1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa ya G7 yatangaza vikwazo vipya dhidi ya Urusi

Iddi Ssessanga
19 Mei 2023

Kwenye mkutano wao wa kilele nchini Japan, viongozi wakuu wa G7 wamekubaliana juu ya vikwazo "kuidhoofisha Urusi kivita", siku chache tu kabla ya Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy kuhudhuria mkutano huo binafasi.

https://p.dw.com/p/4RZZL
Japan Hiroshima G7 Treffen 2023
Picha: Kenny Holston/NYT/AP/picture alliance

Viongozi wakuu wa mataifa ya G7 wamekubaliana Ijumaa juu ya vikwazo ambavyo wamesema vitainyima Urusi teknolojia ya G7, vifaa vya viwandani na huduma ambazo zinaisaidia kuendeleza vita vyake nchini Ukraine.

Hatua hizo ambazo zimetangazwa kwenye mkutano wa kilele unaofanyika mjini Hiroshima, Japan, zinahusisha vikwazo juu ya mauzo ya nje ya vifaa muhimu kwa Urusi katika uwanja wa vita, pamoja na kuzilenga taasisi zinazoshtumiwa kuipatia Moscow vifaa vya kivita.

Marekani na Uingereza zimetangaza vikwazo vipya dhidi ya Urusi mara tu baada ya viongozi kutoka kundi la mataifa makuu saba ya kiviwanda, G7, kuanza mkutano wao wa kilele nchini Japan Ijumaa.

Soma pia: Wakuu wa G7 wawasili Hiroshima tayari kwa mkutano wa kilele

London imesema inapanga kuzilenga almasi za Urusi, huku vyombo kadhaa vya habari vikiripoti kuwa Washington ilipanga kuzishughulikia taasis zinazoidadia Moscow kukwepa vikwazo vilivyopo.

Themenpaket G7 Summit Hiroshima Japan
Wakuu wa G7 wakiwa katika mkutano wa mchana mjini Hiroshima, Japan, Mei 19, 2023.Picha: KYODO via REUTERS

Kabla ya mkutano huo, wakuu wa mataifa na serikali za G7 waliweka mashada ya maua kwenye kituo cha kumbukumbu ya bomu la atomiki lililodondoshwa dhidi ya mji wa Japan wa Hiroshima mwishoni mwa Vita kuu ya Pili ya Dunia.

Katika taarifa yao ya pamoja wakati mkutano huo wa kilele ukiendela, mataifa ya G7yamesema yalikuwa yanaweka vikwazo zaidi na hatua kuongeza gharama kwa Urusi na wale wanaosaidia juhudi zake za kivita.

Taarifa ya G7imesema kundi hilo linajengea kwenye mafanikio ya juhudi zao kuhakikisha kwamba Urusi haiwezi tena kutumia upatikanaji wa nishati kama silaha dhidi yao na dhidi ya ulimwengu.

Soma pia: Kundi la mataifa yaliyoendelea ya G7 yanadaiwa na nchi maskini zaidi ya yuro trilioni 13 za misaada.

Imesema amani nchini Ukraine haiwezi kupatikana bila uondoaji kamili na usio na masharti wa vikosi vya Urusi na zana za kijeshi.

Viongozi hao wamesema walikuwa wanahuisha ahadi yao ya kutoa msaada wa kifedha, kiutu, kijeshi na kidiplomasia kwa Ukraine kwa kadiri itakavyohitajika.

Kundi la G7 kwa ujumla limeazimia kukaza vikwazo vilivyopo dhidi ya Urusi na kutangaza udhibiti zaidi wa mauzo ya mabilioni ya dola ya almasi kutoka Urusi.

Themenpaket - G7 Summit Hiroshima Japan
Viongozi wakuu wa mataifa ya G7 wakishiriki upandaji wa miti katika bustani ya kumbukumbu ya amani mjini Hiroshima, Japan, Mai 19, 2023.Picha: MINISTRY OF FOREIGN AFFAIRS OF JAPAN via REUTERS

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz alisema Berlin inataka hatua zenye utashi ili kuzuwia ukwepaji wa vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Urusi, akionekana kutuliza wito wa Marekani wa marfuku pana dhidi ya mauzo ya nje.

Soma pia: Viongozi wa G7 waanza kuwasili Japan kwa mkutano wa kilele

Marekani mapaka sasa imezuwia fedha za benki kuu ya Urusi, kuzuwia ushiriki wa benki za nchi hiyo katika mfumo wa miamala ya kifedha wa kimataifa wa SWIFT, na imeyawekea vikwazo maelfu ya kampuni za Urusi, maafisa wa serikali, matajiri wa taifa hilo pamoja na familia zao.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy atahudhuria mkutano huo mwenyewe siku ya Jumapili. Zelenskiy ambaye hii leo amewali mjini Jedda, Saudi Arabia kuhudhuria mkutano wa jumuiya ya mataifa ya Kirabu, atasafirishwa kwenda Hiroshima kwa kutumia ndege ya serikali ya Ufaransa.

Chanzo: Mashirika/DW