Leo mabingwa wa ulaya -Spain wana miadi na Ureno | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 29.06.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Leo mabingwa wa ulaya -Spain wana miadi na Ureno

Je, Cristiano Ronaldo atawika ?

default

Christiano Ronaldo Ureno na Xavi wa Spain (kushoto)

Baada ya mabingwa mara 5 wa dunia-Brazil- kuwatimua nje ya kombe la dunia jana jirani zao, Chile, kwa mabao 3-0 na kupanga miadi na Holland ilioitoa Slovakia kwa mabao 2:1, macho yanakodolewa leo katika mapambano mawili ya duru ya mwisho ya kundi la timu 16: Kwanza, Paraguay itateremka uwanjani alaasiri hii kujaribu kuzifuata Brazil, Argentina na Uruguay duru ijayo. Usiku wa leo ni "kufa-kupona" kwa majirani wawili: Mabingwa wa Ulaya-Spain- waliopo nafasi ya pili ya ngazi ya timu bora za FIFA na Ureno inayoshika nafasi ya 3. Ni changamoto pia kati ya Cristiano Ronaldo, upande mmoja, na David Villa, upande wapili.

Nani ana mbinu bora kati ya kocha Del Bosco na Carlos Quiroz. Na kuna tofauti gani kati ya Black Stars-Ghana- na timu nyengine 2 za Afrika-Kameroun na Senegal, zilizowasili hatua ya robo-finali ya Kombe la dunia ?

TIMU 3 ZA AFRIKA ZILIZOWASILI ROBO-FINALI:

Ghana, yenye miadi ijumaa hii ijayo na Uruguay, mabingwa mara 2 wa dunia kukata tiketi ya nusu-finali-hatua ambayo hakuna timu ya Afrika imeifikia, inatofautiana na wenzao wa hapo kabla- Simba wa nyika-Kameroun na Senegal, wanadai wachambuzi kwa kuwa wao hawana nyota maalumu katika kikosi chao. Kinyume na ilivyokuwa na wenzao: Kameroun, 1990 huko Itali, ilitamba na mzee Roger Milla na Senegal, 2002 huko Korea ya Kusini na Japan, na mshambulizi wao El Hedji Diouf.

Nyota wa Ghana-Black Star- Michael Essien, aliumia na hakuichezea Ghana tangu Kombe la Afrika la mataifa, Januari mwaka huu nchini Angola, Ghana ilipotamba hadi finali na Misri na hata katika Kombe hili la dunia, huko Afrika Kusini.

BILA YA NYOTA TIMU ZACHEZA BORA ?

Hali hii, imeiwacha Ghana sawa na Ujerumani, iliomkosa nahodha wake Michael Ballack. Hata hivyo, chipukizi wa Ghana bila ya Essien, na wa Ujerumani bila ya Ballack wametamba.Bila ya mastadi wao, kuna timu zinazocheza kwa ari na kasi mpya.

Ghana , inaikabili Uruguay Ijumaa hii huko Soccer City Stadium kuania tiketi ya nusu-finali ilioikosa Kameroun dakika ya mwisho huko Itali,1990 pale bao la penalty la kutatanisha la Garry Leanecker wa Uingereza , lilipowazima simba wa nyika kipindi cha kurefushwa mchezo.

Kuna kitu kimoja kinazifungamanisha timu zote 3 za Afrika zilizowasili hatua hii ya robo-finali:Kameroun,Senegal na Ghana, zote zilishinda mpambano wao wa kwanza wa Kombe la dunia: Kameroun na Senegal zilitamba zaidi- kwavile, Kameroun iliilaza Argentina mabingwa watetezi na halkadhalika, Senegal,Ufaransa. Francois Omam-Biyek,aliishtusha Argentina na Maradona kwa bao lake huko Itali.Papa Bouba Diop,akaipiga kumbo Ufaransa duru ya kwanza kwa bao lake huko Asia.

KANDA YA AMERIKA KUSINI:

Upande wa kanda ya Amerika Kusini, wachambuzi wanadai duru kali ya kutoana jasho ya kuania nafasi za Kombe hili la dunia kanda ya Amerika Kusini na kuwa fit kwa changa-moto hizi , ndio sababu kwanini timu za kanda ya Amerika Kusini, zimetamba zaidi kuliko kanda ya ulaya: Hivyo, ndivyo anavyodai kocha wa Paraguay, Gerrado Martino, ambae timu yake ina kibarua cha kuthibitisha hayo kwa kuitoa leo nje Japan.

Martino anadai, timu za kanda ya Amerika Kusini, zinakumbana na shida zaidi hadi kukata tiketi zao za kombe la dunia. Brazil na Argentina, zinazoongoza kanda hiyo zilikata dakika za mwisho na ni ushahidi wa hayo. Martino anasifu jinsi wachezaji wa timu kama Brazil na Argentina, walivyo fit kuhimili zahama za Kombe la dunia. Anaongeza:

"Brazil na Argentina, daima ni mahasimu wakubwa katika kombe la dunia na wanakuja wakiwa kila mmoja kajiandaa barabara."

Timu nyengine 3 za kanda hiyo,halkadhalika , ni imara.Na vipi maandalio ya rifu katika Kombe hili la dunia baada ya duru ya kwanza na ya pili ?

Taarifa za hivi punde kutoka Johannesberg, zinasema rais wa FIFA, Sepp Blatter, ameomba msamaha tangu kwa Uingereza hata kwa Mexico kwa madhambi waliofanya marifu wa FIFA yaliochangia kupigwa kumbo timu hizo 2 nje ya Kombe la dunia. Akaahidi kuwa ,FIFA itafungua upya majadala motomoto iwapo au la matumizi ya teknolojia ya video yaruhusiwe kuamua kilichotokea.

Mwandishi:Ramadhan Ali/AFPE

Uhariri: Miraji Othman

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com