Jumuiya ya Usalama na Ushirikiano barani Ulaya kuimarishwa | Matukio ya Kisiasa | DW | 02.12.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Jumuiya ya Usalama na Ushirikiano barani Ulaya kuimarishwa

Nchi wanachama wa Jumuiya ya Usalama na Ushirikiano barani Ulaya, zimekubaliana kwenye mkutano wao mjini Astana, Kazakhstan, kuiimarisha jumuiya hiyo kuwa jukwaa la usalama na mdahalo kwa bara la Ulaya, Amerika na Asia

default

Rais wa Kazakhstan Nursultan Nasarbajev (kushoto) akisalimiana na waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Hillary Clinton

Kwenye mkutano wake wa kwanza katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja, jumuiya ya usalama na ushirikiano barani Ulaya, imejaribu kutafuta makubaliano kuhusu mkakati utakaoimarisha uwezo wake wa kuzuia mizozo. Viongozi wa dunia wanaokutana mjini Astana, Kasakhstan wamekiri kuwa uwezo wa jumuiya hiyo kutimiza malengo yake katika kuzuia mizozo barani Ulaya na katika muungano wa zamani wa Sovieti, umepungua katika miaka ya hivi karibuni.

Jumuiya ya Usalama na Ushirikiano barani Ulaya na uhodari wake kama msuhishi ni muhimu, amesema katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon. Bwana Ban anautazama mzozo wa Kirgistan kama mfano mzuri wa mafanikio katika kukabiliana na mizozo na ushirikiano mzuri wa pamoja. Amesema Umoja wa Mataifa, jumuiya ya Usalama na Ushirikiano barani Ulaya, Umoja wa Ulaya na mashirika mengine yaliungana kutoa msaada kwa watu wa Kirgistan wakati nchi hiyo ilipokumbwa na matatizo.

Ban aidha amesema, "Nchini Afghanistan tunakabiliwa na mtihani mwingine. Tunahitaji kushirikiana kikamilifu kuhakikisha mchakato wa mageuzi unakuwa imara na kudumu kwa muda mrefu. Ili kujenga taasisi imara tunahitaji kuisaidia Afghanistan kwa kipindi kirefu, na Umoja wa Mataifa ungependa jumuiya ya usalama na ushirikiano barani Ulaya iwajibike zaidi."

Ban Ki-moon, neuer UN-Generalsekretär

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon

Kauli ya Ban Ki Moon bila shaka imemfurahisha waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani, Hillary Clinton, kwani hata Marekani ingependa kuona jumuiya ya Usalama na Ushirikiano ya Ulaya iliyo imara nchini Afghanistan. Akiuhutubia mkutano wa jumuiya hiyo mjini Astana, Bi Clinton alizungumzia vita kati ya Georgia na Urusi mnamo mwaka 2008 kuhusu majimbo yaliyojitenga na Georgia, ya Abkhazia na Ossetia Kusini, akisema jumuiya ya Usalama na Ushirikiano barani Ulaya inahitajika pia nchini Georgia. Bi Clinton alikuwa na maana ya kupelekwa kwa waangalizi wa kimataifa katika majimbo hayo.

Mzozo kuhusu majimbo ya Abkhazia na Ossetia Kusini, na mizozo mingine katika himaya ya jumuiya ya Usalama na Ushirikiano barani Ulaya, ilijadiliwa katika mkutano wa mjini Astana. Bi Clinton ametaka mizozo hiyo itafutiwe ufumbuzi.

"Mzozo wa eneo hili na hatari zilizopo kati ya mataifa, zinatishia watu wetu. Mifumo ya kidemokrasia inakabiliwa na shinikizo na mizozo inakuwa vigumu kuisuluhisha. Kwa hiyo tumekutana wakati ambapo jumuiya ya Usalama na Ushirikiano ya Ulaya inaweza tu kuwa na umuhimu ikiwa mataifa yanayoshiriki yataunga mkono taasisi zao katika misingi ya kisiasa."

Kwa kansela wa Ujerumani Angela Merkel mzozo wa eneo la Caucasus ulikuwa mtihani mkubwa kwa jumuiya ya usalama na ushirikiano barani Ulaya. Amesema wakati wa vita vya mwaka 2008 kati ya Georgia na Urusi kulikuwa na mzozo mkubwa wa nchi wanachama kutoaminiana, lakini sasa chembe ya matumaini imechomoza na wanawaza kufurahi kwamba mzozo huo uliweza kutanzuliwa na leo wanaweza kusema hatua mpya zimepigwa katika kujenga tena uaminifu.

"Nadhani ushirikiano unaoshuhudiwa katika jumuiya hii unaonyesha ni kiasi gani cha uaminifu tunachopaswa kuwa nacho miongoni mwetu."

Rais wa Kazakhstan, Nursultan Nazarbayev, ambaye nchi yake inashikilia uenyekiti wa jumuiya ya Usalama na Ushirikiano barani Ulaya, amesema ana matumaini kwamba viongozi watakubaliana kuhusu taarifa ya pamoja na kusuluhisha tofauti zao. Mkutano wa jumuiya hiyo unatarajiwa kumalizika leo.

Mwandishi: Broders, Esther (DP)

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com