Maoni ya wahariri | Magazetini | DW | 16.02.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Maoni ya wahariri

Wahariri wanatoa maoni juu ya mkutano wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Ulaya na pia wanaitahadharisha Uturuki juu ya wazo lake la kupeleka majeshi nchini Syria.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel

Gazeti la "Badische Tagblatt "linasema mkutano wa kilele wa viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya utakaofanyika mwishoni mwa wiki hii utakuwa muhimu hususan kwa Kansela wa Ujerumani Angela Merkel.

Mhariri wa gazeti hilo anatilia maanani kwamba , ikiwa viongozi wa Umoja wa Ulaya hawatakubaliana juu ya suluhisho la pamoja,uzito wa Kansela Merkel utapwaya.

Mhariri huyo pia anakumbusha kwamba fedha ambazo Uturuki iliahidiwa bado hazijakusanywa na mipango ya dharura kwa ajili ya kuwasaidia wakimbizi haifanyi kazi kwa ufanisi. Na kwa hivyo huenda viongozi wa Umoja wa Ulaya wakajaribu kutafuta njia za kuurefusha muda tu.

Gazeti la "Der neue Tag" pia linasema mambo yamekaa kombo kwa Kansela Merkel .Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kwamba Kansela Merkel anatamani kuuona Umoja wa Ulaya ukizumgumza kwa sauti moja juu ya mgogoro wa wakimbizi. Lakini matamanio hayo sasa hayana msingi kwa sababu pamezuka kundi la nchi nne linaloitwa , " Visegrad "linalotofautiana naye.

Viongozi wa nchi za Visegrad wanaompinga Merkel

Viongozi wa nchi za "Visegrad" wanaompinga Merkel

Naye mhariri wa gazeti la "Flensburger Tageblatt" anauzungumzia mkutano wa jana wa mawaziri wakuu wa nchi hizo nne - Poland,Hungary,Jamhuri ya Czech na Slovakia.

Mhariri huyo anakumbusha kwamba hapo awali Kansela Merkel alikuwa mwanasiasa maarufu miongoni mwa nchi hizo za Ulaya ya kati. Lakini tangu Kansela huyo, aonyeshe ukarimu mkubwa kwa wakimbizi , na tangu atoe pendekezo juu ya kugawana wakimbizi hao kwa njia ya haki, nchi hizo nne, sasa zimegeuka kuwa mahasimu wa kiongozi huyo wa Ujerumani.

Ni maoni ya nchi hizo zinazoitwa "Visegrad" kwamba sera ya Ujerumani juu ya wakimbizi si sahihi.

Mpango wa Uturuki kupeleka majeshi Syria ni hatari

Gazeti la "Hannoversche Allgemeine" linaitahadharisha Uturuki juu ya mpango wake wa kupeleka majeshi nchini Syria. Mhariri wa gazeti hilo anasema mpango huo ni wa hatari! Anaeleza kwamba wakati wote Uturuki inakuja na vitendawili. Sasa inafikiria juu ya kupeleka majeshi nchini Syria. Mpango huo utaifanya hali iwe ya kutatanisha zaidi nchini Syria.

Wakurdi wanaozingatiwa kuwa washirika wa Marekani, katika kupambana na magaidi wa dola la kiislamu , ni magaidi kwa Uturuki. Gazeti la Hannoversche, linaiambia Uturuki wazi kwamba majeshi yake nchini Syria yanaweza kuvaana na yale ya Urusi, na kwa hivyo isitumai kuona mshikamano wa nchi nyingine za NATO.

Mwandishi:Mtullya abdu,Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Yusuf Saumu

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com