Marekani yapanga kuwaadhibu washirika wa NATO
24 Aprili 2026
Mawasiliano ya ndani kupitia barua pepe yanaonesha kuwa Pentagon imependekeza njia ambazo Marekani inaweza kuzitumia "kuwaadhibu washirika wake wa NATO", ambao inaamini walishindwa kuunga mkono vita vyake na Israel dhidi ya Iran, ikiwemo kusitisha uwanachama wa Uhispania na kupitia upya msimamo wa Marekani juu ya madai ya Uingereza kwa Visiwa vya Falkland.
Afisa mmoja wa ngazi za juu wa serikali ya Marekani aliliambia shirika la habari la Reuters mambo hayo ya kisera yamefafanuliwa kwa kina kwenye ujumbe unaoelezea jinsi Marekani ilivyokasirishwa na baadhi ya washirika wake kuikatalia ama kusitasita kuipa Washington ruhusa ya kutumia vituo na anga zake kwa ajili ya kuishambulia Iran.
Uhispania imejitokeza waziwazi kuwa mmojawapo wa wakosoaji wakubwa wa vita dhidi ya Iran, ikisema vinavunja sheria za kimataifa na za kibinaadamu.
Trump haridhishwi na NATO
Rais Donald Trump amekuwa akiyakosowa mataifa ya NATO kwa kushindwa kutuma meli zake kwenye Mlango Bahari wa Hormuz, ambao unapitisha asilimia 20 ya mafuta ghafi na gesi duniani, na ambao Iran imeamua kuuwekea udhibiti maalum baada ya kushambuliwa na Marekani na Israel.
Hata hivyo, mapendekezo ya Pentagon hayakufika umbali wa kutaka Marekani izifunge kambi zake za kijeshi barani Ulaya wala kuwaondosha maelfu ya wanajeshi wake waliopo barani humu.
"Kama Rais Trump alivyosema, licha ya yote Marekani iliyowatendea washirika wa NATO, wao hawapo kwa ajili yetu. Wizara ya Vita itahakikisha kuwa Rais ana chaguo la kufanya kuhakikisha kuwa washirika wetu sio tena chui wa karatasi na badala yake wanatenda wajibu wao." Alisema msemaji wa Pentagon, Kingsley Wilson, alipoulizwa kuhusu baruapepe hiyo.
Uingereza, Ufaransa na mataifa mengine yanasema kujiunga na mzingiro wa baharini wa Marekani hivi sasa kutamamaanisha kujiingiza kwenye vita dhidi ya Iran, lakini wanaweza tu kusaidia kuufungua Mlango Bahari wa Hormuz endapo kuna usitishaji mapigano wa kudumu ama vita vimemalizika.
Viongozi wa Ulaya wakutana Nicosia
Viongozi wa Umoja wa Ulaya walikuwa wanakutana mjini Nicosia nchini Cyprus siku ya Ijumaa (Aprili 24) kujadili hatua ya pamoja kwenye mzozo huo wa Mashariki ya Kati.
Haikufahamika ikiwa mkutano wao ungejadili kitisho hicho cha Marekani, lakini Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alisema wakati akiwasili mjini Nicosia kwamba "kurudi haraka eneo la Mashariki ya Kati kwenye utulivu, ni jambo lenye maslahi kwa kila mmoja."
Kwenyewe kwenye vita hivyo, uwezekano wa kuendelea kwa mazungumzo kati ya Marekani na Iran unazidi kufifia, huku Tehran ikishikilia msimamo wake wa kutokubali kujadiliana chini ya vitisho na shinikizo la Washington, nayo Washington kupitia kwa Trump ikiendelea kutoa matamshi yanayokinzana kila baada ya muda.