1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Brazil imerekodi maambukizi mengi kwa siku moja

Sudi Mnette
29 Mei 2020

Brazil imeripoti visa zaidi ya 26,000 vya  maambukizi ya virusi vya corona kwa siku na kufanya idadi jumla ya maambukizi kupindukia watu 438,000

https://p.dw.com/p/3cwBH
Coronavirus - Brasilien
Picha: picture-alliance/dpa/Prefeitura Manaus/Semcom/A. Pazuello

Wakati mataifa ya Ulaya yanatangaza mipango yao ya kuondoa marufuku ya kukabiliana na virusi hivyo, kwa Afrika ripoti mpya ya wakfu wa kijerumani wa Konrad Adenauer unaonya janga hilo kwa Afrika, linaweza kuchochea kuibuka utawala wa kimababvu zaidi.

Brazil taifa la Amerika ya Kusini ndilo lenye kushika nafasi ya pili ya athari ya virusi vya coronacorona baada ya Marekani, kwa kuwa na visa vipya 26,417, ambavyo vimerekodiwa katika kipindi cha masaa 24. Katika kipindi hicho hicho, Wizara ya Afya ya Taifa hilo imerekodi vifo vipya 1,156 na kufanya idadi jumla ya vifo kuwa 438,238.

Marekani bado hali sio nzuri

Nayo, Marekani imerekodi vifo vipya vya watu 1,297 vilivyotokana na virusi vya, na kufanya idadi jumla ya vifo kufikia 101,573, tangu janga la virusi hivyo kuanza. Takwimu hizo ni kwa mujibu wa Chuo Kiuu cha Johns Hopkins. Kwe mujibu wa chuo hicho chenye makazi yake mjini Baltmore pia taifa hilo lina visa vya maambukizi milioni 1.7, likiwa ni zaidi ya taifa lolote duniani.

Hapa Ujerumani nako, idadi ya maambukizi inatajwa kuongezeka. Kwa mujibu wa taarifa za leo za taasisi ya Robert Koch kumekuwa na ongezeko la maambukizi mapya 741 na kufanya jumla ya maambukizi 180,458. Vifo vipya 39 na kufanya idadi jumla ya vifo hivyo kufikia 8,450. Korea Kusini imeripoti maambukizi mapya 58 lakini yote ni katika mji mkuu wake Seoul. Taasisi yenye dhamana ya udhibiti wa magonjwa nchini humo kwa idadi hiyo sasa kuna maambukizi 11,402 na vifo vinasalia kuwa 269.

London Premierminister Boris Johnson PK Corona-Krise
Waziri Mkuu wa Uingereza Boris JohnsonPicha: Reuters/10 Downing Street/A. Parsons

Ufaransa na Uingereza zapanga kulegeza masharti

Aidha kutokana na kuonekana hali ya unafuu Ufaransa na Uingereza zinatajwa kujiandaa zaidi na mipango ya kupunguza masharti ya kukabiliana na janga hilo kwa juma lijalo. Na Serikali ya Afrika Kusini imesema kuanzia Jumatatu itawaruhusu watu kununua pombe na kuhudhuria makanisani ikiwa ni sehemu yake ya kulegeza masharti ya kukabiliana na janga la corona. Afrika ya Kusini ina maambukizi 25, 937 huku vifo vikiwa 552.

Katika hatua nyingine katika ripoti yake iliyotolewa leo hii wakfu wa Kijerumani wa Konrad Adenauer imeonya kwamba janga la virusi vya corona linaweza kusababisha kuibuka kwa watawala wa kimabavu zaidi barani Afrika. Kwa mujibu wa ripoti hiyo wakfu huo wenye kuhusiana na chama cha Kansela Angela Merkel cha CDU, umeyataja mataifa kama Uganda, Mali na Tanzania kwa kuwepo kwa ongezeko la tabia ya vitendo vya utumiwaji wa nguvu katika kipindi hiki cha janga la corona.

Vyanzo; Reuters/AFP/AP/DPA