Lebanon haina rais wa nchi | Matukio ya Kisiasa | DW | 27.11.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Lebanon haina rais wa nchi

Lebanon iko katika mgogoro kwa kukosa kuwa na rais wa nchi.

default

Rais mstaafu wa Lebanon, Emile Lahoud(kushoto) na Rais wa Syria, Bashaar al-Asad.

+

Lebanon sasa iko katika hali ngumu, nchi hiyo haina rais. Wiki iliopita, kwa mara ya tano, bunge la nchi hiyo lilishindwa kuchagua rais wa nchi, na kuna maonyo kadhaa yaliotolewa kwamba Lebanon inaweza ikateleza na kuingia katika michafuko pindi pengo hili litaendelea kutojazwa kwa haraka kama iwezekanavyo.

Wiki iliopita, spika wa bunge, Nabih Berri, alikiahirisha kikao cha bunge hadi tarehe 30 mwezi huu wa Novemba, kwa vile hadi sasa hajachomoza mtu anayekubalika kukamata nafasi ya Emile Lahoud aliyemaliza muda wake wa urais ijumaa iliopita. Utata ni kwamba serekali ya waziri mkuu Fuad Siniora na upande wa upinzani hazijakuliana juu ya nani akamate nafasi hiyo. Emil Lahoud alikabidhi dhamana za usalama katika nchi hiyo kwa jeshi, japokuwa kwa mujibu wa kanuni alitakiwa akabidhi kwa serekali. Yeye alidai, kama unavodai upinzani kwamba serekali ya Fuad Siniora sio halali, kwa vile mawaziri sita walijitoa kutoka serekali hiyo tangu Novemba mwaka jana. Ilivokuwa hakuna mtu aliyechaguliwa kuwa rais, Emil Lahoud aligusia juu ya hatari ya kutangazwa hali ya hatari. Hivyo, mkuu wa majeshi, Michel Suleiman, mwenye umri wa miaka 59, ndiye mtu aliye na nguvu kabisa huko Lebanon kwa sasa. Uamuzi huo wenye utata wa kikatiba uliwekewa alama ya kuuliza na serekali ya Fuad Siniora ilio na mtizamo wa nchi za Magharibi. Hata Kadinali Nasrallah Sfeir, mkuu wa Wakristo wa madhehebu ya Maronite huko Lebanon, ameonya kwamba hivi sasa nchi hiyo iko katika kipindi cha mpito ambacho kinaweza kikapelekea utulivu au michafuko na malumbano. Kwa mujibu wa katiba ya Lebanon, rais wa nchi hiyo anatakiwa atokee kwenye jamii ya Wakrsito wa madhehebu ya Maronite.

Japokuwa serekali ya Fuad Siniora ilisema ilikuwa inabeba dhamana ya kuiendesha nchi hiyo, kuambatana na katiba, lakini upinzani, ukiongozwa na kikundi cha Hizbullah cha wanamgambo wa Kishia ambacho kilipigana vita na Israel mwaka jana, kinapinga tafsiri inayotolewa na serekali kuhusu madaraka yake ya kikatiba. Kwa mujibu wa Hizbullah, Lebanon sasa haina mamlaka yanayojikita kwa rais, na kwamba serekali ya waziri mkuu Fuad Siniora haiko, haiwezi kutawala na haiwezi kuchukuwa mamlaka aliyokuwa nayo rais.

Utata huu unatokana na mapambano baina ya wafadhili wa kigeni wa makundi mawili hayo ya huko Lebanon- Marekani na mshiriki wake mkuu, Saudi Arabia, zikiwa upande wa serekali, na Iran na mshirika wake mkuu wa Kiarabu, Syria, zikiwa upande wa upinzani. Tatizo hili linaweza kutanzuliwa kwa siku moja au kwa mwezi mmoja, kwa vile Lebanon imekuwa mhanga wa mivutano ya kimkoa, alisema mchambuzi wa mambo ya siasa, Profesa Sami Salhab. Alisema Lebanon imekuwa tena sanduku la barua ambapo kila taifa la kigeni linatuma risala kwa mataifa mengine ya kigeni.

Na zaidi tafauti baina ya makundi yanayoingua mkono Syria na yale yanayoipinga Syria huko Lebanon zimezidi kuwa kubwa, kama anavosema Ibrahim Moussawi, mhariri mkuu wa gazeti la Hizbullah la al-Intiqat:

Insert: O Ton Moussawi

+Nam sote tumo katika jahazi moja, yule ambaye hataki kutambua hilo, anahatarisha jahazi zima kuzama. Hapa sio suala la tafauti za maoni, lakini misimamo. Upande mmoja uko pamoja na Wamarekani. Haujafanya kitu kupinga Israel kuikalia Libanon, a katika vita vilivopita ulisaidiwa na Waisraeli kwa silaha na risasi. Upande mwengine ni wa upinzani. Huu ni mpasuko mkubwa ambapo mtu hawezi nchi kuijenga.+

Lakini sasa macho yanakodolewa huko Annapolis, Marekani, kunakofanyika mkutano wa amani juu ya Mashariki ya Kati baada ya Syria, katika dakika ya mwisho, kuamua kwamba itahudhuria, licha ya kwamba mshirika wake, Iran, inaupinga mkutano huo. Wachunguzi wa mambo wanasema mashauriano yote baina ya serekali na upinzani huko Beirut yatasita hadi baada ya mkutano huo wa Annapolis, na hakutakuweko juhudi zozote za kuukwamua mzozo huo hadi pale matokeo ya mkutano wa Annapolisi yatakapojulikana, na hasa vipi yatakavokuwa siku za mbele mahusiano baina ya Syria na Marekani. Bila ya shaka katika kutafuta suluhu baina ya Israel na Wapalastina, Syria inaweza ikatoa mchango muhimu, na jambo hilo likiwezekana itamaanisha kwamba Marekani imefaulu, kama hatua ya kwanza, ya kuuvunja ushirika ulioko sasa baina ya Syria na Iran.

Syria ilitangaza kwamba huko Annapolis itawakilishwa na waziri wake mdogo wa mambo ya kigeni, Feisal Mekdad, baada ya kusema kwamba imehakikishiwa kwamba kurejeshewa Milima yake ya Golan litakuwa jambo ndani ya ajenda ya mkutano huo. Mazungumzo ya amani baina ya Syria na Israel yalivunjika mwaka 2000 pale Israel ilipoyakataa madai ya Syria ya kutaka kurejeshewa ardhi yote ya Milima ya Golan hadi katika fukwe za Bahari ya Galillee, sehemu muhimu ambapo Israel inajipatia maji yake.

Vipi Syria na Israel zitakavokabiliana katiika mazungumzo ya Annapolis ni jambo litakalochangia sana katika matokeo ya mzozo wa kisiasa wa Lebanon. Ama suala la Syria kurejeshewa ardhi yake linafanya maendeleo, na Marekani itaitaka Syria iregeze kamba, ama suala la Syria kurejeshewa ardhi yake halifanyi maendeleo na Syria itazidi kutengwa. Katika njia zote hizo mbili, Syria itabidi iregeze kamba huko Lebanon.

Cha muhimu ni kwamba pande zinazopingana huko Lebanon zimeafikiana kwamba mzozo wao wasijaribu kuutanzuwa mabarabarani. Licha ya kwamba tarehe 30 mwezi huu wa Novemba imewekwa kuwa siku nyingine ya kufanya jaribio la kumpata rais, hata hivyo, haitarajiwi kwamba mafundo yalioko yataweza kutanzuliwa.

Timor Gocksel wa Chuo cha Kimarekani cha Beirut ana wasiwasi kama uvumbuzi utapatikana karibuni:

Insert: O Ton Gocksel…

+Kila mmoja hapa ana maslahi yake. Kila upande hautaki kuregeza kamba. Hapa sio suala la madhehebu ya kidini, lakini maslahi ya kila mmoja. Hatuwezi kutaraji kwamba watu hawa walioivuruga nchi sasa wataiokoa. Hata kidogo. Na kila mmoja wao ana dola ya nje inayomuunga mkono.. Suluhisho pekee ni kwamba madola hayo ya nje yaungane na tamko lao litekelezwe.+

Kumekuweko juhudi kadhaa za upatanishi, lakini zote zimeshindwa. Wafaransa, ambao walipongezwa na pande zote mbili, wamevunjika moyo na wameondoka Beirut.

Lebanon bado haijapona majaraha ya vita vyake vya kienyeji vya miaka ya thamanini na tisini. Vita hivyo vilijiketi katika tafauti za kidini na kimadhehebu, lakini mara hii mambo sivyo; tafauti zilioko ni za kinadharia. Upande wa serekali una muungano wa wanasiasa wa Kisunni, Kikristo, Kidruze, na upande wa upinzani kuna wanasiasa wa wa madehebu ya Shia na wa Kikristo. Katika mzozo wa sasa, Wakristo wa madhehebu ya Maronite wamegawanyika, licha ya kwamba katiba ya nchi inawahakishia wadhifa wa urais kuwa ni wao. Upinzani, na hasa Chama cha Washia cha Hizbullah, kinaiona serekali ya Fuad Siniora inapokea amri kutoka Marekani na nchi za Magharibi na inaituhumu itakuwa tayari kuregeza kamba sana kwa adui mkubwa wa Waarabu, Israel.

Mengi sasa yatategemea vipi mkuu wa majeshi Michel Suleiman atakavokuwa na maingiliano na serekali. Wakati yuko jeshini, jenerali huyo ambaye ni Mkristo, amedhihirisha mara nyingi hapo kabla kwamba anaweza kuleta wizani na kutilia maanani dini mbali mbali.

 • Tarehe 27.11.2007
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CTlC
 • Tarehe 27.11.2007
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CTlC
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com