1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandalizi ya michuano ya AFCON 2027 yashika kasi

23 Aprili 2026

Wajumbe wa mataifa matatu ya Afrika Mashariki ambao wanahusika katika maandalizi ya michuano ya Kombe la Afrika maarufu kama AFCON mwaka ujao 2027, wameahidi kujitahidi zaidi katika kutekeleza maandalizi hayo.

https://p.dw.com/p/5Ci9N
Tansania Arusha 2026 | Bau des neuen Stadions für den Afrika-Cup 2027
Picha: Veronica Natalis/DW

Baada ya kufanya tathmini yao, ujumbe wa ngazi ya juu wa Shirikisho la Soka barani Afrika CAF umeorodhesha masuala kadhaa ambayo waandalizi kutoka Kenya, Uganda na Tanzania wanatakiwa kuzingatia.

Kufuatia ziara zao katika mataifa yote matatu pamoja na kisiwani Zanzibar, ujumbe wa  kiufundi wa CAF umekutana na kamati za maandalizi kutoka Kenya, Tanzania na Uganda kufahamisha zaidi kuhusu masuala nyeti ya maandalizi ya michuano ya AFCONmwaka 2027.

CAF imehimiza kuharakishwa kwa ujenzi wa nyenzo mbalimbali ambao unaendelea katika nchi hizo lakini kwa kuzingatia viwango stahiki kwa michuano hiyo ya kimataifa. Wallace Karia ambaye ni rais wa sasa wa shirikisho la Soka Tanzania TFF ameiambia DW kwamba wanajitahidi ipasavyo kuwekeza katika miradi husika kwa usaidizi wa serikali na umma katika mataifa yote matatu.

"Kikao hiki kinaanza kutupa changamoto ya kutekeleza ushauri na maelekezo yaliotolewa na CAF tunayafuata kuhakikisha kwamba tunafanya vizuri na mwezi Agosti patakuwa na ukaguzi mwingine angalu tuwe kwenye asili mia zaidi ya 80”

Wajumbe wa kundi la maandalizi wa mashindano hayo kutoka mataifa hayo matatu chini ya jukwaa lao lijulikanalo kama  "Pamoja” wamefahamisha kuwa changamoto kubwa kwao inatokana na viwango vilivyowekwa na Morocco katika michuano iliyofanyika mapema mwaka huu.

Michuano inatoa fursa kubwa kwa vijana

Kufuatia uzoefu waliopata katika michuano ya CHAN iliyofanyika katika mataifa hayo matatu, rais wa shirikisho la soka Uganda Moses Magogo ameelezea kuwa wanatakiwa kuhakikisha kuwa changamoto zilizojitokeza zinaepushwa.

"AFCON ni ya kiwango cha juu zaidi kama mara 20 ya CHAN kwa hiyo tunatakiwa kuwekeza zaidi ili kukidhi matarajio ya mashabiki na wanasoka wa kimataifa watakaokuja kwenye michuano hii”

Afrika-Cup 2025 | Finale | Marokko vs. Senegal | Der Pokal des Afrika-Cups
Picha: Thor Wegner/DeFodi Images/picture alliance

Wajumbe wa Pamoja wamezihimiza serikali zao na pia wananchi kutoa michango yao kwa hali na mali kwani matokeo mazuri ya maandalizi  yatawafungulia wanamichezo hasa vijana fursa nyingi maishani sambamba na kuchangia kwa uchumi wa Afrika Mashariki. Rais wa TFF Wallace Karia ameongezea hivi.

"Michuano hii inatoa fursa kubwa kwa vijana wetu kuthamini michezo kama kitega uchumi  na kubuni fursa nyingi kwao ndani na nje ya Afrika Mashariki”

Kulingana na ujumbe wa kiufundi wa CAF, kuna hatua nzuri katika maandalizi ya viwanja hasa kile cha Talanta nchini Kenya na pia kile cha Zanzibar. Wamewashauri wamiliki wa hoteli nao kujitahidi katika kuboresha nyenzo zao kuweza kukidhi matarajio ya wageni.