Kansela wa zamani wa Ujerumani Helmut Kohl afariki dunia | Matukio ya Kisiasa | DW | 16.06.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Kansela wa zamani wa Ujerumani Helmut Kohl afariki dunia

Kansela wa zamani wa Ujerumani, Helmut Kohl, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 87. Kohl alieiongoza Ujurumani kwa muda mrefu zaidi, anakumbukwa kwa kuiunganisha tena nchi na alichangia pakubwa kuinganisha Ulaya.

Aliekuwa Kansela wa Ujerumani Helmut Kohl ni mwanasiasa aliezitambua haraka alama za nyakati. Hakuchelewa kuutambua wasaa wa kuchukua hatua zilizowaunganisha tena Wajerumani.

Alipoulizwa kuhusu kujengwa mnara wa kumbukumbu wa kukumbusha juu ya kazi  yake, Helmut Kohl alijibu kwa utani kwa  kusema, kwamba wageni wakishaondoka, kwanza watakuja njiwa na halafu watakuja mbwa. Watakachokifanya njiwa na watakachokifanya mbwa hao kinajulikana.

Jina la Helmut Kohl lilipanda juu katika  historia, kutokana na umahiri wake wa kuongoza mambo, baada ya kuanguka kwa  kuta la Berlin na kuongoza hatua za  kuungana tena kwa nchi mbili za kijerumani. Hayo aliyoyafanya yangetosha kumjengea mnara wa kumbumbuku.

Gharama za kuungana upya Ujerumani

Kohl alisimama safu moja na watu wengi  mashuhuri duniani. Lakini kisiasa Kohl alikuwa amefikia mwisho mnamo mwaka wa kihistoria wa 1989. Wapinzani wake ndani ya chama  walisimama kidete dhidi yake: ulikuwa uasi dhahiri dhidi yake. 

Ni kwa taabu tu kwamba aliweza kuendelea kwa mara nyingine kuzishika hatamu za  uongozi wa chama  chake  cha CDU. Hata katika hali mbaya ya kiafya Kohl  aliweza kuonyesha ukakamavu.Yeye  ni  mtendaji  mwenye  umahiri. Ni mwanasiasa aliekuwa na uwezo  wa kutangamanisha silika ya uongozi thabiti  na mkakati wa utekelezaji.

Altbundeskanzler Helmut Kohl (picture-alliance/dpa/U. Baumgarten)

Kansela Helmut Kohl katika mkutano wa waandishi wa habari baada ya kikao cha mashauriano kati ya Ujerumani na Ufaransa mjini Bonn, 30.11.1993.

Na fursa  ya kuyathibitisha  hayo ilijitokeza:Jamhuri ya Kidemokrasia ya   Ujerumani - yaani Ujerumani Mashariki ya  hapo awali, ilisambaratika na kuta la Berlin  liliporomoka. Helmut Kohl  aliitambua fursa  hiyo ya kipekee na  hakuchelewa  kuchukua  hatua. Na alichukua hatua sahihi.

Kohl  alisimama bungeni  na kuuwasilisha  mpango  wa  vipengee  10 juu ya kuungana  tena  kwa nchi mbili za kijerumani. Aliichukua hatua hiyo  wiki tatu  baada ummati wa  watu  kutoka  Ujerumani mashariki kusongamana  kwenye vituo  vya kuvukia  mipaka katika mji   wa Berlin. Hiyo ilikuwa kazi ya umahiri  mkubwa .

Hata hivyo lengo la nchi mbili  za  kijerumani kuungana  tena lilisababisha hisia za mchanganyiko katika nchi  za nje. Lakini Kohl aliwakabili wale  waliokuwa na  mashaka kama mwanaulaya. Kama alivyofanya  pia  tarahe 19 mwezi  wa  Desemba mjini Dresden mbele ya maalfu ya raia wa Ujerumani Mashariki. Aliutumia ulimi wa nadhari mbele ya mkutano  wa  hadhara wa maalfu waliokuwa na jazba- mkutano ambao haukupangwa. Na aliweza  kupata  imani ya watu hao.

Umahiri wake wa kisiasa

Sambamba na maandalizi ya sera ya ndani  ya kuujenga umoja  wa nchi mbili  za  kijerumani, sera ya nje ya Helmut Kohl mnamo miaka hiyo, ilithibitisha umahiri wa serikali yake. Urafiki na Ufaransa, maridhiano na  Poland  na uhusiano katika msingi wa kuelewana na Urusi iliyodhoofika wakati huo, ni  ishara  za siasa  ya makini  ya Kohl  kwa nchi jirani.

Helmut Kohl alikuwa mtoto wakati wa vita  vikuu vya pili. Alikishuhudia kipindi cha magofu nchini Ujerumani alipokuwa kijana. Na yeye alikuwa mtetezi mkubwa wa rika linaloifuata sera ya kuhakikisha kwamba vita asilani havizuki tena kutokea Ujerumani.

Helmuth Kohl empfängt Netanjahu in Bonn (picture-alliance/dpa/M. Jung)

Kansela Helmut Kohl alipompokea waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu 06.03.1998 katika ofisi ya Kansela mjini Bonn kuzungumzia hali ya Mashariki ya Kati.

Ni kutokana na juhudi za mwanasiasa Kohl  kwamba Ujerumani iliyoungana tena, ilirejea katika jamii ya Ulaya kuanzia mwaka  wa 1990. Kohl alilitathmini bara la Ulaya  kuwa  ni jukumu la Ujerumani. Na kwa ajili hiyo  aliipigania sarafu ya Euro kwa nguvu  zake zote, kwa lengo la kuhakikisha kwamba  mchakato wa kuujenga Umoja wa Ulaya  haurudi nyuma. Aliweka shinikizo ili nchi  za  Ulaya Mashariki ziingizwe katika Umoja huo, licha ya changamoto kubwa kwa jumuiya.

Helmut Kohl ataendelea kukumbukwa

Yeye siyo sawa na Willy Brandt,  mwanasiasa aliekuwa na  uwezo wa kuona mbali  na  wala yeye hawezi kufananishwa  na Helmut Schmidt, mtaalamu  wa  uchumi. Kohl alikuwa Mjerumani lakini  zaidi alikuwa mwanaulaya mkubwa.

Kohl alikuwa kansela aliyekaa muda mrefu zaidi madarakani baada ya Vita vya Pili vya Dunia, akihudumu kutoka mwaka 1982 hadi 1998 na akihusika moja kwa moja na kuanzishwa kwa sarafu ya pamoja ya bara la Ulaya, Euro. 
 

 

Mwandishi:Wagener, Volker

Mfasiriri:Mtullya Abdu.

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman
         

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com