Mkutano mkuu wa Democrat waanza leo | Matukio ya Kisiasa | DW | 25.08.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mkutano mkuu wa Democrat waanza leo

Mkutano Mkuu wa Chama Cha Demokratic unaanza leo huko Denver, kuelekea siku ya kumtawaza rasmi mgombea wa kiti cha urais nchini Marekani kupitia chama hicho Seneta Barack Obama na mgombea mwenza Seneta Joe Biden.

Seneta Barack Obama kushoto na mgombea mwenza Seneta Joe Biden kulia katika mkutano wa hadhara Springfield, Illinois

Seneta Barack Obama kushoto na mgombea mwenza Seneta Joe Biden kulia katika mkutano wa hadhara Springfield, Illinois

Mkutano huo unafanyika huku kauli mbiu ya chama hicho Umoja ikikabiliwa na changamoto kubwa kutoka kambi ya aliyekuwa mpizani wa Obama katika kuwania tiketi hiyo, Seneta Hillary Clinton, ambapo robo ya wafuasi wake bado wana hasira na kushindwa kwa mgombea wao.


Wakati ambapo Hillary Clinton ameeleza kuelekeza nguvu zake kwa Obama, ambapo hapo kesho anategemewa kuwaomba rasmi wafuasi wake kumuunga mkono Obama,utafiti mpya uliyofanywa na gazeti la USA Today umeonesha kuwa asilimia 30 ya wafuasi wake watampigia kura John MacCain au mgombea mwengine wa tatu.


Barack Obama anajaribu kuondoa mpasuko huo ili kuweza kuunganisha nguvu za chama hicho.


Msemaji wake Robert Gibbs akizungumza muda mfupi kabla ya kuanza kwa mkutano huo, alisema kuwa seneta Clinton dhahiri amekwishaeleza kuwa anamuunga mkono Obama, kwani uchaguzi wa mwezi Novemba ni kati ya Obama na MacCain.


Kati ya hao wawili Gibbs alisema kuwa yule ambaye ataweza, kuujenga upya uchumi, kuleta nafasi za kazi, kuondoa utegemezi katika nishati ya mafuta kutoka nje, ni seneta Barack Obama na si MacCain.Amesema kuwa Seneta Clinton amewahi kufanyakazi na wote wawili na ameamua kuwa mwenye uwezo wa hayo ni Seneta Obama.


Lakini msaidizi wa ngazi ya juu wa John MacCain Carly Fiorina amesema kuwa wafuasi wa kike wa seneta Clinton wanamtaka kiongozi ambaye wanaweza kumuamini kwa maamuzi na uzoefu wake.


Msaidizi huyo wa MacCain pia akazidi kumwaga mafuta katika moto wa mpasuko ndani ya Democrat kwa kusema kuwa Obama aliwashangaza na kuwaduwaza wafuasi hao wa kike wa Clinton kwa kumteua Seneta Biden kuwa mgombea mwenza huku akimnadi kuwa ni mtu anayeweza kufanya kampeni, kitu ambacho Clinton alikionesha zaidi wakati wa mchakato.


Hapo jana Barack Obama alimteua seneta wa jimbo la Delaware Joe Biden ambaye ni mzoefu katika masuala ya siasa za nje kuwa mgombea mwenza katika uchaguzi huo.


Biden ambaye ni Mweyekiti wa Kamati ya Siasa za Nje wa Chama cha Democratic anaonekana kuwa chaguo bora la Obama katika kuzipa pengo lake la uzoefu na masuala ya kigeni.


Ikumbukwe ya kwamba wakati mzozo wa Urusi na Georgia, ulipoibuka zaidi ya wiki mbili zilizopita Obama alikuwa mapumzikoni katika Kisiwa cha Hawahii na alilaumiwa kwa kuchelewa kuvalia njuga suala hilo, wakati ambapo mshindani wake John McCain alikuwa heshi kufanya mikutano na waandishi wa habari kuonesha upinzani mkali dhidi ya Urusi.


Kwa kumchagua Seneta Biden, Obama anaonekana kujiimarisha zaidi kushinda mbio hizo, kitu ambacho hata yeye aliwatanabaisha wafuasi wa chama chake huko Sringfield Illinois.


Obama mwenye umri wa miaka 47 anategemewa ndani ya mkutano huo kuyakinisha mipango yake pale atakapochaguliwa, na kujibu maswali na wasi wasi waliyonao waMarekani wapi atawapeleka watakapomchagua kuwa kiongozi wao.


Lakini kwa upande wao ma-Democrat hawana shaka na wanajiamiani kuwa Obama ambaye atakuwa rais wa kwanza mweusi ni mtu mujarab katika nafasi ya kumshinda mgombea wa Republican John MacCain.


Bill Burton mmoja wa wasemaji wa Obama anasema kuwa wanataka watu wamfahamu Obama ni mtu wa aina gani na wapi anataka kuipeleka nchi, na hapo ndipo wapiga kura watakapochagua mawili ama kuwa na mabadiliko au kuendelea na yale yale yaliyofanyika katika kipindi cha miaka minane ya utawala wa Rais Bush.

 • Tarehe 25.08.2008
 • Mwandishi Liongo, Aboubakary Jumaa
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/F4aW
 • Tarehe 25.08.2008
 • Mwandishi Liongo, Aboubakary Jumaa
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/F4aW
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com