Juhudi za kutafuta amani katika Libya zinapata kasi | Matukio ya Kisiasa | DW | 05.07.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Juhudi za kutafuta amani katika Libya zinapata kasi

Utafutaji wa suluhisho la amani kwa vita vya Libya kwa ukimya unapata kasi, licha ya matamshi ya ubabe yanayotolewa na Muammar Gaddafi na mahasimu wake wanaoasi.

default

Kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi, yuko mashakani.

Pande zote mbili zikiashiria kwamba zinaweza kuendelea kupigana. Kwa sehemu, hisia za kutaka kuharakishwa juhudi za kutafuta amani nyuma ya mapazia, zinatokana tu na idadi ya matamshi yanayotolewa na wapiganaji.

Zaidi anayo Othman Miraji ...

Wao wanahimiza kuweko suluhisho, licha ya kwamba matamshi hayo baadhi ya nyakati yanakuwa makali na yanapingana. Wachunguzi wa mambo wanashuku kwamba mapatano yako njiani kutayarishwa, na tetesi hizo zimepata makali kutokana na mazungumzo yasiokuwa rasmi yanayotaja kwamba waasi wamepunguza baadhi ya operesheni zao dhidi ya Gaddafi kama mbinu ya kijeshi ya muda mfupi, au huenda kuyawezesha mashauriano yafanyike.

Na watu wengine wanasema waranti wa kukamatwa Muammar Gaddafi iliotolewa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa vita huko The Hague imechochea kutafutwa mapatano kwa kuzipa nchi za magharibi huenda ikawa ni karata mpya, aina ya kama kumpa msamaha Gaddafi naye akubali kuondoka kutoka kwenye madaraka. Oliver Miles, balozi wa zamani wa Uengereza nchini Libya, amesema hisia ni kwamba watu hawako mbali kuona kumalizika mchezo huu wa vita. Mwandishi wa habari wa Ki-Libya anayesihi Uingereza amesema bila ya shaka kuna kitu kinachofanyika, akiashiria  imani yake kwamba juhudi za kisiasa zimeongezwa. Alisema hivi sasa kunafanyika juhudi zaidi za kuyakamilisha mambo na kuepusha kutokea mapambano ya kisilaha huko Tripoli ambayo yatakuwa ya mabaya sana.

Gaddafi ameikataa miito ya kimataifa inayomtaka aondoke madarakani, na amesema atapigana hadi mwisho, lakini watu wanaomzunguka na walio karibu sana naye wametoa ishara kwamba wao wako tayari kufanya mashauriano na waasi, pamoja  na kuzungumzia juu ya  hali ya baadae ya kisiasa ya kiongozi huyo.

Libyen Kämpfe Rebellen

Mpiganaji wa waasi wa Libya yumo kwenye mapambano ya vita

Kiongozi wa waasi, Mustafa Abdel Jalil, alisema jumapili iliopita kwamba Gaddafi anakaribishwa kuishi Libya wakati akistaafu, ikiwa ataachana na madaraka yote. Lakini siku ya jumatatu, Jalil alitoa taarifa akisema kwamba anataka kuweka wazi kwamba hakuna uwezekano kwa Gaddafi kubakia Libya, na itabidi akabiliane na mashtaka. Pia Jalil alisema hakujakuweko mashauriano na utawala wa Gaddafi. Lakini utawala huo ulisema umekuwa na mikutano katika miji mkuu ya nchi za kigeni na wawakilishi wa waasi kushauriana juu ya amani.

Hata hivyo, kuna wachambuzi  ambao wanasema Gaddafi yu tayari kuacha madaraka, lakini kwa masharti fulani. Na kati ya hayo masharti ni yeye aweze kubakia Libya bila ya kushtakiwa na kwamba anataka mwanawe wa kiume, anayewakilisha makabila yanayouunga mkono utawala wake, awe sehemu ya Libya ya siku za mbele. Huo ndio mpango wake, ni kama bima yake. Anaamini kwamba siku za mbele pindi patafanywa uchaguzi, yeye na familia yake watapata ulinzi kutoka makabila ambayo yanamuunga mkono sasa. Lakini wachunguzi wengi wa mambo wanasema Gaddafi atakuwa mpumbavu asilikubali azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litakaloungwa mkono kimataifa na ambalo litampa msamaha kutoka mahakama ya kimataifa, na badala yake yeye akubali aachae madaraka, na atoe mwito kwa watu wake waweke chini silaha.

Lakini mapatumaini ya kufikiwa mapatano ya aina hiyo ni madogo.

Wakati huo huo, serekali ya Gaddafi iko katika kujitayarisha na mwezi wa mfungo wa Ramadhan amabo utakuwa ni mtihani kwa mali zake zinazopunguwa. Kwani lazima serikali hiyo ipate vyakula vya kutosha na mafuta kuyawezesha maeneo yanayoshikiliwa na serekali kuwa na sherehe za familia wakati wa Ramadhan na sikukuu.

Mwandishi: Miraji Othman/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdulrahman

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com