1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kivumbi kikali kutarajiwa katika uchaguzi wa urais nchini Afghanistan

Jane Nyingi/ AFPE..Picha AFP14 Agosti 2009

Mpinzani mkuu wa Karzai, Abdullah Abdullah aendelea kuuvutia umati mkubwa wa watu katika mikutano yake.

https://p.dw.com/p/JBHz
Rais Hamid Karzai wa Afghanistan.Picha: AP

Mpinzani mkuu wa rais wa Afghanistan Hamid Karzai, Abdullah Abdullah ameendelea kuuvutia umati mkubwa wa watu katika mikutano yake, huku mashambulio yakizidi kuchacha uchaguzi mkuu unapokaribia tarehe 20 mwezi huu wa Agosti. Abdullah Abdullah ambae alikuwa zamani waziri wa mambo ya nje katika serikali ya Karzai, aliponea chupuchupu katika jaribio kumuuwa ikiwa ni wiki moja kabla ya uchaguzi huo .

Maelfu ya wafuasi wa Abdullah Abdullah walimkaribishwa kwa fijo na hoi hoi katika mkutano mkubwa alioufanya kaskazini mwa mji wa Mazari-i –Sharif ambao ni ngome yake. Katika mkutano huo Abdullah aliwaambia wafuasi wake na namnukuu“ msifikiri haya yamekwisha, msisikilize kile wengine wanachowaambia,uchaguzi huu ni vigumu kutabiri mshindi mwisho wa kumnukuu

Karzai anahitaji kupata ushindi wa zaidi ya asilimia 50 ya kura ili kuzuia kufanyika kwa raundi ya pili ya uchaguzi huo dhidi ya mpinzani wake wa karibu. Kura ya maoni iliyochapishwa na kampuni ndogo isiyojulikana nchini Marekani mapema wiki hii, inampa Karzai asilimia 45 ya kura huku Abdullah akiwa na asilimia 25.

Wataliban wameapa kuuvuruga uchaguzi huo na kufanya mashambulio hasa kusini mwa Afghanistan,eneo lilo na watu wengi kutoka kabila la rais Karzai la Pashtun. Idadi ndogo ya watu inayotarajiwa kujitokeza kushiriki katika uchaguzi huo hasa kusini mwa Afghanistan, kutokana na wasiwasi wa usalama, huenda ikachangia kupungua kwa kura za Karzai na kusababisha kufanyika kwa raundi ya pili ya uchaguzi huo mwezi October.

Abdullah ambae asili yake nusu ni mpashtun, kabila kubwa nchini Afghanistan, anaungwa mkono pia na idadi kubwa ya watu kutoka kabila la Tajik. Mkutano huo uliofanyika katika mji wa Mazar -i -Sharif karibu kilomita 300 kaskazini mwa Kabul, uliwavutia karibu wafuasi elfu 50 wa Abdullah,waliokuwa wamevalia kofia na mavazi mengine yaliyona picha za Abdullah.

Kwa upande mwengine Mashambulio nchini Afghanistan yalifikia kilele chake mwaka huu, tangu Wataliban kupinduliwa na vikosi vya Marekani vikisaidiwa na vile vya Afghanistan mwaka 2001.Baada ya hapo vikosi vya Marekani na vile vya Uingereza vilizindua operesheni kubwa kusini mwa mkoa wa Helmand.

JanaAlhamisi,wanajeshi watatu wa Uingereza waliuawa na bomu lilokuwa limetegwa kando mwa barabara katika eneo hilo la Helmand.Jumla ya wanajeshi 199 wa Uingereza wameuawa tangu kuanzishwa kwa vita nchini Afghanistan, karibu 30 tangu kuazishwa kwa mashambulio katika mkoa wa Helmand.

Operesheni katika mkoa wa wa Helmand ni ya kwanza tangvu aingie madarakani rais wa Marekani Barrack Obama,huu ukiwa ni mkakati mpya wa kukabiliana na Wataliban na kuleta hali ya uthabiti nchini Afghanistan.

Hata hivyo Wataliban wamejibu mshambulio hayo,na harakati zao kuenea Kusini na Mashariki na katika maeneo yaliyokuwa na utulivu zaidi ya Kaskazini na Magharibi na hata vitongoji vya mji mkuu Kabul. Karibu wanajeshi elfu 30 zaidi kutoka Marekani wamewasili nchini Afghanistan mwaka huu na hivyo kufikisha idadi ya vikosi kutoka nchi za magharibi kuwa zaidi ya laki moja kwa mara ya kwanza.

Mwandishi:Jane Nyingi

Mhariri:Abdul-Rahman