1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maas: Ujerumani yapinga Urusi kurudishwa G7

27 Julai 2020

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas amesema haoni uwezekano wa Urusi kurudishwa katika kundi la mataifa yenye nguvu za kiuchumi duniani G7 hivi karibuni, kufuatia pendekezo la rais wa Marekani Donald Trump.

https://p.dw.com/p/3fxro
Griechenland Athen | Bundesaussenminister | Heiko Maas
Picha: Imago Images/T. Imo

Ujerumani imekataa ombi lililowasilishwa na Rais Donald Trump wa Marekani la kutaka Urusi irudishwe katika kundi la mataifa saba yenye uwezo mkubwa wa kiuchumi duniani G7, amesema waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas katika mahojiano yaliyochapishwa katika gazeti la Rheinische Post Jumatatu.

"Sababu ya Urusi kutolewa katika kundi la G7 ni uingiliaji wake katika eneo la Mashariki mwa Ukraine, na kuiteka rasi ya Crimea. Kama bado hakujapatikana suluhu huko, sioni nafasi ya kuiruhusu tena Urusi ndani ya G7”, alisema Maas.

Urusi iliondolewa kutoka kundi la G7 mwaka 2014 baada za Moscow kuiteka rasi ya Crimea kutoka kwa Ukraine.

Trump amependekeza upanuzi wa nchi za G7 na tayari amesema anapanga kuzialika Australia, India, Urusi na Korea Kusini kwa mkutano unaofuata wa G7 ambao anapanga kuwa mwenyeji mnamo mwezi Septemba. Mkutano huo uliahirishwa kutokana na janga la virusi vya Corona.

Maas: Uhusiano na Urusi kwa wakati huu ni mgumu

G7 - "Kundi la mataifa Saba" lilikuja pamoja mwaka 1975 kama mataifa saba muhimu yaliyoendelea zaidi kiviwanda wakati huo.

Nchi wanachama wa G7 ni Uingereza, Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan na Marekani. Mwaka 1998 Urusi iliongezwa kwenye kundi hilo na kuwa G8 lakini baadaye iliondolewa.

Maas amesema uhusiano na Urusi kwa wakati huu ni mgumu katika kila sehemu. Juu ya hayo, ameikosoa Urusi kwa kuzuia kupelekwa kwa misaada ya kibinadamu kwa kiasi ya watu milioni 1.5 nchini Syria.

Waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani ameitolea wito Urusi kuongeza juhudi za kumaliza mzozo mashariki mwa Ukraine, Syria na Libya.