Jukumu la Marekani katika jumuiya ya NATO | Matukio ya Kisiasa | DW | 03.04.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Jukumu la Marekani katika jumuiya ya NATO

Marekani yauhitaji Ulaya katika jumuiya ya NATO

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel (kushoto) na rais wa Marekani Barack Obama wakikagua gwaride la heshima mjini Baden-Baden Ujerumani

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel (kushoto) na rais wa Marekani Barack Obama wakikagua gwaride la heshima mjini Baden-Baden Ujerumani

Wakati wa vita baridi uwanachama wa Marekani katika jumuiya ya NATO ulikuwa kama bima ya maisha kwa nchi za Ulaya.Kama muungano wa zamani wa Sovieti ungeishambulia nchi yeyote ya Ulaya, Marekani ingetoa msaada wake. Lakini hata baada Sovieti ya amani kuvunjika, jumuiya NATO imeendelea kuwepo. Na Marekani nayo imeendelea kuwa imara katika jumuiya hiyo.

Bwana Nile Gardiner wa wakfu wa kikonsavativ ya Heritage nchini Marekani anasema jumuiya ya kujihami ya NATO ni chombo muhimu sana kwa Marekani katika juhudi zake za kulinda maslahi ya usalama ya Marekani katika bara la Ulaya.

Wakati huo huo uanachama wa Marekani katika jumuiya ya NATO ni thabiti katika kuendeleza kuwepo kwa ushirikiano huu, anasema mshauri huyu wa zamani wa waziri mkuu wa Uingereza, Margret Thatcher.

"Bila shaka Marekani inabakia taifa lenye nguvu duniani. Inatumia kiwango kikubwa mno cha fedha katika ulinzi wake asilimia 3.6 ya pato jumla la kitaifa, ikilinganishwa na Ulaya ambayo inatumia kati ya asilimia 1.7 na 1.8. Kwa hiyo Marekani ina ushawishi mkubwa katika jumuiya ya NATO na inachukua uongozi katika operesheni za Afghanistan. Lakini Marekani inawatazamia washirika wake pamoja na Ujerumani kuchukua jukumu kubwa katika operesheni za NATO Afghanistan na kwingineko."

Ulaya ina ushawishi katika NATO

Lakini pia Ulaya imeanza kuwa na ushawishi mkubwa katika jumuiya ya NATO. Hoja kuwa NATO imeundwa na taifa moja lenye nguvu pamoja na vibaraka 27 sio ukweli, anasema Stephen Larrabee wa shirika la RAND lililoko Washington, ambalo huishauri serikali ya Marekani katika maswala ya usalama.

Aidha kiongozi huyo amesema na hapa namnukulu, "Unapofikiria juu ya mkutano wa NATO wa hapo awali uliofanyika Bucharest, nchini Romania, Marekani na Rais Bush walipendekeza mipango ya kuzifanya Ukraine na Georgia ziwe wanachama. Ujerumani, Ufaransa na washirika wengine wasio na ushawishi mkubwa waliweza kuzuia mapendekezo haya. Naweza kusema washirika hawa wana pia jukumu muhimu, " mwisho wa kumnukulu kiongozi huyo.

Hata hivyo umuhimu huu hauonekani katika juhudi zinazoendelea huko Afghanistan. Marekani ndio yenye kisosi kikubwa cha majeshi. Na baada ya Marekani kuongeza vikosi vyake kama vile Rais Obama alivyosema, Marekani itakuwa na vikosi mara mbili zaidi ya vikosi vyote vya nchi nyingine za NATO kwa jumla.

"Lakini sio kwamba Marekani inataka, ila ni kwa sababu Wazungu hawako tayari kutoa wanajeshi. Sio kwamba Marekani inataka kudhibiti jumuiya ya NATO kwa kutuma wanajeshi. Marekani itafurahi ikiwa Wazungu watatuma wanajeshi mara mbili au mara tatu kuliko Marekani."

Serikali mpya ya Marekani imeridhika na msimamo wa Ulaya kwamba nchi hizi hazitaki kutuma vikosi vyao Afghanistan na Marekani imewacha kuitisha vikosi kutoka jumuiya ya NATO. Katika hotuba yake kuhusu mpango mpya wa Marekani nchini Afghanistan, rais wa Marekani, Barack Obama, alisema kabla mkutano wa NATO anataka nchi washirika zisaidie katika juhudi nchini Afghanistan.

"Kutoka kwa washirika wetu wa NATO hatutaomba tu vikosi, lakini pia maelezo kuhusu juhudi zao za kusaidia uchaguzi wa Afghanistan, kutoa mafunzo kwa vikosi vya usalama vya Afghanistan na kujitolea zaidi kwa umma wa Afghanistan."

Lakini mzigo huo unapokuwa haujagawanya sawa sawa jumuiya ya NATO itagawanyika katika vikundi viwili. Waziri wa ulinzi wa Marekani bwana Robert Gates ametoa malalamiko na onyo kuhusu hali hio.

Kuna nchi nyingine chache zikiwepo Marekani, Canada na Denmark ambazo vikosi vyao vinakabiliwa na hatari kubwa zaidi kuliko vikosi vya nchi nyingine. Hii inasababisha kutokuwepo na usawala katika kugawa majukumu lakini hiyo ndiyo jumuiya ya NATO tuliyonayo na tunalazimika kuikubali jinsi ilivyo.

Ulaya yaunda sera za usalama

Wakati huo huo Ulaya iko katika hali ya kuunda sera zake za usalama chini ya mwavuli wa Umoja wa Ulaya pamoja na nchi ambazo sio wanachama wa jumuiya ya NATO. Sera hizi hazitapingana na NATO bali kutakuwa na uwiano.

Wajibu wa NATO utakapobadilika, bado jumuiya hii itakuwa na umuhimu wake. Marekani inaitazama NATO kuwa yenye umuhimu mkubwa kwani wakati wa utawala wa rais Bush kwa vile Marekani ilitoa fedha nyingi kuliko nchi zingine za NATO katika maswala ya usalama, haikuhitaji mshirika.

Lakini hali hii ilibadilika baada ya matatizo kutokea nchini Irak, Afghanistan na pia kuzuka mgogoro wa kiuchumi ulimwenguni ambao ulithibitisha kuwa Marekani inahitaji mshirika.

 • Tarehe 03.04.2009
 • Mwandishi Charo Josephat/Bergmann
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/HPkx
 • Tarehe 03.04.2009
 • Mwandishi Charo Josephat/Bergmann
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/HPkx
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com