1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matumaini ya kuimarika kwa utalii Afrika Mashariki

John Juma
10 Machi 2017

Nchi za Afrika mashariki zinazoshiriki maonesho ya kimataifa ya utalii jijini Berlin zimeelezea matumaini ya kuwavutia watalii wengi zaidi katika miaka ijayo huku wakilenga masoko mapya na aina mpya za utalii.

https://p.dw.com/p/2YyOL
Berlin ITB Afrika
Picha: DW/D. Pelz

Nchi mbalimbali zimeelezea matumaini ya kuviinua viwango vya vivutio vyao vya kitalii ili kuwavutia watalii wengi zaidi. Nchi za Afrika mashariki zinazoshiriki kwenye maonyesho ya kimataifa ya utalii jijini Berlin hazijaachwa nyuma katika juhudi hizo. 

Katika mwaka wa 2015-2016, Tanzania ilirekodi jumla ya watalii milioni moja nukta moja, Kenya ikawapokea watalii milioni moja nukta nne, na sasa nchi hizo zimejiwekea malengo ya kuzidisha idadi hizo ifikapo mwisho wa mwaka wa bajeti 2016-2017.

Kupitia kampeni ya pamoja inayozijumuisha Uganda, Rwanda na Kenya mkurugenzi mkuu wa bodi inayosimamia utalii Kenya Dr. Betty Addero Radier, anasema watafikia masoko mapya na itaiwezesha Kenya kufikia lengo ililojiwekea la watalii milioni mbili ifikapo mwisho wa mwaka wa bajeti 2017-2018.

Mshiriki wa maonesho ya ITB kutoka Gambia
Mshiriki wa maonesho ya ITB kutoka GambiaPicha: DW/D. Pelz

Hiyo ikiwa kando na mikakati ya kutumia usafiri nafuu wa ndege itakayowafikisha watalii katika nchi hizo tatu. Maonesho ya kimataifa ya Utalii mjini Berlin ambayo hufanyika kila mwaka yanawakutanisha wadau muhimu katika sekta hiyo wakiwemo mawakala, kampuni za ndege, wahudumu wa hoteli miongoni mwa wengine.

Mbinu zisizochafua mazingira

Kauli mbiu ya maonesho ya mwaka huu ni, mwaka wa kimataifa wa utalii endelevu wa maendeleo, ambapo mojawapo ya masuala yanayohimizwa ni utoaji wa huduma za kitalii bila kuathiri mazingira. Mkurugenzi wa bodi ya utalii nchini Tanzania Devota Mdachi ameelezea kuwa maonesho haya ni kifungua macho kwao kuyaimarisha zaidi maonesho yao wenyewe kuwakuza wadau katika sekta hiyo ili waweze kuyalenga masoko mapya.

Uturuki pia imeelezea matumaini ya kuimarika tena kwa utalii wake ambao sasa unaoyumba baada ya idadi ya watalii wa kimataifa wanaozuru nchi hiyo kushuka kwa asilimia 30 mwaka jana kufuatia hofu za kiusalama.

Mwandishi: John Juma

Mhariri:Iddi Ssessanga