1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yatishia vikwazo vipya dhidi ya ICC

10 Desemba 2025

Utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump umetishia kuiwekea vikwazo vipya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC kama haitoahidi kuwa haitamshtaki kiongozi huyo na maafisa wake waandamizi mara tu atakapoondoka madarakani.

https://p.dw.com/p/555nb
Makao makuu ya ICC, The Hague, Uholanzi
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICCPicha: Lina Selg/ANP/AFP/Getty Images

Serikaliy ya Trump imeitaka Mahakama ya ICC kufanya marekebisho katika hati ya msingi ya kisheria ya kuanzishwa kwake, ili kuhakikisha haimchunguzi wala kumshtaki rais huyo wa Marekani hapo baadaye.

Kulingana na afisa wa utawala wa Trump aliyezungumza kwa sharti la kutokutajwa jina, utawala huo umeahidi vikwazo  dhidi ya mahakama hiyo kama itashindwa pia kuachana na uchunguzi wa awali dhidi ya wanajeshi wa Marekani kutokana na vitendo vyao nchini Afghanistan na kesi dhidi ya viongozi wa Israel.

Itakumbukwa kuwa mnamo mwezi Novemba mwaka 2024 Mahakama hiyo ya Kimataifa ya Uhalifu ilitoa waranti wa kukamatwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Waziri wake wa zamani wa Ulinzi Yoav Gallant, kutokana na vita vya Ukanda wa Gaza.

Mnamo mwezi Machi mwaka 2020 waendesha mashtaka walianzisha upepelezi nchini Afghanistan unaojumuisha uwezekano wa vitendo vya uhalifu vinavyoweza kuwa vilifanywa na wanajeshi wa Marekani. Tangu mwaka 2021 mahakama hiyo ilipunguza kipaumbele katika kuchunguza jukumu la Marekani katika suala hilo, lakini bado haijafuta rasmi upelelezi wake.

Vikwazo dhidi ya ICC kama taasisi na matokeo yake

Katika kuilazimisha ICC kufuta mashtaka haya, mapema mwaka huu, Marekani iliwawekea vikwazo maafisa tisa wa ICC wakiwemo majaji na waendesha mashtaka, lakini haikuiwekea mahakama hiyo vikwazo moja kwa moja kama taasisi, hatua ambayo ingeweza kutibua kwa kiasi kikubwa shughuli za mahakama.

Marekani imetishia kuiwekea vikwazo vipya Mahakama ya Kimataifa ya ICC kama itamshtaki au kumchunguza Rais wa Marekani Donald Trump
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Evan Vucci/AP Photo/picture alliance

Ikiwa Marekani itaiwekea vikwazo, itachochea zaidi kampeni ya kuipinga ICC, mahakama ambayo imekuwa ikikosolewa na maafisa wa Marekani wakiwemo wa vyama vyote vya siasa vya Republican na Democratic. Maafisa hao wanadai kuwa ICC inakiuka uhuru wa Marekani.

Chanzo kutoka katika utawala wa Trump kimesema kwa sasa, kuna wasiwasi mkubwa kuwa itakapofika mwaka 2029 ICC itammulika Trump, makamu wake, waziri wa ulinzi na wengine na kuanzisha mashtaka dhidi yao. Licha ya wasiwasi huo chanzo hicho hakikusema ni masuala gani hasa yanayoipa wasiwasi serikali ya Trump yanayoweza kusababisha kuchunguzwa na mahakama hiyo.

Kulingana na Afisa huyo wa Trump, Marekani imeshawasilisha matakwa yake kwa nchi wanachama wa ICC ambao wengine ni washirika wake na pamoja na mahakama hiyo. Marekani hata hivyo siyo sehemu ya Mkataba wa Roma ulioianzisha ICC kama mahakama ya mwisho yenye mamlaka ya kuwashtaki wakuu wa nchi.