1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Kombobild Biden und Jinping
SiasaAmerika ya Kaskazini

Biden, Xi wazungumza kwa mara ya kwanza baada ya miezi saba

Mohammed Khelef
10 Septemba 2021

Rais Joe Biden wa Marekani amezungumza na mwenzake wa China, Xi Jinping, kwa mara ya kwanza ndani ya kipindi cha miezi saba, wakijaribu kuuepusha ushindani uliopo baina yao kugeuka kuwa mgogoro.

https://p.dw.com/p/408k1

Ikulu ya Marekani, White House, ilisema kwenye mazungumzo hayo kwa njia ya simu, ujumbe wa Biden ulikuwa ni kwamba Marekani inataka kuhakikisha ushindani baina ya mataifa hayo makubwa duniani "unasalia kwenye kiwango ambacho hakutakuwa na hali yoyote ya kuwaingiza kwenye mgogoro usiokusudiwa."

Afisa mmoja wa Ikulu aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina, amesema mazungumzo hayo ya Alhamis (Septemba 9) yalijikita kwenye masuala makubwa ya kimkakati, ingawa hakuna uamuzi makhsusi uliofikiwa kati ya viongozi hao wawili. 

Jijini Beijing, kituo cha televisheni cha serikali, CCTV, kiliripoti kwamba mazungumzo hayo yalikuwa "ya kina na ya kiungwana" na yalikuwa juu ya "mkakati mpana wa mawasiliano na mabadilishano juu ya mahusiano ya China na Marekani na masuala ambayo yana maslahi kwa pande zote mbili". 

Mazungumzo hayo ya dakika 90 ni ya kwanza baina ya viongozi hao tangu mwezi Februari, walipozungumza kwa masaa mawili, muda mfupi baada ya Biden kumrithi Donald Trump. 

Kuharibika kwa uhusiano

China USA Treffen Joe Biden bei Xi Jinping in Peking
Mkutano wa mwaka 2013 kati ya ujumbe wa Marekani ukiongozwa na aliyekuwa makamu wa rais, Joe Biden, na wa China ukiongozwa na Rais Xi Jinping. Picha: Reuters

Uhusiano wa China na Marekani ulifikia pahala pabaya sana wakati wa utawala wa Trump, ambaye alianzisha vita vya kibiashara baina ya mataifa hayo yanayoshikilia nafasi ya kwanza na ya pili kwa uchumi mkubwa duniani. 

Ambapo utawala wa Biden unapigia debe ushirikiano wa kimataifa na kukomesha itikadi ya "Marekani Kwanza" iliyohubiriwa na Trump, bado umeendelea kubakia na vikwazo vya kibiashara vilivyowekwa na Trump dhidi ya China na takribani msimamo ule ule kwenye maeneo muhimu ya kimahusiano baina ya Marekani na China.

Ikulu ya White House imesema kwamba mkwamo wa kidiplomasia baina ya nchi hizo mbili si endelevu na ni hatari inayohitaji uingiliaji kati wa viongozi wakuu, na ndiyo sababu ya mazungumzo ya jana kwa njia ya simu.

Kwa mujibu wa Ikulu hiyo, lengo kuu lilikuwa kusafisha njia ya kuyawezesha mahusiano kusimamiwa vyema, ikiwemo kuhakikisha kuwa vitendo vya Marekani havitafsiriwi vibaya na China. 

Jitihada za ngazi za chini kuzungumza na China zimeshindwa, hasa baada ya mkutano uliokuwa na majibizano makali kati ya Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Antony Bliken, akisaidiwa na mshauri wa usalama Jake Sulivan, na maafisa wa ngazi za juu wa China walipokutana mjini Anchorage, Alaska, mwezi Machi mwaka huu. 

Kwenye mkutano huo, mkuu wa masuala ya kigeni wa chama cha Kikomunisti cha China, Yang Jiechi, aliituuhumu Marekani kwa kushindwa kushughulikia uvunjaji wa haki za binaadamu ndani ya mipaka yake na badala yake kuingilia mambo ya China, na kuuita huo kuwa ni unafiki wa Kimarekani.
 

Ruka sehemu inayofuata Mada zinazohusiana