Mapinduzi ya Mauritania pigo kwa Umoja wa Afrika | Matukio ya Kisiasa | DW | 08.08.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mapinduzi ya Mauritania pigo kwa Umoja wa Afrika

Mapinduzi ya kijeshi nchini Mauritania,taifa lililotazamwa kama ni mfano wa demokrasia barani Afrika,ni pigo jipya kwa Umoja wa Afrika unaohang'aika kusuluhisha mizozo ya Darfur na Somalia barani Afrika.

President of Mauritania Sidi Mohamed Ould Cheikh Abdellahi addresses the 62nd session of the United Nations General Assembly, Wednesday, Sept. 26, 2007, at the U.N. headquarters. (AP Photo/Ed Betz)

Rais wa Mauritania,Sidi Ould Cheikh Abdallahi aliepinduliwa na maafisa wa kijeshi Jumatano,Agosti 6,2008.

Rais wa Mauritania Sidi Ould Cheikh Abdallahi alipinduliwa na majemadari siku ya Jumatano,muda mfupi tu baada ya kiongozi huyo kuwafukuza kazi baadhi ya maafisa waandamizi katika jeshi, wakituhumiwa kuchochea machafuko ya kisiasa.

Abdallahi alishika madaraka Machi mwaka 2007 baada ya kufanywa uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia nchini Mauritania tangu nchi hiyo kujinyakulia uhuru wake kutoka Ufaransa mwaka 1960.Uchaguzi huo ulisifiwa na Umoja wa Afrika kama ni mfano wa nchi inayojitoa kwenye utawala wa kijeshi na kukaribisha uongozi wa kiraia.Mauritania ilitazamwa na Umoja wa Afrika kama taifa lililofanikiwa kufanya mageuzi ya kidemokrasia,lakini sasa utaratibu huo umekwenda kombo.

Kwa mujibu wa Akuei Bona Malwal alie Makamu Balozi wa Sudan katika makao makuu ya Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa Ethiopia,umoja huo sasa unakabiliwa na changamoto mpya mbali na ile migogoro ya Darfur na Somalia.Hata hivyo anasema,kawaida wanachama katika umoja huo wanapokuwa na msimamo mmoja kuhusu suala fulani,basi hufanikiwa kama ilivyokuwa huko Komoro baada ya kikosi kidogo cha kijeshi kupelekwa kuisaidia serikali ya Shirikisho la Komoro kukidhibiti tena kisiwa kilichotekwa na kiongozi wa waasi.

Lakini suala la kuirejesha Mauritania kwenye mkondo wa kidemokrasia ni changamoto kali,kwani hapo kinachohusika ni mapinduzi ya kijeshi.Na sehemu ya changamoto hiyo,ni kuwa viongozi wa mapinduzi huenda wakaona shida kumrejesha madarakani yule kiongozi waliyomtimua.

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika,Jean Ping amesema,yeye anafuatiliza kwa makini matukio ya nchini Mauritania.Wakati huo huo Kamishna wa Amani na Usalama,Ramtane Lamamra ametumwa Mauritania kutathmini hali ya mambo nchini humo na vile vile kusaidia kupata suluhisho la amani kwa mgogoro huo mpya katika nchi hiyo ya Afrika ya Magharibi.

Hata Umoja wa Nchi za Kiarabu umetuma ujumbe wake nchini Mauritania kwa azma ya kuhifadhi usalama na utulivu pamoja na maendeleo ya kidemokrasia yaliyopatikana katika nchi mwanachama wa Umoja wa Nchi za Kiarabu.Umoja huo umewahimiza mahasimu wa kisiasa nchini Mauritania,kufanya mazungumzo na kuheshimu sheria za demokrasia.

Mapinduzi ya Mauritania yamelaaniwa kote barani Afrika.Wakati huo huo Marekani imezuia msaada wa zaidi ya dola milioni 20,usiohusika na huduma za kiutu.Lakini msaada wa chakula wa dola milioni 4.9 utaendelea kutolewa.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com