Maoni ya wahariri juu ya vita vya nchini Iraq | Magazetini | DW | 12.06.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Maoni ya wahariri juu ya vita vya nchini Iraq

Wahariri wa magazeti wanatoa maoni juu ya vita vya nchini Iraq, silaha zinazouzwa nje na Ujerumani na pia wanatoa maoni juu ya mpango wa Ujerumani wa kuwapokea wakimbizi zaidi wa Syria

Askari wa Iraq watimua mbio

Askari wa Iraq watimua mbio

Juu ya vita vya nchini Irak, gazeti la "Darmstädter Echo" linasema baada ya Syria, nchi nyingine imo katika hatari ya vita na kusambaratika. Na wakati huo huo pana hatari ya kuzuka nchi nyingine ya kigaidi. Gazeti la "Darmstädter Echo"linasema nchi za Ulaya na za magharibi kwa jumla zinapaswa kuwa na wasi wasi juu ya yanayotokea nchini Iraq.

Mwito wa al-Maliki

Gazeti la "Thüringische Landeszeitung" linauzungumzia mwito wa Waziri Mkuu wa Iraq al-Maliki kwa Marekani. Mnamo mwezi wa Mei al-Maliki aliiitaka Marekani ifikirie juu ya kufanya mashambulio ya ndege ili kuwavunja nguvu wanaitikadi kali wa kisuni.

Juu ya maombi hayo gazeti la "Thüringische Landeszeitung" linasema ikiwa Marekani haikuyasikia basi imefanya kosa kubwa nchini Irak,kuanzia kuivamia na kuikalia nchi hiyo,kuziteketeza taasisi zake za dola hadi kumwamini Waziri Mkuu al-Maliki ,mtu asiyekuwa na uwzo wa kuleta umoja nchini mwake. Kutokana na hali hiyo,pemetokea ombwe la kiutawala,ambalo sasa linatumiwa na magaidi.

Gazeti la "Mannheimer Morgen" nalo linasema wanaitikadi kali wa kiislamu hawalengi tu shabaha ya kumwangusha Assad nchini Syria bali pia nchini Iraq wamekuwa wanapigana muda mrefu dhidi ya Waziri Mkuu Nuri al-Maliki ambaye ni Msuni. Chuki baina ya Wasuni na Washia inavuka mipaka ya nchi.Gazeti hilo linasema hiyo ndiyo sababu kwamba sasa pana uwezekano wa kuongezeka idadi kubwa sana ya wakimbizi.

Biashara ya silaha za Ujerumani

Mauzo ya silaha za Ujerumani katika nchi za nje yameongozeka hadi kuvuka Euro Bilioni 5,8 Hilo ni ongezeko la asilimia 25.Ujerumani iliziuza silaha hizo pia kwa Saudi Arabia na Qatar. Gazeti la "Stuttgarter Nachrichten" linasema Ujerumani inapaswa kuziimarisha taratibu zake za udhibiti katika nchi zinazonunua silaha hizo. Silaha kama vifaru kupelekwa Saudi Arabia na Qatar na kutumika nchini Syria siyo uamuzi unaowafiki na sera ya Ujerumani. Uuzaji wa bidhaa nje unapaswa kuisaidia sekta ya viwanda ya Ujerumani iwe sambamba na nchi nyingine katika maendeleo ya tekinolojia. Lakini gazeti la "Stuttgarter Nachrichten" linasema hayo yatawezekana ikiwa Ujerumani itashirikiana na washirika wake wa Umoja wa Ulaya, badala ya kutumbukia katika mkondo wa mashindano ya bei unaosababisha madhara.

Mhariri wa gazeti la "Lausitzer Rundschau"anasisitiza juu ya kauli ya Makamu wa Kansela Sigmar Gabriel kuhusu Ujerumani kupunguza mauzo ya silaha nje.Mhariri huyo anasema sera ya uwazi peke yake haitaiondoa Ujerumani kwenye nafasi ya pili duniani katika uuzaji wa silaha.Kinachotakiwa ni kujizuia kwa hiari katika biashara hiyo.

Wakimbizi wa Sryia

Ujerumani inakusudia kuwapokea wakimbizi zaidi kutoka Syria.Idadi inayolengwa ni 10,000 zaidi. Lakini gazeti la "Münchner Merkur " linahoji kwamba idadi hiyo ni aibu.

Gazeti hilo linasema kwamba Ujerumani haiwezi kujivunia idadi hiyo. Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa nchi kama Lebanon yenye wakaazi Milioni nne imewapokea wakimbizi wa Syria Milioni moja .Uturuki pia inawahifadhi wakimbizi wa Syria Milioni moja. Kinachoitwa ukarimu na utayarifu wa kuwapa wakimbizi 30,000 wa Syraia hifadhi katika nchi za Ulaya ni fedheha.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Yusuf Saumu