Marekani na Israel zazuia ripoti za upelelezi | Matukio ya Kisiasa | DW | 06.11.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Marekani na Israel zazuia ripoti za upelelezi

Baada ya zaidi ya miezi miwili tangu ndege za kijeshi za Israeli kufanya mashambulizi ya siri kaskazini-mashariki ya Syria,serikali ya Marekani na wachambuzi huria wanazidi kuamini kuwa jengo lililolengwa lilikuwa kituo cha nyuklia.

Ushahidi unaotegemewa ni picha za sataliti zinazoonyesha jengo moja na pampu ya maji karibu na Mto Euphartes.Lakini ushahidi huo hautoi uhakika wa kutosha na pia majadiliano yaliyofanywa kati ya Marekani na Israel kuhusu tukio hilo ni siri inayolindwa vikali.Wachambuzi wa nchi za Magharibi wanasema,ndani ya jengo refu lililolengwa huenda ikawa kulikuwepo mtambo wa nyuklia uliokuwa ukijengwa sawa na ule wa Korea ya Kaskazini.Lakini mtambo huo uliteketezwa katika shambulizi la angani lililofanywa na Israel Septemba 6.

Ikiwa kituo kilicholengwa kilikuwa kweli kilikuwa na mtambo wa kinyuklia au la,mkasa huo pamoja na unyamavu wa Israel,Syria na Marekani kuhusu suala hilo huzusha masuala mengi.Kwa mfano,tishio halisi la kituo hicho-wakati wa kufanywa shambulizi hilo pamoja na hatua ya upande mmoja iliyochukuliwa na Israel,humaanisha nini kwa majirani wake walio na malengo ya kinyuklia.

Shirika la Nishati ya Nyuklia la Umoja wa Mataifa-IAEA limeomba kuonyeshwa ripoti za upelelezi zilizopelekea kufanywa shambulizo hilo. Vile vile shirika hilo linajaribu kupata habari zaidi kutoka Damascus kuhusika na madai ya mradi huo wa nyuklia.Kwani Syria inatakiwa kuiarifu IAEA harakati zo zote zinazohusika na nyuklia.

Juma lililopita,mkuu wa IAEA,Mohamed El-Baradei alisema,shirika hilo halikuwa na taarifa yo yote juu ya shambulizi lililofanywa.Amesema,ni matumaini yake kuwa kabla ya kupitishwa uamuzi wa kufanya mashambulizi ya bomu na kutumia nguvu, wahusika watawasiliana na shirika hilo kueleza wasiwasi wao,kwani wakaguzi wa IAEA wangepelekwa Syria kufanya uchunguzi wake.

Kwa maoni ya Ray Close,mchambuzi wa zamani wa shirika la upelelezi la Marekani CIA,uamuzi wa serikali ya Bush kutotoa habari za upelelezi kuhusu kituo cha Syria kwa shirika la IAEA huashiria kuwa Marekani inadhamiria kushughulikia peke yake suala la utapakaaji wa nyuklia duniani bila ya kushirikiana na jumuiya ya kimataifa isipokuwa kwa Israel kama polisi wa masuala ya nyuklia katika Mashariki ya Kati.

Close alipozungumza na shirika la habari la IPS akaongezea,serikali ya Israel ilipoishambulia Syria imeonyesha kuwa inatoa kipaumbele zaidi, kurejesha uaminifu wa nguvu zake za kijeshi kuliko kuunga mkono juhudi za kidiplomasia za Marekani kuendeleza mchakato wa amani wa Mashariki ya Kati,ambao ni ufunguo wa usalama halisi wa Israel.

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com