baraza la usalama wanaamini litakuwa muhimu.´

Wakati huo huo serikali ya Serbia imewaonya washirika wa nchi za magharibi wasiitambue Kosovo kama taifa huru pasipo idhini ya Umoja wa Mataifa, huku kukiwa na hofu serikali ya mjini Pristina huenda ikatangaza uhuru wake kutoka kwa Belgrade.

Jimbo la Kosovo limekuwa likitawaliwa na Umoja wa Mataifa tangu mwaka wa 1999 wakati kampeni ya mashambulio ya mabomu iliyofanywa na majeshi ya jumuiya ya kambi ya magharibi NATO, iliposaidia kumaliza mauaji ya Waalbania yaliyofanywa na Serbia.