Mataifa yanayoinukia kiuchumi yamebadilisha wizani wa nguvu za kiuchumi duniani
12 Novemba 2010Mivutano kuhusu vita vya kibiashara pamoja na sarafu vilikuwa vikigonga vichwa vya habari katika mkutano wa siku mbili wa kundi la mataifa ya G20, lakini suala kuu ni jinsi mambo yanavyobadilika na kutoa kwa nchi zinazoendelea sauti kubwa zaidi katika meza ya kimataifa ya majadiliano.
Mabadiliko haya ya nguvu yanakisiwa katika taarifa ya pamoja iliyotolewa baada ya mkutano huo wa kundi la mataifa ya G20 uliomalizika jana Novemba 12, na kuonyesha kuwa wajumbe wamekubaliana kupanga ajenda elekezi pamoja na hatua za kuzuwia upunguzaji wa thamani za sarafu ambao unaleta athari badala ya malengo yaliyopangwa, ambayo kwa kawaida huweka mbinyo mkubwa kwa mataifa yanayoendelea.
Wito wa Marekani kuweka viwango maalum katika ziada za mauzo ya biashara, ambao haukupendelewa na China nchi ambayo ina ziada ya karibu dola bilioni 272 haukuidhinishwa na mkutano huo wa G20.
Badala yake viongozi wa kundi hilo la G20 wamesema katika taarifa yao ya pamoja baada ya mkutano wao kuwa wataandaa muongozo wenye viashirio kadha ambavyo vitasaidia kugundua na mapema uwiano mkubwa usio kuwa sawa wa kiuchumi ambao unapaswa kuchukuliwa hatua za kuzuiwa pamoja na kusahihishwa.
Rais Barack Obama amesema kuwa amemwambia rais wa China, Hu Jintao, kuwa mataifa yanayoinukia kiuchumi yanahitaji sarafu zao kuendeshwa na masoko na kwamba Marekani itaangalia kupanda kwa sarafu ya Yuan , ambayo maafisa wa China waliruhusu kupanda kidogo tu katika miezi michache iliyopita.
Mataifa mengine yanayoinukia kiuchumi kutoka Brazil hadi Thailand, yameachia sarafu zao kupanda katika kiwango cha juu cha miaka 15 iliyopita, kasi ambayo imesababisha benki kuu kuweka aina mbali mbali za udhibiti wa mitaji.
Utaratibu katika mkutano wa mwaka huu wa G20 uko katika sura ya ambapo mataifa yenye uchumi unaokua kwa haraka katika nchi zinazoendelea , kama China na India , wanachukua jukumu la injini ya kuendesha uchumi wa dunia wakati mataifa ya asili yenye nguvu , ikiwa ni pamoja na Marekani na Japan , yanazuiwa na ukuaji wa taratibu.
Mkutano wa Seoul umeonyesha vipi maafikiano yanavyoweza kwenda sambamba na madai ya mataifa yanayoinukia kiuchumi katika makubaliano ya mwisho, amesema profesa Kenzaburo Ikeda, mkuu wa taasisi ya utafiti ya Taijyu.
Ikeda , ambaye pia amekuwa akifuatilia mikutano ya kundi la G7 kama afisa , anasema kuwa matokeo ya mkutano huo ni kwamba mataifa tajiri hayawezi tena kuchukua jukumu la ukarimu, zikitoa fedha na kupunguza deni la nje, kwa mfano kama vile walivyokuwa wakifanya kwa mataifa masikini yanayoendelea.
Lakini kuna hisia kubwa miongoni mwa nchi zinazoinukia kiuchumi kuwa bado zinahitaji msaada na kusababisha hali ambapo madai katika meza ya majadiliano mjini Seoul yalikuwa hayalingani, anafafanua mwanauchumi Kensuke Kubo, mtaalamu kuhusu uchumi wa India ambaye yuko katika taasisi ya nchi zenye uchumi unaoinukia.
Mwandishi : Sekione Kitojo / IPS
Mhariri: Othman Miraji.