Mkuu wa majeshi ya waasi wa Libya ameuawa
29 Julai 2011Matangazo
Mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa la Mpito la waasi, Mustafa Abdel Jalil amesema, Jenerali Younes alikuwa akirejea Benghazi kutoka uwanja wa mapigano. Viongozi wengine wawili wa waasi pia waliuawa katika shambulio hilo.
Jalil ametangaza siku tatu za maombolezo na amemtuhumu kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi kutaka kuvunja umoja wa waasi. Younes alikuwa waziri wa mambo ya ndani katika serikali ya Gaddafi, lakini alijiunga na waasi katika mwezi wa Februari. Hapo awali, msemaji wa waasi alisema kuwa Younes aliitwa kwenda Benghazi kuhojiwa. Ilishukiwa kwamba Younes aliwasiliana na serikali ya Gaddafi kupitia familia yake.