1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Merkel atunukiwa tuzo ya Fulbright

Oumilkheir Hamidou
29 Januari 2019

Wakfu maarufu wa Fulbright wa Marekani umemtunukia kansela Angela Merkel tuzo ya Fulbright kwa mwaka 2018 kutokana na juhudi zake za kupigania amani, hali ya kuelewana katika jamii na ushirikiano wa kimataifa.

https://p.dw.com/p/3CML6
Berlin: Merkel erhält amerikanischen Fulbright-Preis
Picha: picture-alliance/dpa/W. Kumm

Sherehe za kutunikwa tuzo ya shirika lenye makao yake mjini Washington la Fulbright zimefanyika kwa mara ya kwanza nje ya Marekani. Miongoni mwa waliohudhuria sherehe hizo ni pamoja na balozi wa Marekani mjini Berlin , mkosoaji mkubwa wa kansela, Grenell. Shirika hilo limesifu uongozi wake unaostahiki kuigwa, na juhudi zake za kupigania hali ya kuelewana, ushiriikiano wa kimataifa na amani."

Kansela Angela Merkel
Kansela Angela MerkelPicha: picture-alliance/dpa/W. Kumm

Katika hotuba yake, kansela Merkel ametilia mkazo umuhimu wa ushirikiano katika kupambana na kuongezeka hisia za uzalendo na kujipendelea, akiutaja mchango wa Marekani baada ya vita vikuu vya pili vya dunia katika kusaidia kurejesha uhuru na demokrasia nchini Ujerumani na Ulaya magharibi.

Jukumu la kulinda  uhuru na amani

"Tunabidi tuwajibike kuhakikisha amani inaendelea kuwepo.Tunastahiki kushukuru kwamba katika nchi zetu bado tunajivunia uhuru na amani. Lakini tusipakate mikono tunabidi tuwajibike zaidi na kuwa macho kuangalia yanayotokea katika jamii ndani na nje ya nchi zetu."Amesema kansela Merkel

Bila ya kuutaja kwa jina usemi wa rais wa Marekani Donald Trump- Amerika Kwanza au mvutano kuhusiana na sera zake za kibiashara na masuala mengine kadhaa, kansela Merkel amekosoa hisia za kujipendelea na kusema,"Uzalendo  kwangu mie unamaanisha kufikiria masilahi ya kibinafsi pamoja na yale ya wengine. Na ndio maana sitochoka kila mara kutilia mkazo umuhimu wa kuimarishwa maadili na mwongozo wa dunia unaotilia maanani ushirikianao wa pande tofauti.

Kansela Merkel akipokea tuzo ya Fulbright
Kansela Merkel akipokea tuzo ya FulbrightPicha: picture-alliance/dpa/W. Kumm

 Merkel aingia katika madaftari ya historia

Kansela Angela Merkel ameingia katika madaftari ya historia kuwa miongoni mwa

 viongozi mashuhuri waliotunukiwa tuzo hiyo, wakiwemo Jimmy Carter wa Marekani, Vaclav Havel  wa jamhuri ya Cheki na Nelson Mandela wa Afrika Kusini.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/dpa

Mhariri: Iddi Ssessanga