Mkutano wa G-20 watoa sura mpya ya ulimwengu mkubwa zaidi | Magazetini | DW | 17.11.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Mkutano wa G-20 watoa sura mpya ya ulimwengu mkubwa zaidi

Mkutano wa viongozi wa nchi 20 tajiri zilizoendelea kiviwanda na zinazoinukia kiuchumi uliofanywa Washington kujadili mgogoro wa fedha,ni mada iliyogonga vichwa vya habari katika magazeti mengi ya Ujerumani leo Jumatatu.

Mada nyingine inahusika na Opel-kampuni ya kutengeneza magari iliyokuwa muhanga wa mgogoro wa fedha duniani. Gazeti la BILD ZEIUTUNG linalochapishwa Berlin linasema:

"Daima mikutano ya kilele hupimwa kwa kile kitakachotekelezwa baada ya viongozi kurejea nyumbani.Na hivyo ndio itakavyokuwa pia kuhusu mkutano wa G-20 uliofanywa Washington mwisho wa juma lililopita.Hata hivyo moja limedhihirika-mkutano huo umetoa sura mpya ya ulimwengu ulio mkubwa zaidi na sio vile Ulaya na Marekani zilivyozoea.Wajumbe wanaowakilishi theluthi mbili ya umma na asilimia tisini ya uchumi duniani wanapoketi kwenye meza moja na madola makuu ya zamani yapo tayari kushirikiana na kuwajibika,basi mataifa makuu mapya kama China hayatoweza kujitenga. Sasa ni wakati wa kushikamana na kuukabili mgogoro wa fedha duniani kwa pamoja."

Gazeti la MÄRKISCHE ALLGEMEINE kutoka Potsdam likiendelea na mada hiyo hiyo linasema:

"Hapo mwanzoni mkutano wa Washinton haukutazamiwa kuwa na mafanikio makubwa.Lakini umeshangaza kwani katika taarifa ya pamoja iliyotolewa mwisho wa mkutano huo,viongozi wamekubaliana kuchukua hatua za kuzuia janga la aina hiyo kutokea tena katika siku za usoni.Zaidi ni kuwa hata nchi zinazoinukia kiuchumi kama China,India na Brazil zimekubali kuwajibika na sio tu kundi dogo la kawaida la nchi nane tajiri zilizoendelea kiviwanda."

Kwa maoni ya LANDESZEITUNG LÜNEBURG,mkutano wa kilele wa G-20 mjini Washington umefanikiwa kuzijumuisha nchi zinazoinukia kiuchumi na kuweka msingi imara.Na kufafanua:

"Kwa maneno mengine,ile klabu ndogo imeelewa kuwa inahitaji kushirikiana na mataifa mengine.Yaani sasa hakuna tena kundi la mataifa muhimu tajiri yaliyoendelea kiviwanda yaani G7 au G8 pamoja na Urusi,bali katika siku za usoni hadi nchi 20 zinapaswa kushauriana na kuwajibika kuleta utulivu katika masoko ya fedha duniani."

Tukipindukia mada nyingine,SCHWÄBISCHE ZEITUNG linaamini iwapo serikali itaiokoa kampuni kale ya Opel basi umaarufu wa serikali utapigwa jeki kwa haraka.Lakini kuna tatizo:-

"Naam,kwani kila mmoja atanyosha mkono kuomba msaada wa serikali.Hata makampuni yasioweza kuokolewa yataomba msaada na hivyo kuathiri sekta nzima.Kwa hivyo serikali ya mseto ya vyama vya kihafidhina na kisoshalisti ipo katika njia panda;Je, ielemee upande wa wafanyakazi au iongozwe na siasa za mpangilio?"

Tunamalizia kwa kulitupia jicho gazeti la NORDBAYERISCHER KURIER.

"Kwa maoni ya gazeti hilo,chama cha Kijani kilipomchagua mbunge wao wa Ulaya Cem Özdemir kushirikiana kukiongoza chama hicho,kimejipatia kiongozi mwenye mawazo yakinifu na kipaji cha kuzungumza wakati chama hicho kikikabiliwa na wakati mgumu kuelekea uchaguzi wa mwakani.Kwani hakuna anaeweza kutabiri kitakachotokea mwakani:Je,tena kitaishia upande wa upinzani au kitakuwa mshirika mdogo katika serikali ya mseto?Bora ni kutojifungamanisha na chama cho chote kabla ya uchaguzi kufanywa yaani hivi sasa mlango ubakie wazi lamalizia NORDBAYERISCHER ZEITUNG.