1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini: Marekani na sera yake ya Mashariki ya Kati

Zainab Aziz
9 Agosti 2018

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanatoa maoni juu ya ugeugeu wa Marekani katika sera yake ya Mashariki ya Kati na pia juu ya makubaliano yaliyotiwa saini baina ya Ujerumani na Uhispania kuhusu wakimbizi.

https://p.dw.com/p/32svz
USA Donald Trump und sein Schiegersohn Jared Kushner im Weißen Haus
Picha: Reuters/K. Lamarque

Badische Tagblatt

Juu ya sera mpya ya Marekani katika Mashariki ya Kati gazeti la "Badische Tagblatt'' linatilia maanani  kwamba Rais Donald Trump na Jared Kushner mkwe wake ambaye pia ni mshauri wake mkuu wameamua kusimama katika upande wa Israel na kwa kufanya hivyo Marekani imekiuka siasa yake ya miongo kadhaa juu ya Mashariki ya Kati na imezika suluhisho la nchi mbili. Hata hivyo mtu anaweza kuwa na maoni tofauti juu ya mageuzi hayo lakini jambo moja ni wazi  kabisa kwamba sera ya Marekani ya hapo awali katika Mashariki ya Kati imeshindikana japo ilikuwa malengo ya dhati.

Juu ya makubaliano yaliyofikiwa baina ya Ujerumani na Uhispania kuhusu wakimbizi mhariri wa gazeti la "Frankfurter Rundschau anatilia maanani kwamba makubaliano hayo yanalenga shabaha ya kuwazuia wakimbizi kuingia Ujerumani. Hata ikiwa makubaliano hayo yatatekelezwa, manufaa yake yatakuwa madogo sana sababu ni kwamba mkataba husika utawaahusu watu wachache sana. Na kwamba kuzisukumia nchi za kusini mwa Ulaya wajibu wa kulishughulikia suala la uhamiaji hakutaleta manufaa yoyote.

Neue Osnabrücker

Mhariri wa gazeti la "Neue Osnabrücker " anakubaliana na tathmini hiyo pia anasisitiza katika maoni yake  kwamba makubaliano hayo ni sawa na kujaribu kuikausha bahari kwa kutumia ndoo moja. Hata hivyo mhariri huyo anatilia maanani kwamba moyo wa mshikamano baina ya nchi za Ulaya bado upo.Na kwa sababu hiyo waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Horst Seehofer anaweza kuwa na haki ya kufurahia mafanikio.

Straubinger Tagblatt

Nalo gazeti  la "Straubinger Tagblatt " katika mada hiyo hiyo kuhusu wakimbizi linawaambia wale wanaomtuhumu waziri Seehofer kwa kuendesha siasa za kizalendo kama sehemu ya kampeni ya uchaguzi katika jimbo la Bavaria, wanapaswa kutambua kwamba malengo yake ni ya dhati na hayakugonga mwamba, kabla ya juhudi kuanza kufanyika kama wale wanaomkosoa wanavyotaka kuamini. 

Ludwigsburger Kreiszeitung

Mhariri wa gazeti la "Ludwigsburger Kreiszeitung" anayatilia mashaka manufaa ya mkataba uliofikiwa baina ya waziri Seehofer na Uhispania. Anasema kwanza idadi ya wakimbizi watakaohusika haijulikani.

Hata hivyo mhariri huyo anatilia maanani kwamba Uhispania haikutaka chochote kama zawadi kwa kutia saini makubaliano hayo ya kuwarudisha wakimbizi katika nchi hiyo. Mambo yalikuwa tofauti kuhusu Italia na Ugiriki ambako wako wakimbizi wengi wanaoingia katika nchi hizo kwa njia ya bahari. Bado haijajulikana iwapo makubaliano yatafikiwa baina ya Ujerumani na nchi hizo mbili. Ndiyo sababu kwamba waziri huyo wa mambo ya ndani anapaswa kuchukua hatua.Yeye ndiye mwenye wajibu.

Handelsblatt

Gazeti la masuala ya kiuchumi "Handelsblatt" linaushauri Umoja wa Ulaya usimame kidete ili kuyatetea maslahi yake. Linasema pengo kati ya Ulaya kutaka kuwa na nguvu na uhalisia wa mambo ni kubwa, katika siasa za dunia. Mhariri wa gazeti hilo anasema bara la Ulaya limebakia kuwa bara la kutamani kuwa kubwa duniani. Yafaa kutambua kwamba China inatetea maslahi yake na ikibidi kwa kuchukua hatua thabiti kama jinsi inavyoonekana katika mpango wake wa maendeleo wenye shabaha ya kuiunganisha dunia nzima kwa manufaa yake. Hata Urusi isiyokuwa na nguvu kubwa za kiuchumi nayo pia inatetea maslahi yake. Inaweza hata kulitetemesha bara la Ulaya. Bara la Ulaya mpaka sasa linajaribu kuonyesha nguvu kwa kauli tu!

Mwandishi: Zainab Aziz/ Deutsche Zeitungen

Mhariri.   Sekione Kitojo