Maoni ya wahariri | Magazetini | DW | 29.07.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Maoni ya wahariri

Wahariri wa magazeti wanauzungumzia mtanziko unaoikabili Uturuki kuhusu magaidi wa dola la kiislamu na wapiganaji wa Kikurdi Pia wanatoa maoni juu ya mchango wa Umoja wa Ulaya katika kulinda amani nchini Mali

Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Ursula von der Leyen na mwenzake wa Mali Tieman Hubert Coulibaly

Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Ursula von der Leyen na mwenzake wa Mali Tieman Hubert Coulibaly

Gazeti la "Nürnberger Nachrichten" linasema ndege za Uturuki zinawashambulia wapiganaji wa Kikurdi badala ya kuwakabili magaidi wanaoitwa dola la Kiislamu.

Mhariri huyo anatilia maanani kwamba kile ambacho Marekani imekuwa inakisubiri, kutoka Uturuki, yaani mashambulio dhidi ya magaidi wa dola la kiislamu hayajaonekana dhahiri.


Mhariri wa "Nürnberger Nachriten" anaeleza kuwa, hali iliyopo,haileweki vizuri,kwa sababu,Uturuki inachukua hatua zinazowafanya watu washindwe kupambanua baina ya adui na rafiki wa nchi hiyo.

Gazeti la "Neue Presse" linasema ilikuwa mapema mno kuisifu Uturuki kuhusu harakati za kupambana na magaidi wanaoitwa dola la kiislamu.Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kwamba ni kweli, ndege za Uturuki zinafanya mashambulio kwenye ngome za dola la kiislamu, lakini wakati huo huo zinawatandika wapiganaji wa kikurdi.

Uturuki inafikiri kwamba, kwa kushiriki katika mfungamano dhidi dola la kiislamu itaweza kuzituliza lawama zinazotolewa juu yake kuhusu Wakurdi.Umoja wa Ulaya usikubali demokrasia itiwe kitanzi nchini Uturuki.

Naye mhariri wa gazeti la "Main Post" anasema sera ya Marekani ya kuiunga mkono Uturuki katika kuwashambulia wapiganaji wa kikurdi yumkini inatokana na kuitambua hali halisi, lakini athari zake zinaweza kuwa kubwa.

Mali yahitaji msaada wa kijeshi na kiuchumi

Gazeti la "Rheinpfalz" linazungumzia juu ya mchango wa Umoja wa Ulaya katika kulinda amani nchini Mali na linasema kwamba Umoja wa Ulaya ulichukua hatua za haraka nchini Mali ili kuepusha hali kama ile iliyotokea nchini Syria ambako makundi yenye itikadi kali yamejiingiza.

Hata hivyo Mali bado inategemea msaada wa majeshi ya Ufaransa na ya Umoja wa Mataifa. Lakini sasa mpango unaoleta matumaini umeanza kutekelezwa , utakaozuia watu kuikimbia nchi yao. Na mhariri wa "Eisenacher Presse" anatilia maanani kwamba ,Waziri wa ulinzi wa Ujerumani,Ursula von der Leyen amesema jambo sahihi, kwamba Mali inahitaji msaada wa muda mrefu.

Lakini gazeti hilo linasema kwamba msaada huo haupaswi kuwa kijeshi tu.Mali inahitaji kusaidiwa kijeshi,kidipolamsia na kiuchumi.Serikali ya Mali lazima iwe na uwezo wa kuwalipa askari wake .

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Iddi Ssessanga