Mkutano wa Copenhagen waingia wiki ya pili | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 14.12.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Mkutano wa Copenhagen waingia wiki ya pili

Mkutano huo wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya hewa ulioingia katika mvutano unaonekana kuwa katika hatari ya kushindwa.

Waziri Mkuu wa Australia, Kevin Rudd.

Waziri Mkuu wa Australia, Kevin Rudd.

Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya hewa unaoendelea mjini Copenhagen-Denmark, umeingia wiki yake ya pili ambapo wakati viongozi wa taifa wakianza kuwasili leo, Waziri Mkuu wa Australia Kevin Rudd ameonya kuwa mazungumzo ya kimataifa kuhusu hali ya hewa ambayo yameingia katika hali ya mvutano yako katika hatari ya kushindwa. Rudd, ambaye anatarajiwa kuwasili katika mkutano huo wa Copenhagen, Jumatano ya wiki hii, amesema mataifa yanayotumia gesi zinazoharibu mazingira kama vile China na India yametoa kauli nzuri, lakini wakati mazungumzo hayo yanaingia katika wiki yake ya pili, makubaliano yanaonekana kuwa magumu kufikiwa. Waziri huyo Mkuu wa Austrilia amesema kuna hatari kubwa kwamba kutakuwa na maoni tofauti kati za mataifa yaliyoendelea na yale yanayoendelea.

Amesema malengo ya kupunguza matumizi ya gesi zinazochafua mazingira, fedha na uthibitisho zitakuwa ni ajenda muhimu za kujadiliwa katika mazungumzo hayo yenye lengo la kufikia mkataba ambao unaoweza kuidhinishwa Ijumaa ya wiki hii na zaidi ya viongozi 100 wa dunia. Aidha, Bwana Rudd, ameonya kuwa bila hatua madhubuti kuchukuliwa, Australia itakabiliana na ukame, moto unaozuka misituni na kupoteza rasilimali asilia na za kilimo.

Wakati huo huo, mawaziri wa mazingira kutoka ulimwenguni kote wanafanya mkutano wa faragha usiokuwa rasmi pembezoni mwa kikao cha kilele kitakachopumzishwa kwa siku moja kujaribu kutatua tofauti zilizojitokeza kati ya mataifa yaliyoendelea na yale yanayoendelea juu ya muswada wa makubaliano ya kukabiliana na ongezeko la ujoto duniani. Muswada huo unataka ifikapo mwaka 2050, matumizi ya gesi zinazoharibu mazingira yapunguzwe kwa asilimia 50 hadi 95. Mawaziri hao wa mazingira wanaokutana chini ya mwenyekiti wao, waziri wa zamani wa mazingira wa Denmark, Connie Hedegaard wanatoka katika mataifa yenye uchumi wa aina tofauti. Akizungumza zaidi Waziri wa Mazingira wa India Jairam Ramesh alisema, ''Tuna matumaini tunazishirikisha nchi zote. Tuna matumaini kwamba tutafanikiwa kupunguza tofauti zetu. Nadhani makubaliano ni muhimu. Kama sisi wote tutaaminiana zaidi na kama tuna ujasiri na tukiondoa shaka, nadhani tunaweza bado kufikia makubaliano yenye uwazi na haki katika mkutano wa Copenhagen.''

Kitengo cha Umoja wa Mataifa kinachohusika na athari za mabadiliko ya hali ya hewa-UNFCCC kina lengo la kupunguza matumizi ya gesi zinazoharibu mazingira ambazo zinazosababisha pia ongezeko la ujoto duniani na kwa lengo la kuzuia hatari zitokanazo na mabadiliko ya hali ya hewa. Kitengo hicho cha UNFCCC kinatarajia kuwa mataifa yanayoshiriki katika mkutano huo wa Copenhagen yataahidi kupunguza matumizi ya gesi hizo na kufungua njia ya kutoa mabilioni ya dola kwa ajili ya kuzisaidia nchi masikini zinazokabiliwa na matatizo ya dharura yatokanayo na mabadiliko ya hali ya hewa. Mkutano huo wa hali ya hewa unaangaliwa na baadhi ya wadadisi kuwa ulio muhimu kabisa tangu kumalizika kwa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE)

Mhariri: Abdul-Rahman

 • Tarehe 14.12.2009
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/L1mU
 • Tarehe 14.12.2009
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/L1mU
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com