Mkutano wa kilele wa jumuia ya ushirikiano wa kiuchumi Afrika magharibi ECOWAS mjini Abuja | Matukio ya Kisiasa | DW | 16.02.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mkutano wa kilele wa jumuia ya ushirikiano wa kiuchumi Afrika magharibi ECOWAS mjini Abuja

Hali nchini Guinee,Niger na Côte d'Ivoire ni miongoni mwa mada zitakazojadiliwa na viongozi wa mataifa 15 ya ECOWAS

Kiongozi wa kijeshi wa Guinee aliyejeruhiwa katika njama ya kutaka kumuuwa Dadis Camara

Kiongozi wa kijeshi wa Guinee aliyejeruhiwa katika njama ya kutaka kumuuwa Dadis Camara

Tunaelekea Afrika magharibi ambako viongozi wa jumuia ya ushirikiano wa kiuchumi ECOWAS wanatazamiwa kukutana leo mjini Abuja nchini Nigeria kuzungumzia hali namna ilivyo nchini Guinee,Niger na Côte D'Ivoire.

Tuanzie Guinee ambako matumaini mema yamechomoza baada ya viongozi wa nchi hiyo kukubaliana kuunda serikali ya mpito itakayoitisha uchaguzi mkuu baada ya miezi kadhaa ya mgogoro wa kisiasa.Serikali hiyo ya mpito inawajumuisha raia wa kawaida na wanajeshi.

Hayo ni matokeo ya wiki kadhaa za midahalo kuhusu suala la vipi kurejesha utawala wa kiraia katika nchi hiyo tajiri kabisa kwa maadini baada ya kudhibitiwa kwa zaidi ya mwaka mmoja na wanajeshi.

Serikali mpya ya mpito ina mawaziri 32 na inaongozwa na mwanasiasa mkongwe wa upande wa upinzani Jean Marie Doré,aliyechaguliwa kwa muda kua waziri mkuu mwezi uliopita.

"Tunabidi tulete wizani kati ya pande zote husika.Nnatambua dhamana niliyotwikwa" amesema Jean Marie Doré,kabla ya kutangazwa baraza lake la mawaziri.

Jean Marie Doré alipewa jukumu la kuandaa uchaguzi mkuu hadi ifikapo kati kati ya mwaka huu baada ya njama ya kutaka kumuuwa kiongozi wa utawala wa kijeshi Moussa dadis Camara,december tatu iliyopita.

Wadadisi walihofia kukawia kuundwa serikali ya mpito kusije kukakorofisha juhudi za amani katika nchi hiyo iliyoko katika eneo lililokua limegubikwa na miaka kadhaa ya vita na vurugu.

Elfenbeinküste Präsident Laurent Gbagbo

Rais Laurent Gbagbo wa Côte d'Ivoire

Katika wakati ambapo matumaini mema yameanza kuchomoza nchini Guinee,katika nchi jirani ya Côte d'Ivoire,hali inatia wasi wasi baada ya rais Laurent Gbagbo kuivunja serikali na tume ya uchaguzi ijumaa iliyopita.Polisi imetumia gesi za kutoa machozi kuwatimua mamia ya waandamanaji huko Abengourou,mashariki ya nchi hiyo.

Upande wa upinzani unafungamanisha uamuzi wa rais Laurent Gbagbo na mapinduzi" yaliyolengwa kuakhirisha kwa mara nyengine tena uchaguzi mkuu uliokua ufanyike mwezi ujao.

Kimsingi uchaguzi huo ulikua umalize mgogoro ulioripuka kufuatia njama iliyoshindwa ya mapinduzi mwaka 2002 pamoja pia na vita vya wenyewe vilivyopelekea kugawika sehemu mbili nchi hiyo,inayosafirisha kakao kwa wingi ulimwenguni-sehemu ya kaskazini ikisalia mikononi mwa waasi.

Kiongozi wa zamani wa waasi,waziri mkuu Guillaume Sorro amekua akizungumza na pande zote zinazohusika na mgogoro huu mpya kwa lengo la kuunda serikali mpya ya mpito.Upande wa upinzani unashurutisha lakini kurejea serikalini na kurejeshwa upya tume ya uchaguzi.Guillaume Sorro amekwenda Bouake-ngome ya waasi wa zamani wa Forces Nouvelles,anaowaongoza na ambako anatazamiwa kutangaza msimamo wake kuhusu mgogoro huu wa sasa.

Na wakati huo huo viongozi wa mataifa 15 ya jumuia ya ushirikiano wa kiuchumi Afrika magharibi-ECOWAS wanatazamiwa kukutana leo hii mjini Abuja nchini Nigeria kuzungumzia hali namna ilivyo nchini Guinee,Côte d'Ivoire na Niger.

Mkutano huo ulioakhirishwa mara mbili,utamteuwa pia mwenyekiti mpya atakaeshika nafasi ya rais Umaru Yar'Adua wa Nigeria anaetibiwa maradhi ya moyo nchini Saud Arabia tangu November 23 iliyopita.

Mwandishi:Hamidou,Oummilkheir/ AFP

Mhariri:Abdul-Rahman,Mohammed

 • Tarehe 16.02.2010
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/M2hh
 • Tarehe 16.02.2010
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/M2hh
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com