1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mauwaji ya Texas naq Ohio Magazetini

Oumilkheir Hamidou
5 Agosti 2019

Chanzo cha mauwaji ya Texas na Ohio nchini Marekani na mzozo katika ujia wa maji wa Hormuz ni miongoni mwa mada magazetini.

https://p.dw.com/p/3NMEq
USA Symbolbild Anschlag in El Paso
Picha: Getty Images/AFP/M. Ralston

Tunaanzia Marekani ambako maoni ya wahariri wa Ujerumani yanatofautiana kama chuki pekee ndio chanzo cha mauwaji ya El Paso na Dayton. Gazeti la "Schwäbische Zeitung" linaandika: "Si sawa kuhoji kama matamahsi ya chuki yanayotolewa na rais wa Marekani dhidi ya raia wa Mexico ndio chanzo pekee cha mauwaji hayo. Kilichotokea masaa machache baadae huko Ohio nacho pia hakina mfano-hata hivyo mtu anaweza kuhoji kwamba wepesi wa kumiliki silaha nchini Marekani  ndio sababu. Hata hivyo vyenzo vyote viwili vinabidi vizingatiwe uchunguzi utakapofanywa kuhusiana na mauwaji yote hayo. Juhudi za kuwashinda nguvu wanaotetea viwanda vya silaha, zimeshindwa. Nia ya kisiasa inakosekana katika nchi hiyo kubwa kabisa ambako katika baadhi ya maeneo watu hawataki kuachana na maisha huria ya Cowboys. Kinachojiri, sababu si Donald Trump kwasababu kuna wademocrat wanaofuata misimamo ya wastani, sawa na Republican wanaohisi pia kwamba kumiliki silaha ni muhimu, ingawa ni kweli pia kwamba matamshi yanaweza kuzusha balaa."

Gazeti la "Der neue Tag" linahoji "mwenye kupalilia chuki anavuna mauwaji ya kibaguzi". Gazeti linaendelea kuandika: "Mhariri wa gazeti hilo la Weiden anakumbusha risala iliyoandikwa na mtuhumiwa wa mauwaji ya el Paso mwenye umri wa miaka 21 akisema "shambulio hilo ni jibu kwa uvamizi wa Wahispania katika jimbo la Texas. "Uvamizi hatari, mikururo ya wahalifu, hatari kwa usalama wa taifa" ndio maneno anayoyatumia rais wa Marekani anapozungumzia kuhusu wahamiaji."

Mzozo wa Hormuz wazidi makali

Mzozo unaozidi makali katika ujia wa maji wa Hormuz katika ghuba la uajemi umemulikwa pia na wahariri wa magazeti ya Ujerumani. "Badische Zeitung" linamulika madhara ya mzozo huyo kwa Ujerumani.Gazeti linaendelea kuandika: "Waziri wa mambo ya nchi za nje Heiko Maas anafanya kana kwamba kinachojiri katika ujia wa maji wa Hormuz hakituhusu hata kidogo. Kinachotokea katika ghuba la uajemi kinaweza kugeuka mtihani mkubwa kwa Ujerumani. Mzozo kati ya Marekani na Uingereza kwa upande mmoja na Iran kwa upande wa pili unahatarisha masilahi ya Ujerumani. Biashara huru ya dunia pia inaingia hatarini. Siajabu kwa hivyo kama waingereza watavutiwa na wazo la opereshini itakayoongozwa na Marekani. Lakini Maas na SPD hawaonyeshi kuvutiwa na fikra hiyo na hoja ziko nyingi tu. Lakini pindi Ujerumani ingepania tangu mwanzo na kuonyesha msimamo bayana, hatari isingekuwa kubwa hivi hivi sasa.

 

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Khelef