1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel: Ujerumani imefaulu mtihani wa janga la corona

Yusra Buwayhid
30 Mei 2020

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameeleza matumaini katika siku za usoni baada ya Wajerumani kuchukua tahadhari kubwa dhidi ya virusi vya corona, lakini amewaonya kutojisahau na kudhani mapambano yamemalizika.

https://p.dw.com/p/3d28u
Deutschland Corona-Pandemie Alltag | Einkaufen auf dem Markt
Picha: picture-alliance/dpa/M. Brichta

Kansela Angela Merkel anaamini Ujerumani imefaulu mtihani wa janga la virusi vya corona hadi sasa, lakini ameonya dhidi ya watu kujisahau kadri taifa hilo linavyoendelea kuondoa vizuizi vilivyokuwa vimewekwa kuzuia kuenea kwa maambukizi hayo. "Tumefanikiwa katika mtihani huu hadi sasa," Merkel alisema katika ujumbe wake wa video wa kila wiki. "Idadi kubwa ya watu nchini mwetu wamechukua tahadhari, pamoja na kuwajibika kwa ajili ya wananchi wenzao."

Aidha Merkel ameonya: "Kuna watu wanaoamini kwamba kwa sababu idadi ya walioathirika haikuwa kubwa, basi kitisho nacho hakikuwa kikubwa tangu hapo awali. Huo ni uwongo!"

Merkel amesema anatumai kuendelea kuondoa zaidi vizuizi vilivyowekwa na serikali yake kadri siku zinavyosonga mbele, lakini ameutaka umma kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya virusi hivyo. Ingawa Ujerumani ilishuhudia idadi kubwa ya maambukizi ya virusi hivyo, vifo havikuwa vingi.

Indien Wanderarbeiter verlassen Neu Delhi wegen der Corona Pandemie
Wafanyakazi wahamiaji na familia zao wanangojea kupanda basi kuelekea kituo cha reli ili itakayowarudisha nyumbani kwao Uttar Pradesh, New Delhi, India, Mei 26, 2020.Picha: Reuters/A. Abidi

Trump akata uhusiano na WHO

Soma zaidi: Serikali Ujerumani zatofautiana kuhusu kuondoa vizuizi

Halikadhalika serikali ya Ujerumani imekosoa uamuzi wa Rais wa Marekani Donald Trump wa kukata uhusiano na Shirika la Afya Duniani (WHO), na kusema kuwa ni wa kuvunja moyo na utarejesha nyuma juhudi za kulinda afya ya ulimwengu. "WHO inahitaji kufanyiwa mageuzi kama linataka kuleta maadiliko yoyote" aliandika Waziri wa afya wa Ujerumani Jens Spahn katika mtandao wake wa kijamii wa Twitter, huku akisema Umoja wa Ulaya unapaswa kuchukuwa jukumu kubwa la kulisaidia shirika hilo kifedha na kusema hilo, ndilo litakuwa moja ya vipaumbele vya Ujerumani wakati itakapochukua urais wa kupokezana wa umoja huo Julai Mosi mwaka huu.

Umoja wa Ulaya nao Jumamosi umemtaka Trump kutafakari upya uamuzi wake wa kusimamisha ufadhili wa nchi yake kwa WHO, huku idadi ya maambukizi ya virusi vya corona ikiwa inaongezeka nchini India na kwengineko kuashiria kwamba janga la ulimwengu la ugonjwa wa COVID-19 bado halikumalizika.

Siku ya Ijumaa, Trump alisema anakata mahusiano ya Marekani na WHO anayoishutumu kwa kushindwa kuwajibika zaidi kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona.

Wakati hayo yakijiri, wataalamu kadhaa wameionya serikali ya Uingereza kuwa ni mapema mno kuondoa vizuizi kwa sababu mfumo wa kufanya vipimo na kufuatilia wagonjwa bado hauko tayari na virusi hivyo bado vinaendelea kusambaa kwa kasi kubwa.

Profesa Peter Horby, mwenyekiti wa Kundi la Ushauri dhidi ya Kitisho cha Virusi vya Kupumua (NERVTAG) na mwanachama wa Kundi la Ushauri wa Kisayansi Masuala ya Dharura (SAGE), amesema: "Kwa kweli hatuwezi kurudi nyuma na kuwa na idadi ya maambukizi na vifo kama tulivyokuwa tukipata zamani," aliiambia BBC Radio, na kuongeza kuwa mfumo wa kufanya vipimo, wa kufuatilia wanaoshukiwa kuwa a ugonjwa wa COVID-19 na hatimaye kuwatenga unahitajika kwanza kufanya kazi kwa ufanisi bila hivyo nchi itakuwa "hatarini".

Brasilien Massengräber und Krankenhäuser| Friedhof Vila Formosa in Sao Paulo
Makaburi ya wagonjwa wa COVID-19 nchini BrazilPicha: picture-alliance/ZUMAPRESS.com/P. Lopes

Brazil yaizidi Uhispani kwa maambukizi

Kwa upande wa Amerika Kusini, Brazil inaripotiwa kuwa na idadi kubwa ya vifo vinavyotokana na virusi vya corona kuliko Uhispania, kulingana na takwimu zilizotolea Ijumaa na Chuo Kikuu cha Marekani cha Johns Hopkins.

Wizara ya Afya ya Brazil imesema idadi jumla ya watu waliokufa kutokana na virusi hivyo imeongezeka hadi 27,787. Idadi jumla ya maambukizi yaliyodhibitishwa imefika 465,166, ikiwa ni idadi kubwa ya pili ulimwenguni kote, baada ya Marekani.

Soma zaidi: Brazil imerekodi maambukizi mengi kwa siku moja

Na huko nchini India kumeshuhudiwa siku nyingine tena ya idadi kubwa ya maambukizi ya virusi vya corona, ambapo watu zaidi ya 8,000 wamepata maambukizi hayo katika kipindi cha saa 24. Wizara ya Afya pia imethibitisha vifo 265 vimetokea katika wakati huo huo, kufuatia serikali kutoa mwongozo nchini humo baada ya kuweka vikwazo kwa miezi miwli.

India taifa lenye watu bilioni 1.3, hadi hivi sasa imethibitisha idadi jumla ya visa vya maambukizi 173,763, miongoni mwao watu 4,971 wamekufa kutokana na virusi hivyo vya corona.

Ulimwenguni kote visa vya maambukizi vinakaribia milioni 6 na vifo vimefika 365,000.

Chanzo: DW