1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani Uingereza na Australia zazindua muungano wa usalama

16 Septemba 2021

Marekani, Uingereza na Australia zimetengaza kuwa zimeanzisha ushirikiano wa kiusalama katika eneo la Indo-Pasifiki ambapo Australia itasaidiwa kupata manowari zitakazokuwa zinatumia nguvu za nyuklia.

https://p.dw.com/p/40Nb1
USA I Washington I Präsident Joe Biden
Picha: Andrew Harnik/abaca/picture alliance

Muungano huo uitwao AUKUS, umetangazwa na Rais wa Marekani Joe Biden, Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson na Waziri Mkuu wa Australia Scott Morrison.

Katika tangazo lililotolewa kwa pamoja kupitia njia ya video kutoka miji mikuu ya nchi zao, viongozi hao wamesisitiza kwamba Australia itakuwa haiweki silaha za nyuklia bali itakuwa inatumia mifumo inayoendeshwa na nyuklia katika manowari hizo, kwa ajili ya kujilinda kutokana na vitisho vya siku zijazo.

Ni hatua itakayoifanya dunia kuwa salama

Rais wa Marekani Joe Biden ameelezea sababu ya Marekani kuchukua hatua hiyo.

"Huku ni kuekeza katika chanzo chetu kikubwa cha nguvu, miungano, na kuiboresha kwa ajili ya vitisho vya leo na kesho. Ni kwa ajili ya kuwaunganisha marafiki na washirika wa sasa wa Marekani kwa njia mpya na kuuongeza uwezo wetu wa kuwasiliana, tukifahamu kwamba hakuna mipaka yoyote, inayotenganisha nia za washirika wetu wa Atlantiki na Pasifiki," alisema Biden.

USA I Washington I Präsident Joe Biden
Rais wa Marekani Joe Biden akimsikiliza Waziri Mkuu Scott Morrison wa AustraliaPicha: Oliver Contreras/abaca/picture alliance

Waziri Mkuu wa Uingereza, Johnson, amesema ni uamuzi muhimu kwa Australia kupata teknolojia itakayoiwezesha kuziendesha manowari hizo na zaidi ya hayo dunia itakuwa salama kutokana na muungano huo.

Naye Waziri Mkuu wa Australia Morrison amesema manowari hizo zitatengenezwa katika mji wa pwani ya Australia wa Adelaide kwa ushirikiano wa karibu na Marekani na Uingereza. Morrison baadae alisema pia kwamba Australia itapata makombora ya masafa marefu aina ya Tomahawk kutoka Marekani.

Haya yote yanajiri wakati ambapo ushawishi wa China katika eneo hilo ukiwa unaongezeka. China mara kadhaa imeukosoa utawala wa Rais Biden ambao umejaribu kuwa na matazamo mpya wa sera ya kigeni ya Marekani katika eneo la pasifiki.

Waaustralia wengi wanaunga mkono kupigwa marufuku silaha za nyuklia

Ufaransa haijafurahishwa na ushirikiano huo kwa kuwa ilikuwa na maelewano na serikali ya Australia kuhusiana na kuiuzia manowari za mabilioni ya fedha. Waziri Mkuu wa Australia Morrison amethibitisha kwamba nchi yake sasa imejiondoa kutoka kwenye mkataba huo na Ufaransa.

Trident
Manowari ya Marekani inayoendeshwa na nguvu za nyukliaPicha: picture-alliance/PA

Ufaransa kupitia taarifa iliyotolewa na wizara yake ya mambo ya nje imesema hatua hiyo ya Australia kununua manowari za Marekani ni kinyume na maelewano yao na ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.

Ndani ya Australia kwenyewe muungano huo pia tayari umepata pingamizi. Kundi la mazingira la Greenpeace Australia Pacific, kupitia kwa mkuu wake wa utafiti na uchunguzi Nikola Casule, limesema Australia haitokuwa salama na manowari hizo za nyuklia itakazopata na isitoshe Waaustralia wengi wanaunga mkono marufuku ya kudumu ya silaha za nyuklia.

Vyanzo: AFP/AP/Reuters