1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China: mivutano inaharibu juhudi za mabadiliko ya tabianchi

2 Septemba 2021

Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi ameuonya mjumbe wa Marekani wa mabadiliko ya tabianchi John Kerry kwamba kuzorota kwa uhusiano kati ya mataifa yao kunadhoofisha juhudi za kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

https://p.dw.com/p/3znQj
US-Klimabeauftragter John Kerry
Picha: Christophe Ena/AP/picture alliance

Wang amemueleza hayo Kerry kwa njia ya vidio akiongeza kwamba ushirikiano wa aina hiyo hauwezi kutenganishwa na uhusiano jumla kati ya nchi zao. Taarifa ya wizara ya kigeni ya China imesema kwamba Wang ameishauri Marekani kuchukua hatua za kuimarisha uhusiano wao kwa jumla.

Kerry ambaye yuko katika mji wa China wa Tianjin kwa mazungumzo yanayohusu masuala ya mabadiliko ya tabianchi, amesema Marekani iko tayari kushirikiani na ulimwengu mzima kupambana changamoto hiyo na kuitaka China kuchukua hatua zaidi za kupunguza uzalishaji wa hewa chafu angani.

Soma zaidi: Dunia inahitaji hatua thabiti za kulinda mazingira

Waziri huyo wa zamani wa mambo ya kigeni wa Marekani, pia amesema China ina jukumu muhimu sana katika juhudi za kukabiliana na chanagamoto ya mabadiliko ya tabianchi. Kwani China ndiyo inayoongoza katika kuchafua hewa ikifuatiwa na Marekani.

Klimakonferenz | Joe Biden
Rais Joe Biden akiwa na John KerryPicha: Evan Vucci/AP/picture alliance

Uhusiano kati ya Marekani na China umeharibika kutokana na mizozo inayohusu biashara, teknolojia na haki za binadamu. Lakini mataifa hayo mawili yamekubaliana kuwa kitisho cha mabadiliko ya tabianchi ni suala wanaloweza kushirikiana pamoja kupambana nalo.

Msemaji wa Wizara ya Kigeni ya China Wang Wenbin amesema ingawa China na Marekani zinatofautinana kwenye masuala kadhaa. Lakini wakati huo huo kuna mambo ambayo wanaweza kushirikiana ikiwa ni pamoja na suala la mabadiliko ya tabianchi.

China na Marekani zinapaswa kuheshimiana kwa manufaa ya nchi zao

Wang ameongeza kwamba pande zote mbili zinapaswa kuendelea na mazungumzo kwa kuheshimiana na kwa manufaa ya mataifa yao.

China ni taifa linalotumia makaa ya mawe kwa wingi ulimwenguni. Asilimia 60 ya nishati yake inatokana na  makaa ya mawe ambayo ni chanzo kikubwa cha gesi chafu.

Hata hivyo China inadhamiria kutumia njia mbadala ili kuzalisha asilimia 20 ya nishati inayohitajika nchini humo ifikapo mwaka 2025. Aidha inapanga kutozalisha gesi chafu ya kaboni ifikapo mwaka 2060 na kuanza kupunguza viwango hivyo kuanzia mwaka 2030.

Soma zaidi: Maoni: Lazima tuchukue hatua sasa kuhusu tabia nchi

Wakati huo huo Rais wa Marekani Joe Biden ametangaza lengo lake la kupunguza uzalishaji wa gesi chafu nchini humo kwa asilimia 52 ifikapo mwaka 2030, mara mbili ya viwango vilivyowekwa na Barack Obama katika mkataba wa Paris wa mwaka 2015.

Malengo ya mwaka 2030 yanaiweka Marekani katika ngazi ya juu ya mataifa yenye nia ya kupambana na tatizo la mabadiliko ya tabianchi.

Vyanyo: ap,rtre